Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa kudumu wa Afrika kwenye Baraza la Usalama la UN ni muhimu - Ruto

Rais William Ruto wa Kenya akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Loey Felipe
Rais William Ruto wa Kenya akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Ujumbe wa kudumu wa Afrika kwenye Baraza la Usalama la UN ni muhimu - Ruto

Amani na Usalama

Rais wa Kenya, William Ruto, amesema Umoja wa Mataifa hauwezi kuendelea kujiita Umoja wa Mataifa huku ukipuuza sauti za mataifa 54 ya Afrika, hasa kwenye ujumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama.

Ruto amesema hayo akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Jumatano ya Septemba 24.

Afrika haiwezi kusubiri maamuzi isiyoshiriki

“Afrika haiko tayari tena kusubiria pembeni wakati maamuzi kuhusu amani, usalama na maendeleo kuhusu bara hili  yanafanywa bila uelewa, mitazamo, na sauti zao,” amesema kiongozi huyo wa Kenya.

Amesisitiza kuwa kutengwa kwa Afrika hakukubaliki, si kwa haki, na kunakosa uadilifu na zaidi ya yote kunadhoofisha uaminifu wa chombo chenyewe.

Rais Ruto ametanabaisha kuwa Afrika inatawala ajenda nyingi za Baraza la Usalama, inatoa baadhi ya vikosi vikubwa zaidi katika shughuli za kulinda amani za UN, na inabeba gharama kubwa zaidi za ukosefu wa utulivu.

“Hata hivyo, inasalia kuwa bara pekee lisilo na kiti cha kudumu kwenye meza ambako maamuzi kuhusu hatma yake yanafanywa,” amesema Ruto akimaanisha ndani ya Baraza la Usalama lenye wajumbe 15, kati yao 5 ni wa kudumu, na hakuna hata mmoja kutoka Afrika.

Amesema kwamba dunia lazima uelewe kuwa kulifanyia marekebisho Baraza la Usalama sio upendeleo kwa Afrika; ni lazima kwa ajili ya uhai wa Umoja wa Mataifa.

UN iakisi mahitaji ya zama za sasa si zama za 1945

“Ili Umoja wa Mataifa ubakie na umuhimu katika karne hii, lazima iakisi hali halisi ya leo, na si mipangilio ya nguvu ya baada ya vita ya 1945,” amesisitiza.

Amesema kuwa katika Baraza la Usalama Afrika inastahili viti viwili vya kudumu, pamoja na haki kamili, ikiwemo kura ya turufu, na viti vingine viwili visivyo vya kudumu.

Licha ya udhaifu bado UN muhimu

Pamoja na udhaifu wake, Rais Ruto amekiri kuwa Umoja wa Mataifa unasalia kuwa fursa bora zaidi ya binadamu kwa mshikamano wa kimataifa, akisema hakuna taasisi nyingine yenye uhalali wa ulimwengu wote au uwezo wa kuleta watu pamoja kama chombo hicho.

Ametoa mfano wa jinsi UN imewezesha ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kuratibu misaada ya kibinadamu, kuhamasisha mwitikio wa kimataifa dhidi ya Covid-19, na kuendesha makubaliano juu ya mabadiliko ya tabianchi kupitia Mkataba wa Paris.

Rais Ruto amerejelea nukuu ya Dag Hammarskjöld, Katibu Mkuu wa pili wa UN, kwamba "Umoja wa Mataifa haukuumbwa ili kupeleka binadamu mbinguni, bali kuwaokoa kutoka kuzimu."

Amehimiza mataifa kupinga jaribio la kukata tamaa na Umoja wa Mataifa, na badala yake kuuimarisha ili utekeleze malengo yake, kurekebisha miundo yake, kuimarisha mamlaka yake, na kuhakikisha maamuzi yake yanaakisi hali halisi ya leo.

Hotuba ya Ruto pia imegusia mizozo Mashariki ya Kati, Afrika, Ulaya,halikadhalika mabadiliko ya tabianchi, mfumo wa kifedha duniani na haki za binadamu.

Soma hotuba nzima ya Ruto hapa.