Nchi zaweka bayana ahadi na hatua zinazochukua kukabilii mabadiliko ya tabianchi
Nchi zaweka bayana ahadi na hatua zinazochukua kukabilii mabadiliko ya tabianchi
Viongozi kutoka zaidi ya nchi 100 wametangaza ahadi zao au kile ambacho wanatekeleza kuhakikisha kwamba wanakabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabiachi. Hatua kuanza kutumia nishati safi na salama hali kadhalika kupanda miti.
Ahadi hizo wametoa katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu hatua kwa tabianchi ulioitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kwa kushirikiana na Rais Luiz Inácio Lula Da Silva wa Brazil, ambaye ni mwenyeji wa mkutano wa COP30 utakaofanyika Novemba katika jiji la Belém lililoko eneo la msitu mnene wa Amazon.
Mshikamano dhidi ya tabianchi ni dhahiri– Bi. Mohammed
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, amesema, “zaidi ya nchi 100, takribani 40 kati yao zikiwakilishwa na wakuu wa nchi na serikali, zimekuja kutangaza au kusisitiza tena malengo yao mapya ya tabianchi au nia yao ya kuyawasilisha rasmi katika COP30.”
Bi. Mohammed amesema hatua hiyo inatuma ujumbe wa umoja, matumaini na imani kuwa suala la tabianchi bado ni kipaumbele, “na kuna ahadi kutoka kwa serikali, sekta ya biashara na fedha kuchukua hatua.”
Ameongeza kuwa “matamko ya leo kuhusu Michango ya Kitaifa ya kukabili mabadiliko ya tabianchi, NDCsni hatua chanya kuelekea mkutano wa COP30 huko Belém.
Viongozi kutoka kote duniani wamesimama pamoja kuonesha kuwa “hata katika nyakati za mgawanyiko na hali ya kutokuwa na uhakika, dhamira na azma ya kupambana na janga la tabianchi bado ipo na ni thabiti.”
Mwanzoni mwa mkutano, wanasayansi wakuu wa tabianchi Johan Rockström na Katharine Hayhoe walitoa tathmini kali kuhusu juhudi za dunia hadi sasa katika kutekeleza Mkataba wa Paris, mkataba wa kihistoria wa mwaka 2015 unaolenga kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiasi juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.
Bado joto linaongezeka, lakini tunaweza kuchukua hatua - Wataalam
Miaka kumi baada ya Mkataba wa Paris, utoaji wa gesi chafuzi zinazochangia ongezeko la joto duniani unaendelea kuongezeka, na mwaka jana mabadiliko ya joto duniani kwa mwaka yalivuka nyuzi joto 1.5 kwa mara ya kwanza.
“Hili ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa,” amesema Profesa Rockström, mwanasayansi mkuu katika shirika la Conservation International. “Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba ongezeko la joto linaonekana kuharakishwa, likitangulia hata kasi ya utoaji wa gesi chafuzi.”
Hata hivyo, bado inawezekana kufikia lengo la nyuzi joto 1.5, na wataalamu hao wawili wamebainisha majawabu mbalimbali, ikiwemo kuhama kutoka kwa nishati ya mafuta ya kisukuku hadi vyanzo safi vya nishati, pamoja na kubadilisha mifumo ya chakula ili kuondoa upotevu.
“Hatuwezi kuzuia janga hili peke yetu. Lakini kwa pamoja, tunaweza. Kwa kuweka malengo madhubuti zaidi, kuharakisha muda wa utekelezaji, na kutoa ahadi za kina zaidi,” amesema Profesa Hayhoe, mshindi wa Tuzo ya Mabingwa wa Dunia ya UN ya mwaka 2019.
Nishati safi ndio jawabu, wakati wa kuchukua hatua ni sasa
Mapema asubuhi akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametaka viongozi kupatia kipaumbele nishati safi na salama.
“Dunia inaingia katika enzi mpya ya fursa, ambapo nishati safi si tu chanzo cha umeme cha haraka na cha gharama nafuu, bali pia ni kichocheo cha ajira, ukuaji wa uchumi, na usalama wa nishati,” amesema Katibu Mkuu.
Ametolea mfano China na India ambazo zimekwenda kwa kasi kubwa kwenye kufanikisha nishati salama na kusongesha maendeleo yao, baada ya kufikia malengo muhimu ya nishati mbadala miaka kadhaa kabla ya muda uliopangwa.
Guterres amebainisha maeneo matano muhimu yanayohitaji hatua za haraka:
- Mpito wa nishati: Kuongeza uwekezaji katika nishati mbadala, miundombinu ya gridi na uhifadhi, hasa katika nchi zinazoendelea.
- Kupunguza methani: Kupunguza hewa chafu kutoka shughuli za uchimbaji wa mafuta ya kisukuku, ambapo upunguzaji wa asilimia 40 unaweza kufikiwa bila gharama ya ziada.
- Kulinda misitu: Kukomesha ukataji wa misitu ili kuhifadhi maeneo muhimu ya kunyonya kaboni.
- Kupunguza hewa ya ukaa viwandani: Kuongeza matumizi ya teknolojia safi katika sekta za chuma, saruji, na usafirishaji mzito.
- Haki kwa tabianchi: Kuwezesha ufadhili kwa mataifa yaliyo hatarini yanayokumbwa na majanga ya tabianchi.
Kusonga mbele
Akigusia COP30, Guterres ametoa wito wa kuwepo kwa “mpango wa kimataifa wa kukabiliana na tabianchi bila kudhuru wengine,” na kuzihimiza nchi kuwasilisha mipango mipya ya tabianchi kwa mwaka 2035.
Amesisitiza umuhimu wa kurekebisha mifumo ya kifedha ya kimataifa, kuongeza ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kuanzisha kikamilifu Mfuko wa Hasara na Madhara.
“COP30 lazima ioneshe njia ya kuaminika ya kuhamasisha dola trilioni 1.3 kila mwaka kwa ajili ya ufadhili wa tabianchi kufikia 2035,” amesema, akihimiza vyanzo bunifu vya ufadhili na uwajibikaji thabiti.
Muongo wa kuongeza kasi
Kwa kuwa Mkataba wa Paris tayari umeanza kupunguza mwelekeo wa ongezeko la joto, Guterres amesema muongo ujao lazima uwe wa kuongeza kasi. “Tupo katika alfajiri ya enzi mpya ya nishati. Ni lazima tuchangamkie fursa hii,” amesema..
Guterres amekumbusha kuwa bado inawezekana kudhibiti ongezeko la joto duniani hadi kufikia nyuzi joto 1.5°C — lakini ni lazima mataifa yatende haraka na kwa maamuzi thabiti.
“Sayansi inatulazimisha kuchukua hatua. Uchumi pia unatulazimisha,” amesema, akibainisha kuwa uwekezaji katika nishati safi sasa umeongezeka mara mbili ya ule wa mafuta ya kisukuku, licha ya ruzuku zinazoendelea zinazopotosha masoko.
Kauli ya Rais wa Brazil
Kwa upande wake, Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva amesema, “Kipindi cha mpito kuelekea nishati salama kinafungua mlango wa mageuzi ya uzalishaji na kiteknolojia yanayoweza kulinganishwa na zama za mapinduzi ya viwanda.”
“Michango iliyodhamiriwa kitaifa (NDCs) ni ramani ya njia itakayoongoza kila nchi kupitia mabadiliko haya. Sio tu takwimu au asilimia. Ni fursa ya kutafakari upya mifumo, na sisi tupo katika sera na uwekezaji kuelekea dhana mpya ya kiuchumi,” amesisitiza.
Ili hili litokee duniani kote, Rais Lula amesema, “nchi tajiri zinahitaji kuwasilisha mapema malengo yao ya kutozalisha hewa chafuzi. Na hilo ni pamoja na kupanua upatikanaji wa rasilimali na teknolojia kwa nchi zinazoendelea. Kanuni ya wajibu wa pamoja lakini kwa viwango tofauti bado inaendelea kuwa halali.”
China kuongeza uzalishaji nishati kwa kutumia upepo na jua
Rais wa China, Xi Jinping, amehutubia kwa njia ya video akisema kuwa nchi yake itapunguza uzalishaji wa hewa chafuzi kwa kati ya asilimia 7 hadi 10 ifikapo mwaka 2035.
Pia ametaja kuwa China itapanua uwezo wa mitambo ya kuzalisha nishati kwa kutumia upepo na jua hadi zaidi ya mara sita ya viwango vya mwaka 2020, ikilenga kufikia jumla ya megawati 3,600,000.
Vilevile, magari ya nishati mbadala yatafanywa kuwa ya kawaida katika mauzo ya magari mapya, na soko la kitaifa la biashara ya hewa chafuzi litaongezwa kufikia sekta kuu zenye uzalishaji mkubwa wa hewa chafuzi.