Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kinachohitajika ni biashara tujitegemee na si misaada- Rwanda

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza uu la Umoja wa Mataifa Alhamisi ya Septemba 25, 2025.
UN Photo/Laura Jarriel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza uu la Umoja wa Mataifa Alhamisi ya Septemba 25, 2025.

Kinachohitajika ni biashara tujitegemee na si misaada- Rwanda

Masuala ya UM
  • Tushirikiane UN ikidhi mahitaji ya sasa
  • Biashara badala ya misaada
  • Tunaunga mkono marekebisho ya UN
  • Tuko tayari kupokea ofisi za mashirika ya UN
Rwanda imesema nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa pamoja zina wajibu wa kushirikiana ili chombo hicho kilichotimiza miaka 80 mwaka huu kiweze kukidhi sio tu mahitaji ya sasa, bali pia kiweze kutatua mahitaji ya mabilioni ya watu duniani kote.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe amesema hayo akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Alhamisi ya Septemba 25, 2025.
Amesema kwa ushirikiano wa aina hiyo zinaweza kutatua changamoto zinazokabili dunia sasa kuanzia haki za binadamu, mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kiuchumi, na maeneo mengine sauti zao kutosikika.
 
“Ndio maana Rwanda inaunga mkono kwa dhati marekebisho, hasa ya Baraza la Usalama. Uwakilishi wa chombo hicho hauakisi uhalisia wa sasa,” amesema Nduhungirehe, akitolea mfano bara la Afrika.
 
Amesema “Afrika yenye watu bilioni 1.2, ni bara ambalo ajenda zake nyingi zinajadiliwa kwenye Baraza la Usalama. Kwa hiyo bara hili haliwezi kusalia bila ujumbe wa kudumu kwenye Baraza hilo.”

Ubia wa biashara badala ya misaada

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Rwanda amezungumzia pia ushirikiano wa kimaendeleo akisema umesaidia kusongesha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.
 
Hata hivyo amesema wakati umefika kuhama kutoka misaada kwenda kwenye biashara, “hii itawezesha nchi zinazoendelea kujitegemea kupitia ubia wenye maslahi kwa pande zote.”
Usalama Maziwa Makuu

Amani Mashariki mwa DRC

Hotuba yake yenye kurasa 13 na ambayo ameisoma kwa muda wa dakika 16 na sekunde 54 iliangazia pia mzozo mashariki mwa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC).
 
“Kwa Ukanda wa Maziwa Makuu, suala hili ni dharura. Mzozo wa sasa huko Mashariki mwa DRC si mpya. Umejikita katika miongo kadhaa ya uongozi dhaifu, ubaguzi na mateso ya jamii za wachache, itikadi ya mauaji ya kimbari na ukoloni,” amesema Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Rwanda.
 
Amesisitza kuwa Rwanda inaamini kuwa amani Mashariki mwa DRC ni kwa manufaa ya kila mtu. “Lengo letu limekuwa—na litaendelea kuwa—usalama na ustawi wa Wanyarwanda, na watu wa ukanda wetu."

Ushirikiano na Umoja wa Mataifa

Ametamatisha kwa kusema kuwa Rwanda iko tayari kufanya kazi pamoja na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa, ili kuhakikisha kwamba Umoja wa Mataifa unabaki kuwa chombo cha amani, haki, na maendeleo endelevu.
 
Na katika muktadha huo amesema Rwanda inatoa shukrani zake kwa Katibu Mkuu António Guterres kwa ripoti yake ya kina kuhusu kazi ya Umoja wa Mataifa, inayolenga kuboresha ufanisi wake.
Kwa kuzingatia hili, “Rwanda imeeleza rasmi nia yake ya kuandaa ofisi za mashirika ya Umoja wa Mataifa, kama sehemu ya dhamira yetu ya pamoja ya mfumo wa UN usio na gharama kubwa na uliogawanywa."