Wakati wa Afrika kupewa viti na sauti Baraza la Usalama la UN ni sasa: Lokaale
Wakati wa Afrika kupewa viti na sauti Baraza la Usalama la UN ni sasa: Lokaale
Mwakilishi wa kudumu wa Kenya katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ekitela Lokaale, amesema kuwa ni wakati muafaka kwa Afrika kupewa nafasi ya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ili bara hilo liwe na sauti sawa na mataifa makubwa katika uamuzi wa masuala ya amani na usalama duniani.
Akizungumza katika mahojiano maalum na UN News Kiswahili kandoni mwa Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80, Balozi Lokaale amesema bara la Afrika limekuwa likisukuma ajenda ya mageuzi kwa zaidi ya miaka ishirini bila mafanikio makubwa.
"Nchi za Afrika, kwa miaka ishirini sasa, tumekuwa tukisukuma kwamba lazima tulete mabadiliko katika Baraza la Usalama," amesema.
Kwa mujibu wake, msimamo wa pamoja wa Afrika unaofahamika kama Ezulwini Consensus unapendekeza kuwa bara hilo lipate si chini ya viti viwili vya kudumu katika Baraza la Usalama. "Makubaliano ambapo tulikubaliana kwamba Afrika ipewe sio chini ya viti viwili katika Baraza la Usalama," amesisitiza.
Ingawa hatujafanikiwa lakini kuna matumaini
Balozi Lokaale amefafanua kuwa ingawa harakati hizo hazijafanikishwa kikamilifu hadi sasa, lakini mwaka huu kumekuwa na hatua muhimu. "Mwaka huu kidogo tumeweza kupiga hatua kwa vile yale makubaliano yetu tumeweza kuyabadilisha kuwa pendekezo. Pendekezo ambalo sasa tunawasilisha katika mazungumzo ya mataifa kuhusu mabadiliko katika Baraza la Usalama," amesema.
Ameongeza kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa kumi ya Afrika yaliyopewa jukumu na Muungano wa Afrika AU, kuendeleza mazungumzo hayo katika ngazi ya kimataifa. "Nchi yangu Kenya ni mojawapo ya mataifa ambayo yamepewa hilo jukumu na Muungano wa Afrika. Na tuliwasilisha pendekezo letu katika Seneti ya Marais wote kutoka Afrika ili watupatie kibali cha kuwasilisha sasa katika Umoja wa Mataifa," ameongeza Balozi Lokaale.
Amekumbusha kuwa Afrika kwa sasa haina mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama, licha ya kuwa bara lenye idadi kubwa ya wanachama wa Umoja wa Mataifa na mara nyingi likiwa kitovu cha mijadala kuhusu amani na usalama.
Hivyo amesema Mageuzi ya Baraza la Usalama yamekuwa ajenda inayojirudia kila mwaka katika mikutano mikuu ya Umoja wa Mataifa, lakini bado hayajapata muafaka wa pamoja kutoka mataifa yote.