Comoro yaitaka dunia kuchukua hatua kuhusu Palestina, ikisema kisasi cha Israel ni mauaji ya kimbari
Rais wa Comoro Azali Assoumani akihutubia Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA80
Comoro yaitaka dunia kuchukua hatua kuhusu Palestina, ikisema kisasi cha Israel ni mauaji ya kimbari
Amani na Usalama
Akihutubia viongozi wa dunia katika kikao cha 80 cha Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA80, Rais Azali Assoumani wa Muungano wa Comoros ameonya kuwa binadamu wanazidi kupotea kutoka kwenye dira ya amani na haki iliyoahidiwa na Malengo ya Maendeleo Endelevu.
“Ikiwa imesalia miaka mitano kabla ya muda kuisha, ni dhahiri kwamba dunia siyo ya haki zaidi, yenye amani zaidi au ya usawa zaidi,” amesema. “Kinyume chake, pengo limeongezeka, migogoro imetamalaki, na ubinadamu unasogea mbali zaidi na dira iliyowahi kutuongoza.”
Mauaji ya kimbari mbele ya macho ya dunia
Kiongozi huyo wa Comoros ametoa moja ya shutuma kali zaidi dhidi ya hatua za Israel huko Gaza. Akitambua mashambulizi ya Oktoba 7 nchini Israel kama ya kinyama, lakini amesema kisasi kilichofuatia kimevuka mipaka yote ya maadili na sheria.
“Hatua zisizo na uwiano zilizoighubika Gaza tangu wakati huo ni mauaji ya kimbari,” amesema. “Asilimia 80 ya waathirika ni watoto, wazee au wagonjwa. Wameuawa kwa mabomu ambayo hayakuacha salama hospitali, vituo vya misaada, shule, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa au waandishi wa habari.”
Suluhisho la mataifa mawili ndio njia pekee ya amani
Assoumani amethibitisha “msimamo wa kudumu wa Comoros wa kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili, likiwa na Yerusalemu Mashariki kama mji mkuu wa Palestina”.
Amewashukuru mataifa kama Ufaransa kwa kutambua taifa la Palestina. “Hii si zawadi kwa Hamas,” amesisitiza. “Kuwa na taifa la Palestina linalotambuliwa kutawawezesha wananchi wa Palestina kutimiza majukumu yao chini ya sheria za kimataifa. Amani ndiyo dhamana bora ya kuimarisha amani.” Ameonya kuwa historia haitasamehe ukimya, “Hakuna atakayesema tena, Sikujua. Historia itakuwa hakimu wetu.”
Nafasi ya Afrika katika meza ya dunia
Akigeukia bara la Afrika, Rais Assoumani ametaka mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akiungana na viongozi wengi kutoka Afrika wenye msimamo huo ili bara hilo lipate nafasi yake halali. “Miaka 65 baada ya uhuru, Afrika ni bara lenye watu zaidi ya bilioni 2. Sasa Afrika lazima ipate hatimaye nafasi yake halali ndani ya Baraza la Usalama,” amesema. Amekumbusha kipaumbele chake akiwa mwenyekiti wa Muungano wa Afrika, hususan mpango wa kunyamazisha mtutu wa bunduki na kutekeleza Ajenda ya 2063 ya Muungano wa Afrika AU.
Amesema “Afrika iliyoungana, yenye ustawi, yenye amani na inayojitawala yenyewe, inaleta kabisa ari ya kikao hiki”.
Mgogoro wa Mayotte majeraha ya mwisho ya ukoloni Afrika
Rais wa Comoro pia ameamsha tena suala la mzozo wa eneo na Ufaransa juu ya kisiwa cha Mayotte, akilaani unyanyasaji unaoripotiwa dhidi ya wahamiaji wa Comoro. “Ukweli mzito ulifichuliwa na jarida la Le Monde, ambalo liliripoti njama za makusudi na polisi wa Mayotte, kuzamisha mara kwa mara boti na kusababisha vifo,” amesema.
“Tunaomba Ufaransa, kama nguvu inayokalia eneo hilo, kusitisha operesheni hizi, kuwaadhibu wahusika wa ukatili huu, ili haki itendeke na utu wa maisha ya binadamu uheshimiwe.” Ameliita suala la Mayotte kuwa “moja ya majeraha ya mwisho ya ukoloni Afrika.”
Amekumbusha kuwa “Napenda kurejelea azimio lililopitishwa na Baraza Kuu katika kikao chake cha 26 lililotangaza Bahari ya Hindi kuwa eneo la amani, lisilo na silaha za nyuklia na kambi za kijeshi. Hata hivyo, hata leo, tamaa za washindani zinatishia utulivu huu. Kwa hivyo, ninashutumu vikali na kulaani mradi wowote wa kujenga kambi ya kijeshi huko Mayotte, kisiwa cha Comoro ambacho, kwa bahati mbaya, bado kiko chini ya utawala wa Ufaransa.”
Kisiwa kidogo, sauti ya dunia
Rais Assoumani amehitimisha hotuba yake kwa kusisitiza tishio la mabadiliko ya tabianchi kwa mataifa madogo ya visiwa yanayoendelea kama Comoro. Ametaka “upatikanaji wa haki na rahisi wa fedha za kukabiliana na tabianchi” na kuomba uwekezaji katika mpango wa maendeleo wa taifa lake.
“Taifa letu bado ni changa, lakini linabebwa na ndoto zake,” amesema. “Watu wa Comoros wanajivunia historia yao na wana imani na mustakabali wao. Tunaendelea kushikamana na Mkutano huu, ambao unaakisi matarajio yetu ya pamoja ya amani, haki na maendeleo.”