Mfalme Mswati III apendekeza Kamati Maalum za muda ili kutatua migogoro ya kimataifa
Mfalme Mswati III apendekeza Kamati Maalum za muda ili kutatua migogoro ya kimataifa
Akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani Alhamisi ya Septemba 25, Mfalme Mswati III wa Eswatini ametoa wito wa kuundwa kwa kamati maalum za muda ili kushughulikia migogoro ya kimataifa.
Katika hotuba yake iliyozingatia maudhui ya mkutano wa mwaka huu, "Pamoja ni Bora: Miaka 80 na zaidi kwa amani, maendeleo, na haki za binadamu," mfalme huyo amesisitiza kuwa kamati hizo ni muhimu ili kurejesha dhamira ya awali ya Umoja wa Mataifa ya kukuza amani na kuzuia mateso.
Mfalme Mswati III ameonesha wasiwasi wake kwamba Umoja wa Mataifa umepoteza mwelekeo katika kushughulikia migogoro kwa ufanisi.
Uwakilishi wa kamati uwe mpana
“Napendekeza kuweko kwa kamati mpya na zenye uwakilishi wa haki kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo Afrika, Mashariki ya Kati, na Ulaya. Vyombo hivi vikiungwa mkono na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, vipewe jukumu la kutembelea maeneo ya migogoro, kushirikiana na jamii za eneo hilo, na kupatanisha mijadala ili kupata suluhisho la amani,” amesema Mfalme huyo ambaye wakati anaingia wapambe wake walipiga mbiu.
Mfalme Mswati III ametoa mifano maalum ya maeneo ambapo kamati hizi zinaweza kuingilia, akitaja migogoro nchini Sudan, Sudan Kusini, Somalia, Sahel, na Maziwa Makuu barani Afrika.
Pia amesisitiza umuhimu wa wao kuwezesha mazungumzo katika Mashariki ya Kati, akipendekeza wawashirikishe wapalestina na waisraeli ili kupata njia ya amani. Katika muktadha wa mzozo kati ya Urusi na Ukraine, amesema kamati hizi zinaweza kupatanisha mijadala na kuripoti kwa Umoja wa Mataifa na mapendekezo yanayotekelezwa ili kumaliza vita.
Maendeleo ya kiuchumi
Zaidi ya utatuzi wa migogoro, Mfalme Mswati III amesisitiza umuhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kushughulikia changamoto za kimataifa kama vile umaskini na migogoro ya kifedha.
Amesema kuwa UN sasa inapaswa kuzingatia kuunga mkono uchumi wa dunia ili kuunda mazingira ya amani ya kudumu, hasa baada ya janga la coronavirus">COVID-19.
Mfalme pia amerejelea wito wa muda mrefu wa Eswatini wa marekebisho ya mundo wa Umoja wa Mataifa ili uwe na uwakilishi zaidi wa nchi zote wanachama.
“Marekebisho, hasa ndani ya Baraza la Usalama, ni muhimu ili kuhakikisha uhalali na ufanisi wa chombo hicho.”
Amekumbusha umuhimu wa mataifa kufanya kazi kwa pamoja kupitia Umoja wa Mataifa kwa kuwa chombo hicho ndio chenye nguvu zaidi cha kushughulikia changamoto za kimataifa zinazovuka mipaka.