Haiti yapambana na kichaa cha mbwa kwa chanjo na uangalizi makini
Haiti yapambana na kichaa cha mbwa kwa chanjo na uangalizi makini
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Afya la Pan-America (PAHO) limeripoti kuwa, mwezi wa Julai mwaka jana, katika eneo la mbali la Butête kusini mwa Haiti, mvulana mwenye umri wa miaka 9 aitwaye Jonas alipoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa (rabies).
Jonas alipoumwa na mbwa aliyekuwa akizurura mitaani kwenye mguu, jeraha lake lilionekana kuwa dogo. Kama ilivyo kwa familia nyingi zinazoishi mbali na vituo vya afya, mama yake hakuwa na uelewa kwamba matibabu ya haraka ni muhimu sana. kwa wiki moja, Jonas alianza kujisikia dhaifu na akakataa kula. Alipofikishwa hospitali ya karibu, tayari alikuwa ameanza kuonesha dalili dhahiri za ugonjwa wa kichaa cha mbwa, ikiwemo mishtuko mikali ya misuli na mshtuko wa maji (hydrophobia).
Yeye ndiye mwathirika wa hivi karibuni wa ugonjwa huu hatari lakini unaoweza kuzuilika kabisa, ambao tayari umesababisha vifo vinne mwaka huu katika taifa la visiwa vya Karibiani la Haiti, linalokumbwa na matatizo mengi kama vile misukosuko ya kisiasa na kiuchumi, umasikini uliokithiri, na ukosefu wa huduma za afya.
Takwimu na hatari ya kiafya
Takwimu zilizokusanywa kati ya mwaka 2022 hadi 2024 nchini Haiti zinaonoesha kuwa virusi vya kichaa cha mbwa vinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya umma, ambapo zaidi ya visa 8,000 vya mbwa waliodhaniwa kuwa na kichaa cha mbwa vilichunguzwa. Kati ya hivyo, zaidi ya visa 1,100 vimehesabiwa kuwa na uwezekano mkubwa wa maambukizi, na visa 46 vimethibitishwa katika maabara. Katika kipindi hicho hicho, kulikuwa na visa 24 vya binadamu waliodhaniwa kuambukizwa (hasa baada ya kung’atwa na mbwa), ambapo vifo 8 vilithibitishwa.
Ufuatiliaji, Uchunguzi na Mwitikio
Mara tu Jonas alipoingizwa hospitalini, Mtandao wa Kitaifa wa Ufuatiliaji wa Wizara ya Afya ya Umma ulitaarifiwa. Kwa msaada wa Shirika la Afya la Pan-Amerika (PAHO), ambalo ni sehemu ya Shirika la Afya Duniani (WHO), mtandao huu wa kitaifa wenye wafanyakazi wa mashinani na rasilimali, wakiwemo wasaidizi wa magonjwa ya mlipuko walioko jamii na wahudumu wa afya wanaosafiri kwa pikipiki (‘labo-moto’), ulianza kazi mara moja.
Timu ya dharura ilitumwa Butête ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu mwingine katika jamii ataambukizwa kichaa cha mbwa. Familia ya mvulana huyo imefuatiliwa kwa karibu na ikapokea matibabu ya kinga baada ya kuambukizwa. Timu hiyo pia imeikagua eneo alilokufa mbwa huyo na watoto wake.
Uchunguzi umependekeza kufanyika kwa kampeni ya chanjo ya mbwa, kuimarishwa kwa ufuatiliaji, na kuboreshwa kwa upatikanaji wa chanjo za binadamu dhidi ya kichaa cha mbwa kwa matibabu ya baada ya kung’atwa.
Hatari inayoua lakini inayozuilika kabisa
Ili kupunguza kuenea kwa kichaa cha mbwa nchini Haiti, kampeni ya chanjo kwa mbwa ilizinduliwa mwezi Agosti kwa lengo la kuwachanja mbwa wapatao 140,000, wakiwemo mbwa wa mitaani na wa jamii, sambamba na kuongeza uelewa wa umma kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
Kabla ya kuanza kwa kampeni hiyo, mafunzo yalitolewa kwa waratibu wanne wa ngazi ya mikoa, waratibu kumi na saba wa ngazi ya wilaya, na zaidi ya wasaidizi wa mifugo 480, ambao baadaye wamegawanywa katika timu 240 na kutumwa katika maeneo ya kipaumbele katika mikoa minne: Artibonite, Centre, Nord-Est, na Nord-Ouest.
Ubunifu muhimu katika kampeni hiyo umekuwa matumizi ya programu ya simu ya mkononi kuandikisha mbwa waliopata chanjo, hatua iliyowezesha ukusanyaji wa data kwa wakati halisi, ufuatiliaji wa chanjo, na kuboresha ubora wa taarifa.
“Kwa kuwachanja mbwa kwa wingi, tunawalinda moja kwa moja wanajamii hasa watoto. Hii ni hatua rahisi lakini muhimu sana inayookoa maisha, Kichaa cha mbwa ni hatari, lakini kinaweza kuzuilika kwa asilimia 100.” ameeleza Dkt. Oscar Barreneche, mwakilishi wa PAHO/WHO nchini Haiti.
Kujenga Ustahimilivu wa Muda Mrefu
Kufikia kiwango cha asilimia 80 ya chanjo kwa mbwa waliolengwa kunatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mzunguko wa virusi vya kichaa cha mbwa kwa wanyama. Kampeni hii pia inalenga kuongeza uelewa wa kuzuia kichaa cha mbwa na kukuza hatua sahihi zinazopaswa kuchukuliwa mtu anapoumwa na mnyama anayedhaniwa kuwa na kichaa cha mbwa.
Dkt. Haïm Joseph Corvil, Mratibu wa Kitengo cha Ulinzi katika Wizara ya Kilimo, Rasilimali Asili na Maendeleo ya Vijijini ya Haiti, amesisitaza kuwa licha ya changamoto za kiusalama na hali ya kutokuwa na utulivu nchini, wanachukulia kampeni hii ya chanjo kama mafanikio makubwa.
Changamoto ya Afya Ulimwenguni
Kichaa cha mbwa bado ni moja ya magonjwa ya zoonotic yanayoua zaidi duniani yaani, magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Kote duniani, ugonjwa huu unasababisha takribani vifo 59,000 kila mwaka, ambapo asilimia 40 ya waathirika ni watoto.
Katika bara la Amerika, kumekuwa na upungufu wa asilimia 98 wa visa vya kichaa cha mbwa kwa binadamu vinavyosababishwa na mbwa, kutoka visa 300 mwaka 1983 hadi visa 10 tu vilivyoripotiwa mwaka uliopita, kulingana na PAHO.