Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti iko chini ya vikwazo vya silaha vya UN: Kwa nini kuna salaha haramu 500,000 zikisambaa?

Washiriki wa magenge wakitoa silaha zao katika kitongoji cha Delmas 3 katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.
Giles Clarke
Washiriki wa magenge wakitoa silaha zao katika kitongoji cha Delmas 3 katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.

Haiti iko chini ya vikwazo vya silaha vya UN: Kwa nini kuna salaha haramu 500,000 zikisambaa?

Amani na Usalama

Inakadiriwa kuwa hadi bunduki haramu 500,000, kuanzia bastola hadi bunduki za automatiki za kivita, ziko mikononi mwa magenge nchini Haiti, ingawa nchi hiyo ya Karibea imekuwa chini ya vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Haiti inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa usalama huku magenge pinzani ya uhalifu yakipigania udhibiti wa mji mkuu Port-au-Prince na maeneo yanayouzunguka, yakitisha jamii kupitia vitendo vya unyang’anyi, ubakaji, utekaji nyara kwa ajili ya fidia, na mauaji.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walikubaliana kuweka marufuku ya silaha dhidi ya Haiti mwaka 2022 basi nini kimeenda mrama? Hapa kuna mambo matano muhimu ya kujua:

1. Ni silaha ngapi zipo Haiti?

Haiti haitengenezi silaha wala risasi, lakini kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, inakadiriwa kuwa kati ya silaha haramu 270,000 na 500,000 zipo katika mzunguko nchini humo.

Haziko tu mikononi mwa magenge yanayofanya mauaji mengi yanayodhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu, bali pia zimeenea miongoni mwa vikundi vya ulinzi vya kiraia vinavyojaribu kulinda watu na mali katika mitaa yenye vurugu ya Port-au-Prince.

Athari ya wingi huu wa silaha katika eneo lenye wakazi takribani milioni 2.6 ni kubwa.

Mwaka 2024 pekee, zaidi ya watu 5,600 waliuawa kutokana na shughuli za magenge ya uhalifu, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Katika siku tano za mwanzo wa Desemba 2024, takriban watu 207 waliuawa na magenge yaliyokuwa yakidhibiti eneo la Wharf Jérémie mjini humo.

Maelfu ya watu wameuawa nchini Haiti kutokana na vita vya magenge.
© UNOCHA/Giles Clarke
Maelfu ya watu wameuawa nchini Haiti kutokana na vita vya magenge.

Mashambulizi ya magenge yamesababisha maelfu ya vifo nchini Haiti. Ukiukaji wa haki za binadamu uliorekodiwa na Umoja wa Mataifa unajumuisha mauaji ya halaiki, utekaji nyara kwa fidia, ubakaji, ukatili wa kijinsia, uharibifu wa mali, na vizuizi vya upatikanaji wa huduma muhimu kama afya na elimu.

2. Ni aina gani za silaha zinazozunguka?

Ni vigumu kukadiria kwa usahihi idadi ya silaha haramu mikononi mwa magenge na vikundi vya ulinzi, lakini kuna viashiria vya matumizi ya silaha za kisasa zaidi na hatari zaidi.

Mamlaka za Haiti zimekuwa na mafanikio madogo kuzuia mtiririko wa silaha. Usafirishaji mmoja wa silaha uliopatikana Miami, Marekani, na kukamatwa Jamhuri ya Dominika Februari 2025, ulijumuisha bunduki nzito ya Barret M82 nusu-otomatiki, bunduki za walenga shabaha, bastola ya uzi, na zaidi ya risasi 36,000.

Mwanamume mmoja anatibiwa majeraha mabaya ya moto hospitalini baada ya magenge kushambulia na kusababisha moto katika kituo cha mafuta alichokuwa akifanya kazi.
© UNOCHA/Giles Clarke
Mwanamume mmoja anatibiwa majeraha mabaya ya moto hospitalini baada ya magenge kushambulia na kusababisha moto katika kituo cha mafuta alichokuwa akifanya kazi.

3. Marufuku hiyo ya silaha inasema nini?

Marufuku ya silaha, pamoja na vikwazo vya kusafiri na kufungia mali, viliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Oktoba 2022.

Vililenga magenge na watu binafsi wanaohusishwa na kuhatarisha amani na usalama wa Haiti.

Inazitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kupiga marufuku usambazaji, uuzaji au uhamishaji wa silaha na vifaa vyote vinavyohusiana, ikiwemo msaada wa kiufundi, mafunzo na msaada wa kifedha unaohusiana na shughuli za kijeshi.

Azimio hilo linatambua kwamba hali nchini Haiti inahatarisha amani ya kikanda.

4. Marufuku hiyo inakwepwa vipi?

Njia za usafirishaji haramu kutoka Marekani, hasa kutokea Miami na pia kutoka New York kupitia Jamhuri ya Dominika zinaendelea kutumiwa vibaya kutokana na udhaifu wa ukaguzi wa forodha na rushwa.

Baadhi ya mizigo hukamatwa na mamlaka za Marekani kabla haijafika Haiti.
Kuna pia ushahidi wa silaha kupelekwa kutoka Venezuela na nchi nyingine za Amerika Kusini.

Silaha nyingi hufichwa ndani ya mizigo iliyochanganywa au kutangazwa kama mizigo ya misaada ya kibinadamu au ya kibiashara ili kuepuka ukaguzi.

Kuna wasiwasi pia kwamba bunduki za kivita ambazo awali zilisajiliwa kwa kampuni binafsi za ulinzi zinazofanya kazi Haiti sasa zinajikuta mikononi mwa wanamgambo wa magenge ya uhalifu.

Silaha zilizokamatwa na mamlaka za kutekeleza sheria za Marekani ambazo zilipelekwa Haiti zinaonyeshwa.
© CPB/HSI
Silaha zilizokamatwa na mamlaka za kutekeleza sheria za Marekani ambazo zilipelekwa Haiti zinaonyeshwa.

5. Nini kifanyike kuhakikisha marufuku inazingatiwa, na UN inasaidiaje?

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na Dawa na Uhalifu (UNODC), inayoshughulika na masuala ya usafirishaji haramu, imesema utekelezaji wa marufuku hiyo unahitaji mbinu ya kina na ya pamoja katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Hii inamaanisha kuwapatia maafisa wa forodha, bandari na udhibiti wa mipaka nchini Haiti uwezo wa kiufundi wa kugundua na kuchunguza usafirishaji wa silaha haramu.

Kwa sasa, hakuna hata skana moja kubwa nchini Haiti inayoweza kutambua kwa ufanisi yaliyomo kwenye kontena au malori.

Kwa kuwa silaha nyingi huingia kupitia njia za baharini, ni muhimu kuboresha usalama wa bandari na ukaguzi wa mizigo, sambamba na ushirikiano bora na mamlaka za nchi ambako silaha hutoka.

Watu wanakimbia kitongoji cha Solino huko Port-au-Prince kufuatia mashambulizi ya magenge huko Mei 2024.
© UNICEF/Ralph Tedy Erol
Watu wanakimbia kitongoji cha Solino huko Port-au-Prince kufuatia mashambulizi ya magenge huko Mei 2024.

Kuimarisha ulinzi katika mpaka usio rasmi na Jamhuri ya Dominika, ambayo inashiriki kisiwa cha Hispaniola na Haiti, kutasaidia pia kudhibiti usafirishaji haramu.

Umoja wa Mataifa unasaidia kuratibu juhudi kati ya Haiti na nchi jirani, kuhakikisha utekelezaji wa marufuku, na kutoa msaada wa kiufundi kuboresha ufuatiliaji wa silaha, udhibiti wa forodha na uchunguzi wa kifedha.

UNODC imesema Kupambana na rushwa na mtiririko haramu wa fedha ni jambo la msingi katika kuhakikisha marufuku inazingatiwa,

Ofisi hiyo imeongeza kuwa “Kwa kuwa Haiti haitengenezi silaha wala risasi, kukata usambazaji wa risasi pekee kunaweza kumaliza uwezo wa magenge kupigana na kutishia jamii.”