Je, AI inaweza kujenga mustakabali wa haki zaidi kwa watu wenye ulemavu?
Picstry AI inabadili picha binaffsi kuwa kumbukumbu ya sauti, iikijumuisha majina, uhusiano na matukio
Je, AI inaweza kujenga mustakabali wa haki zaidi kwa watu wenye ulemavu?
Na Na Anshu Sharma
Afya Kwa mamilioni ya watu wanaoishi na ulemavu duniani kote, akili Mnemba (AI) inaweza kuwa chachu ya mabadiliko makubwa.
Katika tamasha la Purple Fest huko Goa, nchini India, wajasiriamali wanaonesha jinsi AI inavyogeuza teknolojia saidizi kuwa nguvu ya uwezeshaji wa kila siku.
Ikiwa imeundwa kwa kuzingatia uzoefu halisi wa maisha, zana za AI kama wasomaji wa skrini wenye uwezo wa mazungumzo, dashibodi zinazobadilika, na maandiko ya papo kwa papo ya video, haziwezi tu kuondoa vikwazo bali pia zinaweza kupanua upeo wa uwezekano.
Zinageuza upatikanaji wa fursa hizo kuwa mamlaka na uhuru wa kujifunza, kuongoza na kuchangia kikamilifu.
Kuepuka upendeleo uliokita mizizi
Surashree Rahane alizaliwa na ulemavu kadhaa wa kimwili, ukiwemo kupinda miguu au club foot na polymelia hali ambayo mtu huzaliwa akiwa na viungo vya ziada.
Alikua katika familia ambayo ulemavu ulikuwa sehemu ya maisha ya kila siku, na hakuwahi kuuona kama kizuizi, bali njia tofauti tu ya kuishi duniani.
“Walimu wangu walinifundisha kwamba usitafute tu ajira, bali tengeneza ajira,” anasema. “Ndipo nilipojifunza kwamba uongozi wenyewe ni ujumuishaji.”
Bi. Rahane sasa ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Yearbook Canvas, jukwaa la kiteknolojia lililobobea katika utengenezaji wa vitabu vya kumbukumbu vya kidijitali kwa taasisi za elimu.
Alipokuwa akijenga kampuni yake, aliona jinsi vikwazo vya kimfumo kama miundombinu isiyofikika, mitandao ya ufadhili yenye upendeleo, na mifumo migumu ya elimu, vinavyoendelea kuwepo.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, kwa sasa anashirikiana na Newton School of Technology karibu na New Delhi, akilenga kubuni mitaala jumuishi na zana za ujifunzaji za AI zinazobadilika kulingana na kasi ya mwanafunzi.
“AI inaweza kusambaza elimu kwa usawa,” anasema, “lakini ni lazima tuifundishe kuelewa wanafunzi wenye utofauti. Vinginevyo, tutaunda toleo jipya lenye upendeleo uleule wa zamani.”
Teknolojia saidizi zinawawezesha watu wenye ulemavu
AI inaondoa vizuizi
Kuanzia zana za kubadilisha sauti kuwa maandishi kwa watu wenye ulemavu wa kutosema, hadi viti mwendo vinavyodhibitiwa kwa ishara za mikono, teknolojia sasa inavunja vizuizi ambavyo hapo awali vilionekana kuwa vya kudumu.
Prateek Madhav, Mkurugenzi Mtendaji wa AssisTech Foundation (ATF), anaielezea AI kama msawazishaji mkuu.
Wakati dunia inahofia AI kuchukua ajira, anasema, “kwa watu wenye ulemavu, AI inazalisha ajira.”
AI imegeuza mawazo kuwa vitendo
Ketan Kothari, mshauri katika Xavier’s Resource Centre for the Visually Challenged huko Mumbai, anaonesha jinsi zana za AI zimemfanya awe huru kikamilifu kazini.
“Leo ninaweza kupanga hati, kushiriki mikutano yenye maandiko ya moja kwa moja, na hata kupata maelezo ya picha kupitia programu,” anaeleza. “AI imegeuza mawazo kuwa matendo.”
Tamasha la Purple Fest linaleta hasa wajasiriamali na viongozi wa biashara kutoka India, lakini kama anavyoeleza Tshering Dema kutoka Ofisi ya Uratibu wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDCO) “Hii si hadithi ya nchi moja pekee ni mabadiliko ya kimataifa.
Ujumuishaji si kuhusu sheria au miundombinu pekee, ni kuhusu mtazamo na ubunifu wa pamoja.
Mustakabali wa ajira lazima ujengwe si kwa ajili ya watu tu, bali pamoja nao.”
Roboti Maria kushoto na Estevão kulia washindi wa shinano la roboti kwa ajili ya mema kwa vijana 2025
Tamasha la Kimataifa la Purple Fest
- UN News imezungumza na wajasiriamali wa kijamii na maafisa wa Umoja wa Mataifa katika International Purple Fest, tukio la kimataifa linalochagiza ujumuishaji na upatikanaji wa fursa, lililofanyika Goa, India, kati ya tarehe 9 na 12 Oktoba.
- Purple Fest huandaliwa na Idara ya Uwezeshaji wa Watu Wenye Ulemavu ya Goa na Ofisi ya Kamishna wa Jimbo la Watu Wenye Ulemavu, kwa ushirikiano na Wizara ya Haki ya Kijamii na Uwezeshaji ya India, pamoja na Umoja wa Mataifa nchini India.