Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kukomesha vita Gaza, madhila ya miaka miwili yametosha: Guterres

Moshi ukifuk kutoka kwenye jengo lililoshambuliwa kwa bomu  katika jiji laGaza
UN News
Moshi ukifuk kutoka kwenye jengo lililoshambuliwa kwa bomu katika jiji laGaza

Ni wakati wa kukomesha vita Gaza, madhila ya miaka miwili yametosha: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, leo ametoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa mateka wote wanaoshikiliwa Gaza, na amesisitiza tena umuhimu wa kusitisha mapigano yanayoendelea kati ya Israel na makundi ya wanamgambo wa Kipalestina, wakati dunia ikiadhimisha miaka miwili tangu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023.

Waachilieni mateka, bila masharti yoyote na mara moja, amesema Katibu Mkuu kwa kauli ya msisitizo. “Malizeni mateso kwa watu wote. Hili ni janga la kibinadamu linalozidi uwezo wa kueleweka.”
Guterres amesema huzuni ya siku ile iliyoghubikwa na giza,” ambapo Hamas na makundi mengine ya kivita yalifanya “shambulio la kigaidi kubwa na la kutisha dhidi ya Israel itasalia milele katika kumbukumbu zetu zote.”
Mama akiwa ameketi kando ya kitanda cha mwanaye mgonjwa katika hospitali jijini Gaza
© UNICEF/Rawan Eleyan
Mama akiwa ameketi kando ya kitanda cha mwanaye mgonjwa katika hospitali jijini Gaza

Mamia waliporeza maisha

Katika shambulio hilo la Oktoba 7 zaidi ya watu 1,250 Waisraeli na raia wa mataifa mengine waliuawa katika, huku zaidi ya watu wengine 250 wakitekwa nyara na kupelekwa Gaza, wakiwemo wanawake, watoto na wazee.
Katibu Mkuu amesema hadi sasa, baada ya miaka miwili, baadhi ya mateka bado wanashikiliwa katika mazingira ya kusikitisha, na ameeleza kuwa amekutana na familia za mateka hao “zilizoshiriki naye maumivu yao yasiyovumilika.
Waachieni raia wasiendelee kulipa gharama kwa maisha yao na mustakabali wao, ameongeza Guterres. Sitisheni mapigano Gaza, Israel na katika eneo lote sasa.
Katibu Mkuu pia ametaja pendekezo la hivi karibuni lililotolewa na Rais wa Marekani Donald J. Trump kuwa ni fursa inayopaswa kukumbatiwa kikamilifu ili kukomesha mzozo huu wa kusikitisha.
Maiti ya mwanamke aliyepigwa risasi na kuuawa ukiwa katika barabara ya Al Rashid nje ya jiji la Gaza
UN News
Maiti ya mwanamke aliyepigwa risasi na kuuawa ukiwa katika barabara ya Al Rashid nje ya jiji la Gaza

Amani ya kudumu ndio jawabu

Amesisitiza umuhimu wa kuwa na usalama wa kudumu na mchakato wa kisiasa wenye uhalisia ili kuzuia umwagaji damu zaidi na kufungua njia kuelekea amani ya kudumu.
Sheria za kimataifa lazima ziheshimiwe, amesema kwa msisitizo.
Katika wito wake wa mwisho, Guterres amehimiza umoja na matumaini. “Baada ya miaka miwili ya majeraha na mshtuko, lazima tuchague matumaini sasa.”
Amerejea kusema kuhusu kujitolea kwa Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono juhudi za amani, akisema Umoja wa Mataifa unasalia thabiti katika dhamira yake ya kuunga mkono amani.
Ameongeza kuwa “Katika kumbukumbu hii ya huzuni, tuwaheshimu waathirika wote kwa kufanya kazi kuelekea njia pekee ya kusonga mbele, amani ya haki na ya kudumu, ambapo Waisraeli, Wapalestina na watu wote wa eneo hilo wanaishi kwa usalama, utu na heshima ya pamoja.