Burkina Faso yasema miaka 80 ya UN yahitaji tafakuri ya kina, la sivyo mwelekeo ni tete
Burkina Faso yasema miaka 80 ya UN yahitaji tafakuri ya kina, la sivyo mwelekeo ni tete
Katika siku ya tano ya Mjadala Mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, (UNGA80), Waziri Mkuu na Kiongozi wa Serikali ya Burkina Faso, Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo, amezungumzia ‘tamu na chungu’ ya miaka 80 ya chombo hicho chenye wanachama 193.
Ametambua mchango wa Umoja wa Mataifa na wadau wake katika kusongesha amani, ustawi na utulivu lakini wakati huo huo amesema miaka hiyo 80 imegubikwa pia na fursa zilizopotea, kushindwa kwa miundo ya taasisi, na kupoteza umuhimu katika kukabili migogoro ya kimataifa.
Wakati wa tathmini ya kina na si sherehe
Akirejelea kaulimbiu ya mjadala huo, “Tuko Bora Pamoja: Miaka 80 ya Huduma kwa Amani, Maendeleo na Haki za Binadamu,” Waziri Mkuu Ouedraogo amesema ni wakati wa kutathmini na si kusherehekea.
“Tunatakiwa tufanye tathimi ya kina ya kile tulichofanikiwa. Taarifa ya miaka hii 80 si ya ushindi, bali ni aibu ya pamoja — kushindwa kwa muundo wa taasisi,” amesema.
Ouedraogo ametaja kuendelea kwa migogoro ya kivita, kuongezeka kwa ugaidi, na kutotambuliwa kwa Afrika katika maamuzi ya kimataifa kama mifano dhahiri ya mapungufu ya Umoja wa Mataifa.
Kulikoni kuenguliwa Afrika kwenye Baraza?
Amekemea hali ya kutotambulika kwa bara la Afrika kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akiita hali hiyo kuwa ni “ukosefu wa haki wa kihistoria” unaodhoofisha misingi ambayo Umoja wa Mataifa unadai kuisimamia.
“Afrika — chimbuko la binadamu, makazi ya zaidi ya watu bilioni moja, na kitovu cha changamoto nyingi za dunia — inawezaje kuendelea kutokuwa na nafasi kwenye meza ya maamuzi ya Baraza la Usalama?” amehoji.
Kuhusu ulinzi wa amani, amesema bado kuna changamoto kwani amesema zinashindwa kukidhi matakwa yake.
Ameelekeza chimbuko la kushindwa huko kuwa ni muundo na utendaji wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
“Chombo kilichojaa maamuzi ya kisiasa, kikipoozwa na migongano ya ndani, na iliyolemazwa na migawanyiko ya kudumu.” Amekwenda mbali zaidi, akilifananisha Baraza hilo na “biashara mbaya” inayodhibitiwa na tamaa za baadhi ya wanachama wake wa kudumu.
Baraza la Usalama limegeuzwa kuwa eneo la biashara
“Wanachama hawa, ambao wanapaswa kuwa walinzi wa amani, mara nyingi hugeuka kuwa tishio kuu — wakifadhili na kuchochea migogoro ambayo Umoja wa Mataifa unapaswa kuitatua,” amesema, akitoa mfano wa mgogoro wa muda mrefu kati ya Israeli na Palestina na vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi kama mifano ya kushindwa kwa jamii ya kimataifa.
Ouedraogo ameeleza kuwa asili ya maazimio ya Mkutano Mkuu yasiyo na nguvu ya kisheria imeufanya kuwa “taasisi isiyosikika wala yenye ufanisi,” na hivyo mageuzi ya kweli yamebaki kuwa ndoto isiyotimizwa.
“Muda wa mageuzi ya ujasiri umefika,” amesema. “Bila hayo, Baraza la Usalama litaendelea kuwa taasisi iliyopitwa na wakati, isiyoweza kukabiliana na changamoto za zama zetu.”
Hata hivyo Ouedraogo ametambua mchango muhimu wa Umoja wa Mataifa na washirika wake katika kusaidia Burkina Faso kwenye harakati zake za amani na maendeleo huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa kweli wa kimataifa, — unaozingatia usawa, haki, na ufanisi — haiwezi tena kucheleweshwa.