Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel na Hamas zingatieni kikamilifu masharti ya mpango wa amani wa Marekani:Guterres

Umati wa Wapalestina washerehekea huko Deir el Balah, Gaza, baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kutekelezwa.
© UNRWA Watu wa Gaza wakisherehekea Deir el Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza (Kutoka Maktaba)

Israel na Hamas zingatieni kikamilifu masharti ya mpango wa amani wa Marekani:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kwamba Israel na Hamas wamekubali awamu ya kwanza ya mpango wake wa amani wenye vipengele 20, baada ya siku kadhaa za mazungumzo ya kina yasiyo ya moja kwa moja yaliyofanyika nchini Misri.

Katika taarifa yake iliyotolea mjini New York Marekani Jumatino suiku Katibu Mkuu António Guterres “amezitaka pande zote zinazohusika kuheshimu kikamilifu masharti ya makubaliano hayo, ikiwemo kuachiliwa kwa heshima kwa mateka wanaoshikiliwa Gaza kwa zaidi ya miaka miwili.”

Rais Donald Trump alitangaza kupitia mitandao ya kijamii Jumatano usiku kwamba Hamas imekubali kuwaachilia huru mateka wote walioko Gaza “Hivi karibuni kabisa, huku Israel ikikubali kuanza kuondoa vikosi vyake vya ardhini hatua kwa hatua hadi mstari ulioafikiwa.”

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari zikiinukuu Qatar, makubaliano hayo yanahusisha “masharti na taratibu za utekelezaji wa awamu ya kwanza itakayomaliza vita, kuachiliwa kwa mateka wa Kiyahudi na wafungwa wa Kipalestina, na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.”

Mwanamke na mtoto wa Kipalestina wakisherehekea usiku huko Gaza kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano.
© UNRWA Wapalestina Gaza wanasherehekea tangazo la makubaliano ya kusitisha mapigano.

Sifa kwa wapigania amani

“Nakaribisha tangazo la kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza, kulingana na pendekezo lililowasilishwa na Rais Donald J. Trump,” Guterres amesema katika taarifa yake.

Ameongeza kuwa “Naipongeza juhudi za kidiplomasia za Marekani, Qatar, Misri na Uturuki ambazo zimefanikisha hatua hii muhimu sana.”

Bwana Guterres amesisitiza umuhimu wa kufikiwa kwa usitishaji mapigano wa kudumu.

Kulingana na mpango wa Marekani, Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Hilali Nyekundu utasimamia uingizaji na usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

“Ni lazima kuruhusu mara moja na bila vizuizi misafara ya misaada yenye bidhaa muhimu na biashara kuingia Gaza. Mateso haya lazima yakome,” amesema Katibu Mkuu, akiahidi kuwa Umoja wa Mataifa utasaidia kutekeleza makubaliano hayo na kuongeza kiwango cha misaada ya kibinadamu, pamoja na juhudi za uokoaji na ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya na vita.

Mahema ya watu waliokimbia makazi yao yamejaa kando ya ukanda wa pwani wa Jiji la Gaza kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
UN News Mahema ya watu waliokimbia makazi yao yamejaa kwenye ukanda wa pwani wa Jiji la Gaza katika sehemu ya kaskazini ya Ukanda wa Gaza.

Kutumia fursa hii

Katibu Mkuu amewahimiza “wadau wote kutumia fursa hii ya kipekee kuweka njia ya kisiasa yenye uaminifu kuelekea kumaliza ukaliaji, kutambua haki ya Wapalestina ya kujitawala, na kuanzishwa kwa suluhy ya mataifa mawili itakalowawezesha Waisraeli na Wapalestina kuishi kwa amani na usalama.”

“Kamwe hatujawahi kuwa katika hali ya hatari zaidi ya sasa.” Amesema Guterres

Makubaliano hayo yanabainisha kuwa mabadilishano ya mateka yatafanyika ndani ya saa 72 baada ya kutiwa saini. Trump amesema anaamini kuwa mateka wote, walio hai na waliokufa, “watakuwa nyumbani ifikapo Jumatatu.”

Wakati huo huo, takriban malori 400 yenye misaada ya kibinadamu yataingia Gaza kila siku katika siku tano za kwanza za kusitisha mapigano, na idadi hiyo itaongezeka siku zinazofuata, kwa mujibu wa vyombo vya habari.

Kuhakikisha upatikanaji usio na 

Watoto waliokimbia makazi yao wakipanga foleni kwa ajili ya chakula cha moto katika jiko la jamii linaloendeshwa na Wakfu wa Usaidizi wa Kibinadamu wa IHH huko Deir al Balah, Gaza, Oktoba 2025.
UNOCHA/ Olga Cherevko Wasichana wadogo wanapokea chakula katika jiko la jumuiya huko Deir al Balah, Gaza.

Kizuizi wa Misaada

Akisisitiza umuhimu wa hatua hiyo, Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa “kuachiliwa kwa mateka na kuwasilishwa haraka kwa misaada ya kibinadamu.”

Kwa mujibu wa Tom Fletcher, mratibu wa masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura ambaye pia ni mkuu wa OCHA, timu zimejitayarisha kikamilifu kusafirisha malori kwa wingi na kuokoa maisha.

“Wanahitaji tu mazingira salama ya kufikia maeneo hayo. Tutawajulisha mara kwa mara,” amesema kwenye mtandao wake wa  X.

Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yameonya juu ya haja ya kupeleka misaada mara moja katika eneo la Gaza lililoathirika na njaa.

Katika mbio hizi dhidi ya muda, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema lina chakula, dawa na bidhaa nyingine muhimu tayari kupelekwa Gaza.

“Tunazo akiba za kutosha kulisha idadi yote ya watu kwa miezi mitatu ijayo,” almesema Kamishina Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini kupitia mtandao wa X.

Kwa upande wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, hitaji la dharura ni kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya chakula na bidhaa za kuokoa maisha bila vizuizi.

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain kwenye ukurasa wake w Xamesema

“WFP ipo ardhini na iko tayari kuongeza operesheni zake, lakini lazima tutende sasa hatuna muda wa kupoteza”

Kuongeza nguvu za uokoaji

Kwa upande wake Shirika la Afya la Umoja wa Maataifa Duniani (WHO) pia limeeleza kuwa liko tayari kuongeza jitihada za kukidhi mahitaji ya dharura ya kiafya kwa wagonjwa huko Gaza na kusaidia katika kurejesha mfumo wa afya uliobomolewa.

Hata hivyo, kwa shirika hilo la afya duniani, dawa bora zaidi ni amani. “Natumai pande zote zitaheshimu makubaliano haya ili mateso ya raia wote yaweze kumalizika, na mateka wote warejee nyumbani kwa heshima,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia mtandao wake wa X.

Kwa mujibu wa Ofisi ya WHO ya Kanda ya Mashariki ya Mediterania, zaidi ya dola bilioni 7 zinahitajika kujenga upya mfumo wa afya, na kwa jumla dola bilioni 53 zinahitajika kujenga upya Gaza baada ya miezi 15 ya vita kati ya Israel na Hamas, kulingana na tathmini ya Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya na Benki ya Dunia.

Watoto waliokimbia makazi yao na mwanamume mmoja wamesimama kwenye foleni kwenye jiko la jamii huko Deir al Balah, Gaza, mnamo Oktoba 2025.
UNOCHA/ Olga Cherevko Watoto wakiwa kwenye foleni ya chakula katika jiko la jumuiya huko Deir al Balah, Gaza, kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Furaha na shamra shamra Gaza

Katika eneo la Gaza, Wapalestina na Waisraeli walionekana kusherehekea habari za uwezekano wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya uongozi wa kisiasa wa Hamas na Israel.

“Kuna hali chanya sana na ya furaha hapa Gaza leo asubuhi, kama ilivyokuwa jana usiku,” afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa wa misaada ameiambia UN News. “Watu wanapiga filimbi, wanasherehekea. Bila shaka, vipaumbele vyetu vinabaki vilevile kuwafikia walio hatarini zaidi kwa misaada ya kutosha na kuhakikisha inawafikia wanaohitaj. Ni wazi hakuna kiwango chochote cha misaada ya kibinadamu kinachoweza kuchukua nafasi ya amani. Hivyo makubaliano haya ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote.”

Maafisa wa misaada ya Umoja wa Mataifa wana tani 170,000 za chakula, vifaa vya makazi, dawa na bidhaa muhimu zilizohifadhiwa nje kidogo ya Gaza.

Vyote hivyo vinaweza kupakiwa kwenye malori na kuingia Gaza mara tu usitishaji wa mapigano utakapokuwa umeanza, amesema afisa huyo wa misaada. “Tunatarajia kuona nafasi yetu itakuwaje katika siku zijazo na jinsi tutakavyoweza kupeleka misaada hii haraka na kwa ufanisi kwa wale wanaohitaji sana.”