Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi yasema vikwazo haramu vya upande mmoja ni silaha ya nchi za magharibi

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la UN.
UN Webcast Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la UN.

Urusi yasema vikwazo haramu vya upande mmoja ni silaha ya nchi za magharibi

Amani na Usalama

Urusi imetumia sehemu ya hotuba yake ya leo kwenye mimbari ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuzungumzia hatua ya nchi za magharibi kupinga ndani ya Baraza la Usalama pendekezo la kuiongezea muda Iran nafuu ya vikwazo kwa mujibu wa makubaliano ya mwaka 2015.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov amesema “jana ndani ya Baraza la Usalama, nchi za magharibi (akimaanisha Marekani na Uingereza), zimepinga pendekezo la China na Urusi la kuongeza mud awa makubaliano ya 2015 juu ya Mpango wa Nyuklia wa Iran, kwa lengo la kupatia fursa zaidi diplomasia.”

Hii ina maana vikwazo dhidi ya Iran vilivyokoma tangu mwaka 2015, vitaanza kuzingatiwa kuanzia leo Septemba 27.

“Hatimaye, hatua hii bila shaka imefichua ajenda ya nchi za maghairbi ya kuhujumu juhudi za kutafuta suluhisho lenye kujenga amani,” amesema Lavrov.

Lavrov pia amelaani vikwazo haramu vya upande mmoja, ambavyo amesema "vimekuwa chombo kikuu cha diplomasia ya magharibi."

Akizungumzia kuhusu Ukraine, Lavrov amesema kuwa Urusi imekuwa — na bado iko — tayari kwa mazungumzo ili kushughulikia chanzo kikuu cha mgogoro huo.

“Urusi inapendekeza kujenga mfumo wa usalama wenye usawa na usiogawanyika huko eneo la kati ya Asia na Ulaya — sio tu kwa nchi wanachama wa Umoja wa Kujihami wa nchi za Magharibi, NATO na washirika wao, bali kwa nchi na mashirika yote katika bara hilo, bila ubaguzi."

Mwamko mpya Afrika na nchi nyingine za kusini

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Urusi amezungumzia pia harakati za kujikwamua kutoka utegemezi wa kiuchumi na uhuru kamili kwa mataifa ya Afrika na mengine yanayoendelea.

“Afrika na nchi nyingine za kusini zinazoendelea, zinapitia mwamko mpya, wakijitahidi kupata uhuru kamili — na Umoja wa Mataifa haupaswi kubaki kando. Mwezi Desemba mwaka jana, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la ‘Kutokomeza Ukoloni katika aina na mifumo yake yote.”

Kama hatua inayofuata, tunatoa wito wa kupitisha uamuzi wa kutangaza tarehe 14 Desemba kuwa siku ya kimataifa ya mapambano dhidi ya ukoloni.

Ramani ya dunia hivi sasa tofauti na miaka 80 iliyopita

Kwa mujibu wa Lavrov, mizania ya sasa ya nguvu duniani ni tofauti kabisa na ile iliyowekwa miaka 80 iliyopita. “Mchakato wa ukuaji wa uhuru na mabadiliko mengine makubwa yameibadilisha kabisa ramani ya kisiasa ya dunia. Wakazi wengi duniani wanazungumza kwa sauti kubwa wakitetea haki zao.”

Ametaja taasisi kama SCO ambayo ni Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai na BRICS yanacheza nafasi maalum kama mifumo ya kuoanisha maslahi ya nchi za kusini na mashariki mwa dunia.

“Nguvu ya mashirika ya kikanda kama vile Muungano wa Afrika na mengineyo yanaendelea kukua kwa kasi. Hali hizi mpya bado hazijaakisiwa ipasavyo katika muundo wa taasisi wa Umoja wetu,” ameonya Lavrov.

Hivyo amesema “Urusi inaunga mkono demokrasia ndani ya Baraza kwa kuongeza uwakilishi kutoka Asia, Afrika, na Amerika ya Kusini. Tunaunga mkono maombi ya Brazil na India ya kuwa wanachama wa kudumu katika Baraza hilo, sambamba na kurekebisha dhuluma ya kihistoria dhidi ya Afrika — kwa mujibu wa vigezo vilivyokubaliwa na nchi za Afrika zenyewe.”