UNICEF yalaani shambulio lililoua watoto 17 Kaskazini mwa Darfur Sudan
UNICEF yalaani shambulio lililoua watoto 17 Kaskazini mwa Darfur Sudan
Watoto wasiopungua 17 wasichana tisa na wavulana wanane, akiwemo mtoto mchanga wa siku saba wameuawa katika shambulio lililotokea katika kituo cha wakimbizi wa ndani cha Dar al-Arqam mjini El Fasher, Kaskazini mwa Darfur, mapema Jumamosi asubuhi, kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.
Watoto wengine 21 wanaripotiwa kujeruhiwa katika shambuio hilo la kikatili.
Kwa mujibu wa UNICEF kituo hicho kilikuwa kikihifadhi familia ambazo tayari zilikuwa zimeyakimbia makazi yao kutokana na vita vinavyoendelea nchini Sudan.
“Shambulio hili la kusikitisha dhidi ya watoto na familia ambazo tayari zimekimbia na kusaka usalama ni jambo la kushtua,” amesema Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.
Ameongeza kuwa “Kuwaua na kuwajeruhi watoto ni ukiukaji mkubwa wa haki zao, na mashambulio dhidi ya raia katika maeneo yanayokusudiwa kutoa hifadhi ni jambo lisilokubalika kabisa.”
El-Fasher chini ya mzingiro wa RSF
Mji wa El Fasher, makao makuu ya Kaskazini mwa Darfur, umekuwa chini ya mzingiro wa Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF kwa zaidi ya siku 500, hali iliyosababisha raia kukosa chakula, maji na huduma za matibabu.
Hali ya kibinadamu imezidi kuwa mbaya kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara na ukosefu wa mahitaji muhimu.
Kwa mujibu wa UNICEF, maeneo kadhaa ya Kaskazini mwa Darfur yamekuwa yakikabiliwa na baa la njaa kwa miezi kadhaa, na hali ya lishe duni kwa watoto imefikia kiwango cha janga.
Familia nyingi zinajikimu kwa posho ndogo mno, huku vituo vya afya vikiripoti vifo vingi vya watoto vinavyotokana na njaa na magonjwa yanayoweza kuzuilika. Uharibifu wa njia za usambazaji, uporaji wa misafara ya misaada, na vizuizi vya ufikiaji wa kibinadamu vimeifanya kazi ya kutoa misaada kuwa ngumu na karibu kutowezekana.
UNICEF imerejelea wito wake wa haraka kwa:
- Kusitishwa mara moja kwa mapigano kote nchini Sudan na kuondolewa kwa mzingiro wa El Fasher.
- Kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwemo kulinda raia na miundombinu ya kiraia.
- Kupitishwa kwa usalama kwa watoto na familia zinazokimbia vurugu.
- Upatikanaji salama na usiokatizwa wa misaada ya kibinadamu kwa jamii zilizoathirika.
- Kuwawajibisha waliohusika na mashambulio dhidi ya raia, hususan watoto.
Licha ya changamoto za usalama na ufikiaji wa waathirika, UNICEF na washirika wake wanaendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha, ikiwemo huduma za afya, lishe, maji safi na usafi wa mazingira kwa watoto kote Sudan.
“Watoto nchini Sudan wamepitia mateso yasiyoelezeka,” ameongeza Russell. “Wanastahili amani, ulinzi, na fursa ya kuishi na kustawi.”
Rais 57 wauawa ndani ya siku mbili: OCHA