Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ili Afrika ‘iimarike kiafya’ inabidi isiwe tegemezi kwenye masuala ya kifedha - Dkt. Ntuli Kapologwe

Dkt. Ntuli Kiapologwe wa ECSA akizungumza na Anold Kayanda wa Habari za UN Kiswahili katika SDG Media Zone katika makao makuu UN jijini New York, Septemba 2025.
UN News Mkurugenzi Mkuu wa ECSA - HC, Dkt. Ntuli Kiapologwe akizungumza na Anold Kayanda wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, Septemba 2025.

Ili Afrika ‘iimarike kiafya’ inabidi isiwe tegemezi kwenye masuala ya kifedha - Dkt. Ntuli Kapologwe

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Tukisalia hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, kandoni mwa Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA80, inafanyika mikutano mingine ya pembezoni kujadili masula mengine ya kusongesha maendeleo ya ulimwengu. Wiki iliyopita tulizungumza na Dkt. Ntuli Kapologwe Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, ECSA wakati alipokuwa akisubiri kushiriki mkutano  wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kujadili jinsi ya kusongesha diplomasia ya kisayansi ili kuhakikisha bara la Afrika haliachwi nyuma kwenye kukabiliana na changamoto za kiafya.

Anold Kayanda wa Idhaa hii amezungumza tena na Dkt. Kapologwe mara tu baada ya mkutano huo

Katika mazungumzo haya, Dkt. Kapologwe anaanza kwa kuzishukuru nchi wanachama wa Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, ECSA kwa kuitikia wito na kushiriki mkutano huu muhimu.

ECSA iliyoundwa mwaka 1974 kusongesha ushirikiano wa kikanda katika afya inajumuisha nchi 9 ambazo ni Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Eswatini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Anasema nchi wanachama wameukubali mpango wa kuanzisha kituo cha umahili cha masuala ya sayansi, utafiti na ubunifu kinachotarajiwa kujengwa nchini Tanzania katika moja ya maeneo ya mkoa wa Arusha, kaskazini mwa nchi ambako serikali ya Tanzania imejitolea kwa kutoa ardhi kwa ajili ya kituo hicho mahili.”

Changamoto ya ufadhili duniani

Hivi sasa ulimwenguni kote, mataifa, mashirika na taasisi mbalimbali zinazotegemewa kusongesha maendeleo ya ulimwengu zinakabiliwa na changamoto ya ufadhili. ECSA wameshaliona hilo na ingawa nchi wanachama zinachangia mchango wao wa kila mwaka, lakini uongozi wa ECSA unahamasisha nchi kujenga mfumo wa kujitegemea ili kuweza kufadhili huduma za afya.

“Lakini pili tunawahamasisha sekta binafsi kuhakikisha zinakuwa na mchango katika maeneo mbalimbali. Na nchi nyingine tuna Ushahidi mzuri tu. Nchi kama Tanzania, nchi kama Kenya,nchi kama Mauritius, sekta binafsi imekuwa na mchango mkubwa katika kuunga mkono sekta ya afya.” Anaeleza Dkt. Kapologwe.

Anasema wanaamini ili Afrika iwe na nguvu na kuweza kutimiza malengo hayo, na majadiliano ambayo wameyafanya,  “ni lazima isiwe tegemezi kwenye masuala ya kifedha na lazima nchi wanachama zenyewe zibebe jukumu kwamba hiki kitu ni cha kwetu, tutazalisha wanasayansi wa Afrika na wabunifu wa Afrika, na pia tutajenga kituo cha umahili cha kusaidia bara letu kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo.”