Mashirika ya UN yatoa wito kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka Gaza
Mashirika ya UN yatoa wito kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka Gaza
Miaka miwili tangu mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 7 Oktoba 2023, maafisa wakuu wa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa wametoa tena wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano Gaza, kuachiliwa kwa mateka na wafungwa wote, pamoja na kuruhusiwa bila vizuizi kwa misaada ya kibinadamu kufika kwa raia walio katika janga la vita vinavyoendelea.
Tom Fletcher, Mratibu Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura wa Umoja wa Mataifa amesema maumivu yanayosababishwa na mzozo huo “hayaelezeki,” akirejelea mikutano aliyofanya na manusura na familia za waliotekwa wakati wa mashambulizi yaliyofanywa na Hamas dhidi ya Israel.
“Miaka miwili imepita tangu Hamas na makundi mengine ya wanamgambo walipotekeleza mashambulizi hayo ya kikatili nchini Israel. Kama nilivyoona na kusikia kutoka kwa manusura na familia za waliotekwa, maumivu hayaelezeki,” amesema Fletcher katika taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswisi.
Vita lazima vikome
Ameongeza kuwa “Leo, narudia wito wangu wa kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote na wakati huohuo, wanapaswa kutendewa kibinadamu. Raia kila mahali wanapaswa kulindwa.”
Fletcher pia ameeleza hali ngumu kwa Wapalestina huko Gaza, akibainisha kuwa “makumi ya maelfu ya Wapalestina wameuawa na mamia ya maelfu wanakabiliwa na njaa na kufurushwa makwao.”
Ameitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kumaliza mapigano hayo.
“Tunatoa tena wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja Gaza, kwa raia wote kulindwa, na misaada ya kibinadamu kuruhusiwa kuingia kwa kiwango kinachohitajika,” amesema, akiongeza kuwa sasa “kuna mwanga wa matumaini kwamba jambo hili linaweza kufanyika lazima tuulinde.”
Hali ya gaza ni jinamizi kubwa
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu waShirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA Philippe Lazzarini ameelezea miaka miwili iliyopita kama “jinamizi kwa watu wa Gaza.”
Kupitia chapisho katika akaunti yake rasmi ya X, Lazzarini amesema wakaazi wa Gaza hawajui kingine zaidi ya uharibifu, kutawanywa, mabomu, hofu, kifo na njaa.”
Ameongeza kuwa “Huzuni, mateso, maumivu makubwa na ya kina ndiyo hali halisi kwa watu wengi sana tangu tarehe 7 Oktoba 2023”.
Sasa imetosha tugange yajayo
“Tunapoadhimisha miaka miwili tangu kuanza kwa jinamizi hili, ninatoa tena wito wa kuachiliwa kwa mateka wote na wafungwa wa Kipalestina, kusitishwa mara moja kwa mapigano silaha zinyamaze kila mahali na kuruhusiwa bila vizuizi kwa utoaji wa mahitaji ya msingi ya kibinadamu Gaza, ikiwemo kupitia UNRWA.”
Lazzarini pia amesisitiza umuhimu wa kuwawajibisha wote waliotenda ukatili wakati na baada ya mashambulizi hayo.
“Hakuna njia nyingine ya kutoka kwenye shimo hili la vurugu na machafuko,” amesema.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu yameonya mara kadhaa kuhusu janga linalozidi kuwa baya huko Gaza, ambako zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wameyakimbia makazi yao na upatikanaji wa chakula, maji na huduma za afya umefikia kiwango cha hatari.