Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia: Ufadhili tete kwa ATMIS, Katibu Mkuu UN atoa wito mzito

Maafisa wa ATMIS na Jeshi la Polisi la Somalia wakipiga doria mtaani Mogadishu, Somalia, wakati wa Ramadhani, huku afisa mmoja akikagua injini ya gari.
ATMIS / Mukhtar Nuur Askari polisi wanaohudumu chini ya ujumbe wa mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) wakiwa kwenye doria ya pamoja na polisi wa Somalia ili kuimarisha usalama wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani tarehe 20 Machi mwaka 2023 kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. (Maktaba)

Somalia: Ufadhili tete kwa ATMIS, Katibu Mkuu UN atoa wito mzito

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, akizungumza leo 25 Septemba 2025 New York Marekani katika Mkutano wa ngazi za juu, mbele ya viongozi wa kimataifa ameeleza kuwa dunia inashuhudia wakati wa matumaini na hatari kwa ajili ya mpito wa Serikali ya Somalia.

Katika hotuba yake, Guterres amesisitiza kuwa Ujumbe wa Mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, ATMIS unaendelea kuwa muhimu kwa mafanikio ya nchi hiyo, lakini inakabiliwa na changamoto kubwa za kifedha.

Kwa sasa, Guterres amebainisha kuwa hakuna mpango wa wazi wa ufadhili kwa mwaka 2025 na kuendelea. Akifichua hali ya sasa ya kifedha, Amesema kuwa ni dola milioni 24.6 pekee ambazo zinakuwa zimeahidiwa dhidi ya mahitaji ya dola milioni 196, huku dola milioni 20 zikitolewa na Muungano wa Afrika.

Wakati huo huo, nchi zinazochangia wanajeshi zinaendelea kuwa mstari wa mbele licha ya kutolipwa posho kwa kipindi cha miezi 15, jambo ambalo Guterres ameliita hali isiyokubalika.

“Haiwezekani kuwaomba wale wanaohatarisha maisha yao kupambana na Al-Shabaab  na ambao wamepoteza wenzao wengi  kufanya kazi bila malipo,” amesema Guterres kwa msisitizo.

Guterres ameeleza kuwa fedha hizi zinawakilisha zaidi ya bajeti  zinamaanisha ulinzi wa raia, kufanikisha utoaji wa misaada ya kibinadamu, kuunga mkono vikosi vya usalama vya Somalia katika kipindi hiki cha mpito na kuimarisha maandalizi ya uchaguzi ujao.

Pia amesisitiza kuwa, rasilimali hizi  zinahitajika kutekeleza majukumu yaliyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.

Akiwa mbele ya wajumbe wa kimataifa, Katibu Mkuu  anawakumbusha  kuwa Somalia imetoka  katika hali ya migogoro hadi mafanikio ya kisiasa na sasa imekuwa na sauti ndani ya Baraza la Usalama. Ameelezea kuwa hatua hizi zinaakisi ujasiri wa watu wa Somalia pamoja na mchango wa muda mrefu wa Umoja wa Afrika na nchi zinazochangia vikosi.

Ufadhili wa Misheni si tu mstari wa bajeti wa kawaida  ni suala la kulinda raia, kushughulikia tishio la ugaidi na kuhakikisha ustawi wa Somalia na kanda nzima,” ameongeza.

Guterres ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufanya mambo mawili muhimu:

kwanza, ameomba  pengo la ufadhili kwa mwaka 2025  linazibwa mara moja.

Pili, amesisitiza  umuhimu wa kuwa na mfumo wa uhakika wa ufadhili wa muda mrefu kwa ajili ya misheni hiyo.

Anakumbusha kuwa Azimio la Baraza la Usalama namba 2719  limeunda msingi wa kuchangia kifedha kwa operesheni za amani zinazoongozwa na Umoja wa Afrika kupitia michango ya lazima, lakini utekelezaji wake bado haujafanikiwa.

Kwa kumalizia, Guterres ametoa wito kwa wafadhili, taasisi za kifedha za Kimataifa na wadau wapya  kujitokeza. Anasema kuwa Somalia imepiga hatua kubwa na haiwezi kuruhusiwa kurudi nyuma.

Kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa, tunaweza  kusaidia kujenga Somalia salama, kanda iliyo na  utulivu na dunia iliyo salama zaidi.