Türk alaani kuzorota kwa hali ya haki za binadamu Sudan Kusini
Türk alaani kuzorota kwa hali ya haki za binadamu Sudan Kusini
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk,leo Ijumaa tarehe 26 mwezi Septemba 2025 ameeleza wasiwasi wake mkubwa kutokana na hali ya haki za binadamu inayozidi kuzorota nchini Sudan Kusini,kufuatia ripoti za kuaminika kwamba takribani raia 2,000 wameuawa mwaka huu pekee kutokana na kuongezeka kwa mivutano ya kisiasa na mapigano.
Kauli ya Türk imo kwenye taarifa iliyotolewa leo na na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) mjini Geneva, Uswisi ikinukuu taarifa zilirekodiwa na ofisi hiyo kuanzia mwezi Januari hadi mwezi huu wa Septemba.
Takwimu za kutisha za waathirika
Watu 1,854 wameripotiwa kuuawa, wengine 1,693 wamejeruhiwa,423 wametekwa nyara na 169 wamefanyiwa ukatili wa kingono katika muktadha wa migogoro.
Kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 59 ya idadi ya waathirika ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. “Inadhaniwa kuwa takwimu halisi ni kubwa zaidi kutokana na vikwazo vya kiusalama na vizuizi vya kufikia maeneo yaliyoathriwa na migogoro,ambavyo vimezuia uthibitishaji kamili wa matukio ya vurugu,” imesema taarifa hiyo.
Robo ya kwanza ya mwaka huu imerekodi idadi kubwa zaidi ya waathirika wa raia katika kipindi cha miezi mitatu tangu mwaka 2020, hii ni kwa mujibu wa Kitengo cha Haki za Binadamu cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS).
Kwa kiwango cha pekee, robo ya pili imeshuhudia ongezeko kubwa la waathirika kutokana na mapigano yaliyochochewa na pande za mzozo wa kivita na makundi yenye silaha, ambapo idadi ya waathirika ilipanda kutoka 144 hadi 438 ikilinganishwa na mwaka jana.
Ongezeko la vurugu za kijeshi na kikabila
Turk amesema, “Kwa kuzingatia hofu ya kuporomoka kwa Mkataba wa Amani wa mwaka 2018 ambao umehusishwa na kurejea kwa machafuko ya kiwango kikubwa,nina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya raia nchini Sudan Kusini,”
- Jeshi la Sudan Kusini limefanya operesheni za kijeshi, ikiwemo mashambulizi ya anga kiholela katika maeneo yenye watu wengi katika majimbo ya Upper Nile, Jonglei, Unity, Equatoria ya kati, na Warrap tangu Machi, na kusababisha idadi ya vifo vya raia, kuhama kwa wakazi, na uharibifu wa vituo vya matibabu, shule, na nyumba.
- Vurugu za kijamii pia zimeongezeka, na kusababisha vifo vya raia kwa asilimia 33 ikilinganishwa na mwaka uliopita, hasa kutokana na ongezeko la mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya vikundi vyenye silaha vya Dinka katika Jimbo la Warrap, na vile vile kati ya wanamgambo wa Murle kutoka Mkoa Mkuu wa Utawala wa Pibor na Dinka Bor na Lou Nuer kutoka Jimbo Kuu la Jonglei.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN pia imerekodi mauaji yanayoendelea ya kiholela yanayofanywa na vikosi vya usalama. Idadi ya watu 45 waliuawa katika hali inayoashiria kunyimwa uhai kiholela, wakiwemo wavulana wawili. Mauaji mengi yametokea katika majimbo ya Warrap na Lakes.
“Wanaume, wanawake na watoto wameuawa, wamejeruhiwa na kulazimishwa kuhama makazi yao, huku nyumba, shule, vituo vya afya na miundombinu mingine vikiharibiwa, na kuacha athari mbaya sana kwa raia. Hili haliwezi kuvumilika na lazima likome,” amesema Türk.
Wito wa utekelezaji wa amani na haki
Hata hivyo, Kamishna Türk ametoa wito: “Ninazisihi pande za Mkataba wa Amani uliohuishwa na jumuiya ya kimataifa, ikiwemo mashirika ya kikanda, kufanya kila wawezalo kuiondoa Sudan Kusini ukingoni; kuhakikisha mkataba uliopatikana kwa taabu unashikiliwa na kutekelezwa kikamilifu.”
Türk amemalizia kwa kulisihi jeshi la Sudan Kusini na wapiganaji wengine wote kuhakikisha wa raia na kutimiza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.
Mashtaka dhidi ya Makamu wa kwanza wa Rais
Mnamo tarehe 22 mwezi Septemba 2025,kesi mahakamani ilikuwa imeanza ikiwahusisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo,Riek Machar, na viongozi wengine wakuu wa chama cha Upinzani wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan (SPLM-IO).
Wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji, uhaini, uhalifu dhidi ya binadamu, na makosa mengine yanayohusiana na shambulio kwenye kituo cha Jeshi la Ulinzi la Watu wa Sudan Kusini (SSPDF) katika mji wa Nasir ulioko mpakani kaskazini-Mashariki mwa Sudan Kusini,katika jimbo la Upper Nile karibu na mpaka wa Ethiopia mwezi Machi mwaka huu.
Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN amesisitiza umuhimu wa kesi hiyo kuambatana kikamilifu na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, huku akihimiza serikali ya Sudan Kusini kuhakikisha haki ya mchakato wa kisheria na usawa wa kesi kwa washtakiwa wote inaheshimiwa,na kwamba mahakama inaweza kufanya kazi bila kuingiliwa kisiasa.