Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hotuba ya Netanyahu yakumbana na upinzani, yeye augeuza ukumbi kuwa darasa

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Hotuba ya Netanyahu yakumbana na upinzani, yeye augeuza ukumbi kuwa darasa

Amani na Usalama

Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukiwa umeingia katika siku yake ya nne hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani leo Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amekuwa wa kwanza kuzungumza akitumia muda wake mwingi kushambulia wanamgambowa kipalestina, Hamas na kutetea kila uamuzi wa Israel. Anold Kayanda ameifuatilia hotuba hiyo kwa kina. 

Ilikuwa majira ya saa tatu na dakika chache hivi asubuhi ya leo saa za New York nchini Marekani ambapo Waziri Mkuu wa Isreal Benjamin Netanyahu amepewa fursa ya kuhutubia na ndipo ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukakosa utulivu.
 
Wajumbe kwa makundi walinyanyuka katika viti vyao na kuondoka huku wakiwaacha maafisa wa Israel wakimpigia makofi kiongozi wao na pia nchi zinazoiunga mkono Israel zikasalia katika viti vyao ikiwemo Marekani. 

Baadhi ya wajumbe watoka nje

Katika eneo la walipotakiwa kukaa wawakilishi wa Palestina kulikuwa wazi, huku katika eneo la Iran ikibakia picha iliyokusanya sura za baadhi ya watu wao waliouawa na mashambulizi ya Israel.
 
Bwana Netanyahu kwa mara nyingine tena ameingia na ubao wenye picha ya ramani ya eneo la Mashariki ya Kati akiutumia kuishambulia Iran na kwa kutumia kalamu akiweka alama ya vema kuonesha namna ambavyo Israel imefanikiwa kupambana na ngome za Irani katika ukanda huo.
 
Katika suti yake, kifuani upande wa kulia, Bwana Netanyahu pia ameweka kibandiko chenye QR Code na akawaambia watu kuwa Israel bado inakumbuka tukio walilofanyiwa na Hamas mwezi Oktoba mwaka juzi na kwamba ikiwa watu wamesahau hilo basi waelekeze simu zao kwenye QR Code hiyo kwenye nguo yake ili iwaoneshe madhara yaliyofanywa na Hamas.

Majina ya mateka yakasomwa

Waziri Mkuu huyo wa Israel ameyasoma majina ya mateka ambao bado wako mikononi mwa Hamas katika eneo la Ukanda wa Gaza na pia akaueleza mkutano kuwa amesambaza vipaza sauti au spika katika eneo lote la Gaza ili anapoongea leo, azungumze moja kwa moja na mateka huko walikofichwa. Na hapo akabadilisha lugha na kuongea kwa kihebrania akiwaahidi kuwa atawakomboa.
 
Vilevile amedokeza kuwa kwa namna ya kiintelijensia Israel imefanya simu leo ziweze kusambaza hotuba katika ukanda wa Gaza na hivyo akautumia muda huo kupeleka ujumbe mkali kwa Hamas kuwa ataendelea kuwadhibiti.
 
Bwana Netanyahu pia  ameingia ukumbini na vibao viwili vyenye maswali na majibu ya kuchagua japokuwa jibu sahihi kwa mujibu wake na waliojibu kuwa ni All the Above, yaani majibu yote ni sahihi. Maswali yote yalikuwa yakiwatuhumu Iran, Hamas, Al Caeda, Hezbollah na Houthi kuwa pia wanaitakia kifo Marekani na wameua watu wengi Ulaya.
 
Huenda hotuba hii ya Netanyahu ikaingia katika orodha ya hotuba tano ndefu zaidi baada ya ile ya Rais wa Marekani Donald Trump wa Marekani, Ya Mahmoud Abbass wa Palestina na Félix-Antoine Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambao wote hao walitumia zaidi ya dakika arobaini licha ya muda wa hotuba uliopangwa kuwa angalau dakika 15.