Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia: Afrika haiwezi kuachwa nje tena ni wakati wa kuwa na usawa wa kimtazamo duniani

Hassan Sheikh Mohamud, Rais wa Somalia akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la UN
UN Webcast Hassan Sheikh Mohamud, Rais wa Somalia akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la UN

Somalia: Afrika haiwezi kuachwa nje tena ni wakati wa kuwa na usawa wa kimtazamo duniani

Amani na Usalama

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, ametoa hotuba yenye uzito mkubwa kwenye Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80 hii leo akitaka nchi wanachama kujitolea upya kwa misingi ya usawa, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa.

Ameonya kuwa dunia ya leo inatembea “katika njia ya giza na hatari” ambapo migogoro inatatuliwa kwa nguvu badala ya sheria.

Amewakumbusha nchi wanachama kwamba “Umoja wa Mataifa ulianzishwa ili kuendeleza amani, usalama, maendeleo na ustawi wa dunia. Baada ya miaka 80, tungekuwa tayari bora zaidi pamoja, siyo bado kujitetea kwa nini tuwe bora pamoja.”

Changamoto za dunia zinahitaji umoja

Rais Mohamud ameweka bayana hali ngumu ya ongezeko la udhaifu, umaskini na njaa, duniani akitaja takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani WFP zikionesha watu milioni 319 wanakabiliwa na njaa kali katika nchi 67.

Amesema “Haya ni mambo makubwa yanayopaswa kutufanya tusimame na kutafakari, Kama tumeazimia kweli kufanikisha ustawi kwa wote, lazima tuongeze juhudi katika kuimarisha mshikamano na ushirikiano wa kimataifa.”

Ameonya kuwa bila hatua za haraka, dunia itashindwa kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu kufikia mwaka 2030.

Sauti ya Afrika Lazima Isikike

Kiongozi huyo wa Somalia amesisitiza kuwa kutoshirikishwa kwa Afrika kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ni “ukosefu wa haki usiopingika.”

Ikiwa na mataifa 54, Afrika ndiyo bara pekee lisilo na uwakilishi wa kudumu. “Hali hii haiwezi kuendelea,” amesema Mohamud. “Kutoijumuisha Afrika katika uanachama wa kudumu ni kutoitendea haki, ni kitendo cha kizamani na hakiwezi tena kuhalalishwa. Usawa wa kweli na uhalali wa dunia unataka Afrika ijumuishwe kikamilifu kwenye maamuzi ya Umoja wa Mataifa.”

Maendeleo ya Somalia dhidi ya ugaidi

Akiangazia hali ya kitaifa, Mohamud ameeleza mabadiliko ya Somalia tangu mwaka 2012 kama ushahidi kuwa mshikamano wa kimataifa unazaa matunda. “Somalia ni uthibitisho kuwa mshikamano wa kimataifa unaweza kuifanya dunia kuwa salama,” amesema, huku akipongeza vikosi vya Somalia kwa kujitoa mhanga katika kupambana na makundi ya kigaidi ya Al-Shabaab na ISIS. Amesisitiza kuwa “Kamwe hatutakubali kushindwa na magaidi waoga,” akiahidi kuendelea kuimarisha usalama wa taifa kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa.

Demokrasia na mageuzi ya uchumi

Rais huyo ameeezea kuhusu maandalizi ya Somalia ya kufanya uchaguzi wa kidemokrasia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 57, akikitaja kama kurudi kwa kihistoria katika demokrasia.

Amesema “Hakuna kilicho bora kuliko taifa linaloongozwa na wananchi na sheria”.

Kuhusu uchumi, Mohamud ameeleza hatua za kumaliza madeni, mageuzi ya mapato ya ndani na ushirikiano wa kibiashara kama hatua muhimu kuelekea kujitegemea, lakini akaonya kuwa mataifa yanayoendelea yanakabiliwa na “mshtuko mara tatu wa madeni makubwa, gharama kubwa za mikopo, na majanga ya mara kwa mara.”

Somalia haichangii tabianchi lakini inalipa gharama zake

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Mohamud alitoa wito wenye nguvu, akieleza kuwa ni “hali halisi ya maisha yanayovurugwa na kuharibiwa” kwa Wasomali. “Sisi hatuchangii lolote kubwa la uzalishaji wa hewa chafuzi duniani, lakini tunabeba athari kali zaidi changamoto hiyo,” amesema.

Ameitaka dunia tajiri kutimiza ahadi zake za fedha za tabianchi, akibainisha kuwa Afrika inapokea chini ya asilimia 3 ya fedha hizo licha ya kuathiriwa vibaya zaidi. “Mataifa yaliyo mstari wa mbele kama Somalia hayawezi kuachwa yakikabiliana na janga hili peke yake,” amehitimisha hotuba yake, akisisitiza msaada wa haki, rahisi na wa kupatikana kwa haraka.