Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makamu wa Rais wa Uganda atoa wito wa ushirikiano wa kimataifa na amani katika UNGA80

Makamu wa Rais wa Uganda Jessica Rose Epel Alupo akihutubia Mjadala Mkuu wa UNGA80
UN Photo/Loey Felipe
Makamu wa Rais wa Uganda Jessica Rose Epel Alupo akihutubia Mjadala Mkuu wa UNGA80

Makamu wa Rais wa Uganda atoa wito wa ushirikiano wa kimataifa na amani katika UNGA80

Amani na Usalama

Makamu wa Rais wa Uganda, Meja Mstaafu Jessica Alupo, akihutubia Kikao cha 80 cha Mjada Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York siku ya Alhamisi, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuongeza juhudi za kudumisha amani, maendeleo na haki za binadamu.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Yoweri Kaguta Museveni, amesema, Maadhimisho haya ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa ni kumbukumbu kwa wakati muafaka ya wajibu wetu wa pamoja wa kuendeleza ushirikiano wa kimataifa na kuimarisha mshikamano wa dunia katika kushughulikia changamoto za pamoja zinazotukabili hivi sasa.”

Nafasi ya Uganda katika amani ya Kikanda

Bi. Alupo amesisitiza mchango mkubwa wa Uganda katika kuendeleza amani na usalama wa kikanda, akitaja nafasi yake ya uongozi nchini Somalia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
“Kama taifa, tumewekeza rasilimali watu na fedha katika kuendeleza amani na uthabiti bila kusita,” mesema, akitoa wito wa ufadhilii wa uhakika na ambao ni endelevu kwa operesheni za kulinda amani.
Pia lionya kwamba bila msaada huo, juhudi za kikanda za kudumisha amani zitadhoofika.

Wito wa mageuzi ya Baraza la Usalama la UN

Kuhusu uongozi wa dunia, Makamu wa Rais wa Uganda ameungama na viongozi wengine kutoka Baraza Afrika akisisitiza haja ya mageuzi ya dharura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akionesha ukosefu wa uwakilishi wa Afrika katika viti vya kudumu vya Baraza hilo.
Amesema “Afrika lazima ipate viti viwili katika kundi la Kudumu, vyenye haki na hadhi zote, na viti viwili vya ziada katika kundi la muda,”.
Alupo pia amerudia wito wa Uganda wa suluhu ya mataifa mawili kati ya Israel na Palestina na kudai kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa la Cuba.

Mzigo wa wakimbizi waipa shinikizo Uganda

Bi. Alupo katika htuba yake ameangazia pia sera ya wakimbizi ya Uganda, akieleza kuwa ni miongoni mwa za kisasa zaidi duniani, ambapo karibu wakimbizi milioni mbili wanahifadhiwa nchini humo.
Hata hivyo, ameonya kuwa kupungua kwa msaada wa kimataifa kumeweka mfumo huo katika hatari kubwa. “Kuhifadhi wakimbizi hakupaswi kuwa mzigo wa madeni. Uganda haipaswi kulazimishwa kukopa fedha ili kuhudumia watu waliokimbia vita makwao” ameambia wajumbe wa mjadala huo wa Baraza Kuu.
Amesisitiza wito wa kupatakana ufadhili wa kutosha kuweza kukidhi mahitaji ya wakimbizi hao walioingia Uganda Kusama amani na usalama.

Ahadi kwa elimu, afya na haki za binadamu

Makamu wa Rais pia alisisitiza dhamira ya Uganda katika elimu, afya na haki za binadamu, akitaja hatua ya kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo na hatua kubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Alibainisha pia kupungua kwa maambukizi ya VVU na kuongezeka kwa uwekezaji katika huduma za afya ya msingi, akisema afya ni “kiini cha mkakati wa maendeleo ya taifa letu.”

Uongozi katika harakati za kutofungamana (NAM)

Kama Mwenyekiti wa sasa wa Harakati za Kutofungamana na upande wowote (NAM), Alupo amesisitiza nafasi ya Uganda katika kuendeleza mshikamano na ushirikiano miongoni mwa nchi zinazoendelea.
Alitangaza kwamba Kampala itakuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wa NAM mwezi Oktoba mwaka huu, akisema, “Tunaunga mkono ushirikiano thabiti zaidi kati ya NAM na Umoja wa Mataifa katika kulinda maslahi ya nchi zinazoendelea.”

Wito wa kuimarisha Umoja wa Mataifa

Akihitimisha hotuba yake, Bi. Alupo amewakumbusha viongozi wa dunia kuhusu nafasi muhimu ya Umoja wa Mataifa, akisema “Haiwezekani kufikiria dunia ya leo bila Umoja wa Mataifa. Zaidi ya hapo lazima tufanye kila liwezekanalo ili kuboresha na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa. Tujitahidi tusimuache mtu yeyote nyuma tukiwa bora zaidi pamoja.”