Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini: Wafadhili wa tabianchi timizeni ahadi zenu

Makamu wa Rais Josephine Joseph Lagu wa Sudan Kusini akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu.
UN Photo/Loey Felipe Makamu wa Rais Josephine Joseph Lagu wa Sudan Kusini akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu.

Sudan Kusini: Wafadhili wa tabianchi timizeni ahadi zenu

Amani na Usalama

Pamoja na kuwa nchi ya Sudan Kusini inachangia kwa kiasi kidogo kwenye uharibifu wa tabaka la ozoni lakini taifa hilo changa duniani linaendelea kuathirika kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwaacha wananchi wakiteseka.

Kutokana na hali hiyo Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Josephine Joseph Lagu akihutubia kwenye Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani amesema wakati umefika kwa wafadhili wa miradi inayoshughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi kutimiza ahadi zao.

Akieleza zaidi kuhusu masahibu wananchi wa Sudan Kusini wanayokuta nayo ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita nchi yetu imekumbwa na mafuriko ya mara kwa mara kwa upande mmoja na ukame wa muda mrefu kwa upande mwingine “na hivyo kuchangia uharibifu wa mazao, upotevu wa bayoanuwai, na watu wengi kuhama makazi yao.” Ameongeza kuwa changamoto hizi zinazidisha uhaba wa chakula, kudhoofisha uwezo wa watu kujikimu kimaisha, na kutishia utulivu wa kijamii.

“Kwenye suala hili serikali ya sudan kusini inatoa wito kwa ufadhili wa tabianchi wenye usawa na unaotabirika ili kujiimarisha na kujenga mnepo wa tabianchi. Makubaliano ya Paris na mikutano iliyofuata ya Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Tabianchi- COP ilitoa ahadi ambazo lazima ziheshimiwe.”

Wananchi wanarejea

Licha ya mabadiliko ya tabianchi , taifa hilo lililoingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka michache baada ya kupata uhuru wake linaendelea na harakati za kuhakikisha wana amani ya kudumu kupitia mikataba na makubaliano mbalimbali iliyowekwa wakati wakitafuta suluhu na kukomesha vita nchini mwao.

Makamu wa Rais Lagu amesema “Kazi inaendelea ikiwa ni pamoja na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mnamo mwezi Desemba 2026. Hadi hivi majuzi usitishaji wa kudumu wa uhasama ulionekana kuendelea kuwepo na amani kiasi kupatikana nchini kote.”

Amesema wananchi wa Sudan Kusini wameendelea kuonesha imani na taifa hilo kwani wengi waliokuwa wamekimbia wakati wa machafuko kwenda kusaka hifadhi katika nchi za jirani wameendelea kurejea, hata wale waliokuwa wakiishi ughaibuni nao wameanza kurejea.

Masuala mengine yaliyozungumzwa na Makamu huyo wa Rais wa Sudan ni pamoja na namna nchi hiyo ilivyojipanga na inavyotimiza Malengo ya Maendeleo endelevu SDGs kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, Usawa kijinsia, Miradi ya kuimarisha amani na usalama kwa kushirikiana na ujumbea wa Umoja wa Mataifa nchini humo na uwekezaji kwenye michezo ambapo wanamichezo wa nchi hiyo wamekuwa waking’ara katika michezo mbalimbali duniani ikiwemo katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2024 ambayo Makamu wa Rais Josephine Lagu amesema yanasaidia kuliunganisha taifa hilo.