Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka miwili ya vita Gaza wananchi bado wanateseka

Israel ilipiga hospitali ya Nasser kusini mwa Ukanda wa Gaza tarehe 25 Agosti, na kuua takriban watu 20, wakiwemo waandishi wa habari watano.
© WHO
Israel ilipiga hospitali ya Nasser kusini mwa Ukanda wa Gaza tarehe 25 Agosti, na kuua takriban watu 20, wakiwemo waandishi wa habari watano.

Miaka miwili ya vita Gaza wananchi bado wanateseka

Amani na Usalama

Kwa miongo kadhaa, Israel na Palestina zimekuwa katika migogoro ya mara kwa mara. Lakini tarehe 7 Oktoba mwaka 2023, hali ilibadilika ghafla.

Siku hiyo ya jumamosi, wanamgambo wa Hamas walivamia Israel kwa mashambulizi ya roketi na ardhini, na kusababisha vifo vya watu karibu 1,250 wengi wao raia wa Israel na raia wa mataifa mengine na kuwateka nyara zaidi ya watu 250, wakiwemo wanawake, watoto na wazee.

Baada ya shambulizi hilo, Israel ilijibu kwa nguvu kubwa, ikiapa kuangamiza Hamas kabisa. Mpaka sasa, vita bado vinaendelea huku watu 48 wakiwa bado mateka Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akihutubia kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwezi uliopita alisema “Bado hatujamaliza. Wahusika wa mwisho, mabaki ya mwisho ya Hamas, wamejificha katika Jiji la Gaza. Wanaapa kurudia ukatili waliofanya Oktoba 7 tena, na tena, na tena haijalishi vikosi vyao vimepungua kiasi gani. Ndiyo maana Israel lazima imalize kazi. Ndiyo maana tunataka kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.”

Athari kubwa zaidi za vita hizi zimekuwa kwa raia wa Palestina. Maeneo ya makazi, shule, hospitali na hata maghala ya chakula yamekuwa yakishambuliwa. Maelfu wameuawa, wengine kupata ulemavu, na mamilioni wamelazimika kuhama mara kadhaa.

Israel imefunga vivuko vya misaada, jambo lililosababisha uhaba mkubwa wa chakula, dawa na mafuta. Umoja wa Mataifa umetangaza hali ya njaa Gaza na watu wengi wamekuwa wakipoteza maisha sababu ya njaa, mathalani shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO limeripoti vifo 400 vinavyohusishwa na utapiamlo mwaka huu pekee, wakiwemo watoto 101, 80 kati yao wakiwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Dkt Rana Abu Zaatir, ni Mkuu wa Idara ya Lishe ya Tiba, Hospitali ya Al-Awda huko Gaza“Kuna idadi kubwa ya watoto na watu wazima ambao wamekufa kutokana na utapiamlo na matatizo yanayowakumba watu baada ya kupata utapiamlo. Kwa bahati mbaya, katika siku zijazo na hata katika kipindi kijacho, ikiwa vivuko vitasalia vimefungwa na bei ya bidhaa za msingi kuendelea kupanda kwa njia hii, tutakabiliwa na maafa ya kweli katika Ukanda wa Gaza kutokana na utapiamlo na ukosefu wa rasilimali za kutosha za chakula kwa watu hawa wa maisha ya kawaida.”

Huko wodini hali ni mbaya pia mama huyu aitwaye Amneh Abu Autawy, akiwa mjamzito sababu ya ukosefu wa chakula alipungua uzito kutoka kilo 70 mpaka 46, alijifungua mtoto wake aitwaje Shaher Al-Qra akiwa na uzito mdogo sana na hadi sasa anaugua utapiamlo. Mtoto wake wa miezi minne ana kilo 3.7. “Mtoto wangu haongezeki uzito, hali ni ngumu sana, hakuna chakula, kwa hivyo sina maziwa yoyote ya kumnyonyesha, na hakuna chakula kwa ujumla. Kwa kuwa simnyonyeshi, hana kinga hivyo anapata maambukizo haraka sana. Kama mtoto amechoka sana, na dhaifu, nikimshika hivi, hawezi hata kujishikilia mwenyewe, hana kinga, hakuna chakula, hakuna kitu.”

Kutokana na mateso haya, Rais wa Marekani Donald John Trump tarehe 29 Septemba alitangaza mpango mpya wa kumaliza vita vya Gaza.
Mpango huo una vipengele 20, ikiwemo kusitisha mapigano mara moja, kuachilia mateka wote ndani ya saa 72, na kuunda serikali ya mpito isiyo ya kisiasa chini ya usimamizi wa kimataifa.

Hamas watakaokubali amani watapewa msamaha, huku misaada ya kibinadamu ikianza kuingia mara moja kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa na Hilali Nyekundu.
Trump pia amependekeza Baraza la Amani litakaloongoza ujenzi mpya wa Gaza, akisema yeye mwenyewe atakuwa mwenyekiti pamoja na viongozi kama Tony Blair.
Jeshi la kimataifa la muda litaundwa kusaidia usalama, kufundisha polisi wa Kipalestina, na kuratibu kuondoka kwa wanajeshi wa Israel hatua kwa hatua.

Trump amesema mpango huo unalenga kuleta Gaza yenye amani, uchumi imara na matumaini mapya kwa watu wake.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alikaribisha mpango huo kama anavyosema Naibu msemaji wake, Farhan Haq, “Katibu Mkuu anakaribisha tangazo la Rais Trump wa Marekani, lenye nia ya kusitishwa vita na kuleta amani endelevu katika eneo la Gaza. Ameshukuru zaidi jukumu muhimu la mataifa ya Kiarabu na Kiislamu katika kufanya kazi hadi kufikia lengo hili. Sasa ni muhimu kwamba pande zote zijitolee kwenye makubaliano na utekelezaji wake.”

Katibu Mkuu pia ametoa wito wa kuachiliwa kwa mateka wote mara moja, na amesisitiza tena umuhimu wa kusitisha mapigano, wakati dunia ikiadhimisha miaka miwili tangu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023.

Tayari Hamas wametangaza wako tayari kutekeleza mpango huo wa Marekani ishara ya matumaini mapya kwamba huenda mwisho wa vita vya Gaza ukawa unaonekana.