Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais wa Namibia akihutubia  akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la UN

Namibia ni simulizi ya mafanikio makubwa zaidi ya UN - Rais Netumbo

UN Webcast
Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais wa Namibia akihutubia akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la UN

Namibia ni simulizi ya mafanikio makubwa zaidi ya UN - Rais Netumbo

Masuala ya UM

Rais Netumbo Nandi-Indaitwa wa Namibia amehutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, (UNGA80) jijini New York Marekani  ambapo pamoja na mambo mengine amesihi jamii ya kimataifa kutambua mchango wa wanawake na wanaume wanaohudumu chini ya bendera ya buluu ya Umoja wa Mataifa wakihaha huku na kule kusongesha amani.

Ameweka bayana kuwa safari ya Namibia katika kupata uhuru wake mwaka 1990 ni moja ya simulizi bora zaidi za mafanikio ya Umoja wa Mataifa akisema “ni kupitia shirika hili ambapo watangulizi wetu wa mapambano ya kusaka uhuru waliwasilisha maombi ya kutokomezwa kwa ubaguzi wa rangi na ukoloni nchini Namibia,” amesema Rais Netumbo.

Amegusia pia yeye ni mwenyewe binafsi kuwa safari yake iliyomwezesha hadi sasa kuwa rais wa 5 wa taifa hilo la kusini mwa Afrika, kuwa ilianzia mwaka 1974 ndani ya Umoja wa Mataifa akihudumia nchi yake na Afrika katika nyadhifa mbali mbali.

Wasichana na wanawake kuweni na ndoto

Ni katika muktadha huo akasema, “mimi ni mwanamke hivyo ninamtia moyo kila msichana na mwanamke kwa kusisitiza kuwa ndoto yako ni muhimu. Maono yako yanahitajika kwa kuwa yatakufungulia njia kufika ngazi ya juu ya taasisi yoyote ile.”

Rais huyo wa Namibia ambaye mara baada ya kukaribishwa kwenye mimbari kuzungumza alipigiwa vigelegele na shangwe kutoka kwa wajumbe wa mkutano, amezungumzia pia masuala akili mnemba au akili unde, kwa kiingereza Artificial Intelligence.

Akili unde isiengue binadamu

Amesema, “Namibia inatambua maendeleo ya teknolojia, katika nyanja zote, lakini mipaka ya kimaadili lazima iheshimiwe.”

Amesisitiza kuwa akili unde isichukue nafasi ya binadamu kwa kupitisha maamuzi au kutekeleza majukumu yake.

“Hivyo tunatoa wito wa kuweko kwa viwango vya kimataifa vya kuhakikisha matumizi ya akili unde yanasalia ya uwazi na haki kwa ubinadamu,” amesema.