Hakuna amani kama hakuna haki na hakuna haki kama Palestina haiko huru: Abbas
Hakuna amani kama hakuna haki na hakuna haki kama Palestina haiko huru: Abbas
Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, leo amehutubia Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80 kwa njia ya video baada ya Marekani kushindwa kumpa visa ya kuingia nchini humo.
Abbas ameanza hotuba yake kwa kulaani ukatili unaoendelea Gaza, akisema: “Nawaeleza baada ya takriban miaka miwili ambapo watu wetu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza wamekabiliwa na vita vya janga kubwa, uharibifu, kufuriushwa makwao, na njaa vinavyosababishwa na nguvu za ukoloni za Israel.”
Upanuzi wa makazi ya Walowezi
Amemlaumu “serikali ya kigeni ya Kiyahudi” kwa kuendeleza sera zake za kikoloni Ukingo wa Magharibi kupitia upanuzi haramu wa makazi ya Walowezi. Abbas pia amelaumu mpango wa Israel wa kujenga Israeli Kubwa, ambao ameueleza kuwa ni upanuzi katika mataifa ya Kiarabu yenye uhuru, akiuita ni wa “hatari sana” na ni“uvunjaji mkubwa wa sheria za kimataifa.”
Shambulio la Hamas na kuachiliwa mateka
Rais wa Palestina Abbas amethibitisha kupinga kwake shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na Hamas, lililolenga raia wa Israeli na kuwateka nyara, akisema kuwa vitendo hivyo “havihusishi watu wa Palestina wala mapambano yao ya haki kwa uhuru na uhuru wa kuwa na taifa.”
Ametaka mateka wote wanaoshikiliwa waachiliwe na kuitaka Isrfael bila masharti kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza ambako amesema maelfu ya watu wanakufa kwa njaa na magonjwa bila huduma za msingi kwa uhai wa binadamu.
Kutambuliwa na uanachama kamili wa UN
Rais Abbas amebainisha mbele ya mjadala huo mkuu wa kimataifa wa ngazi ya juu kuhusu kusuluhisha suala la Palestina na kutekeleza suluhisho la mataifa mawili yatakayoishi pamoka kwa amani na utulivu.
Aliwashukuru mataifa yote ambayo hivi karibuni yametambua Jimbo la Palestina na kuwahimiza wengine kufanya vivyo hivyo.
Abbas pia ameitaka dunia kusaidia Palestina kupata uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, akisisitiza: “Tulitambua haki ya Israel kuwepo mwaka 1988 na tena mwaka 1993, na bado tunatambua. Hivyo ni haki taifa la Palestina likatambuliwa pia”
Kujitenga na Hamasi
Amesisitiza kuwa Ukanda wa Gaza utaendelea kuwa sehemu ya Taifa la Palestina na tuko tayari kuwajibika kikamilifu kwenye uongozi na usalama wa eneo hilo. Hamas hawatokuwa na jukumu lolote kwennye utawala.”
Kiongozi huyo wa Palestina amesema hakutakuwa na amani popote duniani kama hakuna haki na kwa Palestina amesema hakutakuwa na haki kama Palestina haitokuwa huru, hivyo ameisihi jumuiya ya kimataifa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha damu haiendelei kumwagika Gaza na watu wa Ukanda huo wanapewa haki yao.