Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yataka mageuzi ya UN, hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na mshikamano wa ulimwengu: UNGA80

Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango
UN Photo/Cia Pak Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango

Tanzania yataka mageuzi ya UN, hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na mshikamano wa ulimwengu: UNGA80

Amani na Usalama

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, amezihimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuimarisha mshikamano, kuimarisha taasisi za kimataifa, na kuipa kipaumbele amani na maendeleo endelevu wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake.

Akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani  Dkt. Mpango amesema kaulimbiu am waka huu “Bora Pamoja: Miaka 80 na Zaidi kwa Amani, Maendeleo na Haki za Binadamu” ni mwito wa kurejea katika dira ya waanzilishi wa Umoja huo. Amekemea, “vita vya kinyama,” na ukosefu wa haki unaoongezeka, akisisitiza kwamba “amani ndiyo shauku kuu ya binadamu” na lazima ifuatwe bila kuchoka kupitia mazungumzo na sheria za kimataifa.
 

Afrika katika Baraza la Usalama

 
Katika hotuba yake, Makamu huyo wa Rais wa Rais amesisitiza msimamo wa muda mrefu wa Afrika wa kudai angalau viti viwili vya kudumu vyenye kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa Makubaliano ya Ezulwini. Pia ametaka mageuzi ya haraka ya taasisi za kifedha za kimataifa, ikiwemo mifumo ya ukadiriaji wa deni na viwango vya mkopo, ili kutoa nafasi kubwa zaidi kwa Afrika na kufungua mitaji kwa ajili ya uwekezaji katika miundombinu, elimu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
 

Tanzania na utekelezaji wa SDGs

 
Akitaja mafanikio ya Tanzania katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Dkt. Mpango amesema vifo vya akina mama wakati wa kujifungua vimepungua kwa kiasi kikubwa, upatikanaji wa maji safi na salama umeongezeka, na karibu vijiji vyote nchini vimeunganishwa na umeme. Hata hivyo, ameonya kuwa zaidi ya asilimia 80 ya malengo ya kimataifa ya SDGs hayako katika mstari, kutokana na pengo la kifedha la dola trilioni 4 kwa mwaka.
 

Mabadiliko ya tabianchi

 
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, aliitaka jamii ya kimataifa kutumia vyema fursa ya Mkutano wa COP30 nchini Brazil kuhakikisha ahadi zinatekelezwa, ikiwemo mfuko wa fidia kwa hasara na madhara. Amesisitiza haja ya ufadhili nafuu wa muda mrefu, uhamishaji wa teknolojia na masharti ya haki ya kibiashara, huku akitaja uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 inayolenga malengo ya SDGs.
 

Dhamira ya Tanzania katika Baraza la Usalama

 
Dkt. Mpango amethibitisha tena dhamira ya Tanzania kwa amani ya dunia, akitangaza kugombea kiti cha muda kisicho cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2029–2030.
 
Pia akalaani vikwazo vya upande mmoja, akaonesha mshikamano na nchi zilizowekewa vikwazo kama Zimbabwe na Cuba, na kurudia msimamo wa Tanzania wa kuunga mkono haki ya Wapalestina na Wasaharawi ya kujitawala.
 
Akihitimisha hotuba yake, Makamu wa Rais Mpango amenukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewataka viongozi kutokaa kimya mbele ya dhuluma. Alilaani unyonyaji wa rasilimali za Afrika unaofanywa na kampuni za kimataifa na kukemea ongezeko la matumizi ya kijeshi, akilitaja kama kosa la kimaadili linaloondoa rasilimali zinazoweza kutumika katika maendeleo endelevu.