Haiti: Kiongozi wa mpito atoa wito wa hatua za haraka za kimataifa kukabili mgogoro wa usalama
Haiti: Kiongozi wa mpito atoa wito wa hatua za haraka za kimataifa kukabili mgogoro wa usalama
Rais wa Baraza la Rais la Mpito la Haiti, Anthony Franck Laurent Saint Cyr, ametoa wito mbele ya Mjadala Mkuu waBaraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akionya kwamba Haiti iko katikati ya tishio kubwa la kiusalama la kikanda na ametaka hatua za haraka na za pamoja za kimataifa zichukuliwe kuinusuru.
Saint Cyr. Amesema “Njia zilizoshindwa zamani hazitatupatia suluhu kwa Haiti leo. Ni lazima kusikiliza sauti ya wananchi wa Haiti na kukubali suluhu mpya.”
Ameonya dhidi ya hatua za nusu nusu, akisisitiza kuwa ukimya au kutochukua hatua kutazidisha matatizo ya nchi hiyo.
“Jumuiya ya kimataifa lazima kwa kushirikiana na Haiti, iwekeze rasilimali kubwa si hatua za nusu nusu, bali hatua madhubuti, zilizoratibiwa na za haraka. Ukimya au kutofanya chochote si chaguo. Ni lazima tuchukue hatua mara moja.”
Jukumu la ujumbe wa kimataifa linatetereka
Kiongozi huyo wa Haiti ameeleza udhaifu wa ujumbe wa kimataifa uliopo sasa unaotakiwa kuleta utulivu nchini humo.
“Leo, kati ya askari 2,500 waliokuwa wanahitajika na kuahidiwa awali katika ujumbe uliowasili Haiti, ni elfu moja pekee ndio wako ardhini Haiti,” amesema.
“Ujasiri wao, ukiwa umeunganishwa na jitihada zetu wenyewe, haujafaulu kudhibiti mgogoro wa kiusalama.”
Haiti katikati ya tishio la kikanda
Akiuita mgogoro huo hatari inayozidi mipaka ya Haiti, Saint Cyr ameonya kuhusu mashirika yenye nguvu ya wahalifu yanayosambaza machafuko kote katika kanda hiyo.
Ameongeza kuwa “Ni lazima tukubali ukweli. Haiti iko katikati ya tishio kubwa la kiusalama la kikanda ambalo halijawahi kushuhudiwa. Mitandao yenye silaha nzito na yenye nguvu inajaribu kuudhoofisha nchi na kutawala uchumi wa eneo letu la pamoja. Mstari mpya wa mbele wa mapambano haya uko Haiti. Tukishindwa kuwakabili katika ardhi yetu, itakuwa ni ndoto kudhani kwamba tunaweza kuwadhibiti sehemu nyingine za kanda.”
Wito wa kuundwa kwa kikosi chenye nguvu na udhibiti mkali zaidi
Saint Cyr amesisitiza umuhimu wa kuundwa kwa haraka kwa kikosi chenye nguvu, chenye mamlaka iliyo bayana, vifaa vya kutosha na msaada wa kifedha.
Ametanabaisha kuwa “Leo, ni lazima kuhamasisha kuundwa kikosi madhubuti, chenye mamlaka ya wazi na chenye vifaa na nyenzo, na msaada wa kifedha wa kutosha”.
Pia ametaka ushirikiano wa kimataifa kuimarishwa ili kukomesha mtiririko wa silaha, risasi, dawa za kulevya na fedha zinazofadhili magenge ya uhalifu ya Haiti.
Amesisitiza “Amani inaweza kurejeshwa tu iwapo washirika wetu wa kikanda watahakikisha, kupitia hatua halisi, kwamba maeneo yao hayatumiwi tena kama chimbuko au njia za kupitisha biashara hizi haramu.”
Wito kwa Baraza la Usalama
Kiongozi huyo wa mpito wa Haiti ametaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liunge mkono azimio la kuanzisha kikosi maalum cha kupambana na magenge ya uhalifu. “Tunaiomba jumuiya nzima ya kimataifa kuwa na mshikamano, na hasa wanachama wa Baraza la Usalama wajitolee kupiga kura ya kuunga mkono azimio la kuanzisha kikosi cha kudhibiti magenge u ya uhalifu ,” amesema.
Fidia na haki ya kihistoria
Akihitimisha hotuba yake, Saint Cyr amekaribisha hatua ya hivi karibuni ya Ufaransa kutambua dhuluma za kihistoria dhidi ya Haiti.
Amesema “Tunakaribisha tamko la Rais wa Ufaransa linalotambua haja ya kuanzisha nafasi za mazungumzo na ukweli wa kihistoria, pamoja na azimio la tarehe 5 Juni 2025 la Bunge la Taifa la Ufaransa linalotambua dhuluma ya kodi hii,”.
Amebainisha kuwa Haiti tayari imeanzisha Kamati ya Taifa ya Fidia na Marejesho, na akatoa wito hatua hizo za kimkakati zifuatwe na hatua halisi.