Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Timu za UN zasisitiza wito wa kuingiza misaada Gaza bila vizuizi

Watoto huko Gaza wakisherehekea usitishaji mapigano.
© UNOCHA
Watoto huko Gaza wakisherehekea usitishaji mapigano.

Timu za UN zasisitiza wito wa kuingiza misaada Gaza bila vizuizi

Amani na Usalama

Wakati Wagaza waliokimbia makazi yao wakiwa wamefurika barabara kuu kuelekea eneo kaskazini leo Ijumaa baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas kuripotiwa kuanza kutekelezwa, timu za misaada ya kibinadamu za Umoja wa Mataifa zimerejea kusistiza wito wao wa kufungua mipaka yote kuelekea ukanda huo ulioharibiwa vibaya na vita ili kuzuia baa la njaa kusambaa.

“Kuna taarifa chache kuhusu maelezo au jinsi makubaliano haya yatazingatiwa. Hata hivyo, tunatoa wito mipaka yote ya Gaza ifunguliwe mara moja ili vifaa na misaada ya kibinadamu viingie katika ukanda huu ulioathirika na vita,” amesema Juliette Touma, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wapalestina, UNRWA.

Maelezo yake yametolewa huku vikosi vya Israel vikiripotiwa kujiondoa kutoka sehemu fulani za Gaza, kwa mujibu wa makubaliano kati ya Israel na Hamas, yaliyosuluhishwa Misri wiki hii na wasuluhishi wa Marekani pamoja na wawakilishi kutoka Qatar na Uturuki.

Wapalestina huko Gaza wanakaribisha usitishaji vita.
© UNOCHA
Wapalestina huko Gaza wanakaribisha usitishaji vita.

Kukabiliana na baa la njaa

“Hiki chakula kutoka UNRWA ni muhimu kwa kuzuia na kudhibiti baa la njaa,” Bi. Touma amesisitiza, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF likiashiria kuwa watoto 50,000 wako hatarini kutokana na utapiamlo mkali.

“Wanatakiwa kutibiwa mara moja kwa kusitisha mapigano, tunatarajia kuweza kupata matibabu ya dharura wanayohitaji kwa dharura,” amesema msemaji wa shirika hilo Ricardo Pires.

Afisa mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, amesisitiza jana Alhamisi kwamba “familia yote ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inajishughulisha kuhakikisha misaada inaingia Gaza.”

Akizungumza na waandishi wa habari, amesisitiza kuwa  “nafasi isiyoweza kuachwa ya UNRWA katika kusambaza vifaa vya msaada kote ukanda huu huku akionesha pia nafasi kuu iliyotolewa kwa Umoja wa Mataifa katika mpango wa vipendele 20 wa Rais wa Marekani, Donald Trump, ambao sasa unatekelezwa.”

Mgogoro unaoendelea

Timu za msaada zinazofanya kazi ndani ya ukanda huo zimeripoti kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano hayakuanza kutekelezwa mapema Ijumaa asubuhi.

Hata hivyo, kazi muhimu za kibinadamu zinaendelea, ikiwa ni pamoja na operesheni moja ya UNICEF kuelekea Jiji la Gaza Alhamisi “kuokoa watoto wawili waliokuwa kwenye incubators na kupigania maisha yao,” amesema Bwana Pires.

“Kwa bahati nzuri, kwa kazi ngumu ya wenzetu na wahudumu wa afya walioko mashinani, watoto hao walinusurika na leo wameunganishwa na familia zao.”

Msemaji wa UNICEF ameeleza kuwa operesheni hiyo ililazimika kusubiri saa 15 kupata ruhusa ya kuingia Jiji la Gaza kwa sababu “hali ilivyo mashinani ilikuwa bado haiko thabiti na kulikuwa na shughuli za mapigano na ghasia nyingi.”

Akithibitisha tathmini hiyo, Bi. Touma wa UNRWA amebainisha kuwa wenzake walioko ukanda huo wameripoti mashambulizi ya anga yaliendelea leo Ijumaa asubuhi.

Msemaji wa shirika hilo la la Umoja wa Mataifa pia amebainisha kuwa zaidi ya wafanyakazi 370 wa UNRWA wameuawa katika kipindi cha mgogoro uliozuka kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas kusini mwa Israel 7 Oktoba 2023. “Hii ni idadi kubwa zaidi ya vifo katika Umoja wa Mataifa tangu kuanzishwa kwake,” ameongeza.

Akijiunga na wito wa “ufiishaji wa msaada bila vizuizi kupitia njia zote zinazowezekana,” msemaji wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, Christian Lindmeier, amesisitiza “haja ya kuendelea na uhamishaji wa dharura wa kiafya kutoka Gaza kwenda Ukingo wa Magharibi ikiwa ni pamoja na Yerusalemu Mashariki, pamoja na ufadhili unaohitajika kuendeleza urejeaji.”

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yana tani 170,000 za chakula, dawa na vifaa vingine tayari kupelekwa Gaza.

Lengo ni kuongeza upatikanaji wa chakula kote Gaza kufikia watu milioni 2.1 na takriban watu 500,000 wanaohitaji msaada wa lishe.