Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyuklia ni tishio kubwa la kimataifa linaloongezeka: UN

Mtazamo wa angani wa Kuba la Bomu la Atomiki na Mto Naka huko Hiroshima, Japani, ukiwa na mashua ya watalii juu ya maji na anga ya jiji la kisasa nyuma.
© Unsplash/Desmond Tawiah Bustani ya kumbukumbu ya amani ya Hiroshima ambako bomu la atomiki lilianguka kusini mwa Japan

Nyuklia ni tishio kubwa la kimataifa linaloongezeka: UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  leo ameonya mbele ya wajumbe wa mkutano wa ngazi ya juu kando ya Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA80 mjini New York unaojadili kuondoa silaha za nyuklia kuwa “tishio hilo linaendelea kuwa hatari kubwa ya kimataifa.”

Tarehe 26 Septemba kila mwaka inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Matumizi ya Silaha za Nyuklia inayosisitiza uharibifu unaoendelea kutokana na kasi ya kusambaa kwa silaha za nyuklia ambayo inatoa fursa kwa jumuiya ya kimataifa kuthibitisha tena dhamira yake ya kupunguza silaha za hizo.
Hata hivyo, amesema ahadi za kupunguza silahahzo za nyuklia  bado hazijatekelezwa.
Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu António Guterres mkuu wa masuala ya utendaji wa Umoja wa Mataifa Courtenay Rattray amesema “Silaha za nyuklia zinaendelea kuhatarisha dunia yetu. Na licha ya miongo ya ahadi, tishio linaendelea kuharakisha dunia na kubadilika.”
Amewakumbusha washiriki wa mkutano huo katika ukumbi uliosheheni kuhusu uharibifu uliojitokeza kutokana na bomu la atomiki lililorushwa na Marekani nchini Japan mwaka 1945, na amewataja hibakusha, waathirika waliokuwepo Hiroshima na Nagasaki miaka 80 iliyopita, ambao “wamegeuza mateso yao kuwa wito wa amani.”
Picha nyeusi na nyeupe inayoonyesha magofu na uharibifu katika Hiroshima, Japani, baada ya kumbukumbu la atomiki mwaka 1945. Kumbukumbu la Atomiki (Atomic Bomb Dome) inaonekana kwenye mandhari kati ya makoloni.
UN Photo/Mitsugu Kishida Hiroshima, muda mfupi baada ya bomu la nyuklia kurushwa kwenye mji huu mnamo Agosti 1945

Dunia imelala wakati changamoto ikiendelea

Hata hivyo, ameonya kuwa tunapita katika hali ya kulala huku tukiendelea kuelekea mbio za silaha za nyuklia ambazo ni changamoto zaidi, zisizotarajiwa na hatari zaidi.
Bwana Rattray  amesema “Teknolojia mpya na nyanja mpya za migongano zimefuta nafasi ya kufanya makosa,” akirejelea mtandao wa kielektroniki na anga za juu, pamoja na teknolojia kama vile makombora ya hypersonic na ndege zisizo na rubani zinazofanya uwezekano wa kuongezeka kwa migongano na makosa ya kimahesabu kuwa mkubwa.
“Hii siyo tu mgogoro wa silaha. Ni mgogoro wa kumbukumbu, uwajibikaji, na ujasiri.”

Jopo jipya huru limeundwa

Ili kukabiliana na vitisho vinavyoibuka, Bwana Rattray metangaza kuundwa kwa jopo huru la kisayansi la Umoja wa Mataifa ili kutathmini athari za vita vya nyuklia na kuhakikisha kuwa “Hatua za pamoja kwa hatari za nyuklia zina msingi wa ushahidi thabiti wa kisayansi.”
Akirejelea Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT), makubaliano ya kimataifa yanayolazimisha kisheria ambayo yanalenga kuzuia kusambaa kwa silaha za nyuklia, amesema kuwa hakuna “wakati sahihi wa kupunguza silaha za nyuklia kama sasa na kwamba hautatokea kamwe ikiwa tutaendelea kusubiri.”
Amesisitiza kuwa “Kupunguza silaha za nyuklia si tu zawadi ya amani ni msingi wa amani”.
Picha nyeusi na nyeupe ya kihistoria ya raia watatu wa Japani, ambao huenda wamenusurika bomu la atomiki la Hiroshima, ambao wamepokea huduma ya matibabu.
UN Photo/Hajime Miyatake Manusura wa bomu la Hiroshima ambao walikuwa wamepatiwa matibabu

Nchi zinapaswa kutimiza ahadi zao

Bwana Rattray amesisitiza kuwa mataifa yenye silaha za nyuklia lazima yarejeshe mazungumzo, yachukue hatua za kuimarisha uaminifu, na kuhakikisha vita vya nyuklia viko mikononi mwa binadamu si mifumo inayodhibitiwa na akili mnemba AI.
Katika htuba hiyo ameongeza kuwa “mataifa yanapaswa pia kutimiza ahadi zao chini ya mkataba wa NPT.”
Aidha, ameyahimiza mataifa yote kuridhia Mkataba Kamili wa Kuzuia Majaribio ya Nyuklia, unaokataza majaribio ya nyuklia, na kuwataka Marekani na Urusi kujadiliana na kupunguza silaha zao za nyuklia.
“Hizi hatua peke yake hazitaunda dunia isiyo na silaha za nyuklia. Lakini bila hizo hatua, tunakubali kuukabidhi mustakbali wetu kwenye hofu na kukatika kwa ahadi ya amani.”
Uwezekano wa teknolojia ya nyuklia kuhudumia binadamu
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, ameonya kuhusu hatari na “changamano zinazotokana na silaha za nyuklia, ikiwemo uwezekano wa kuingia mikononi mwa magaidi au kuibuka kwa AI katika uwanja wa vita”.
Wingu kubwa la uyoga mweupe kutoka kwa jaribio la nyuklia linainuka kutoka baharini katika Atoll ya Enewetak.
US Government Jaribio la nyuklia lililofanywa na Marekani katika eneo la Enewetak Atoll, Marshall Islands, 1 Novemba 1952.
Amesisitiza kuwa “mikataba pekee haitoshi isipokuwa mataifa yaitekeleze na kuhimiza sera ya kutotumia kwanza,” pamoja na kupanua rasilimali kuanzia kasi ya kusambaa kwa silaha hizo hadi hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Bibi Baerbock ameihimiza jumuiya ya kimataifa kufikiria jinsi teknolojia ya nyuklia inavyoweza “kutoa huduma kwa binadamu kwa njia ya kujenga na salama,” kama vile katika tiba ya saratani na ufuatiliaji wa changamoto ya mazingira.