Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ITU, Will.i.am, na Google wazindua mafunzo ya AI na roboti kwa vijana barani Afrika

ITU, Will.i.am, na Google wazindua mafunzo ya AI na roboti kwa vijana barani Afrika.
© ITU ITU, Will.i.am, na Google wazindua mafunzo ya AI na roboti kwa vijana barani Afrika.

ITU, Will.i.am, na Google wazindua mafunzo ya AI na roboti kwa vijana barani Afrika

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Muungano wa Mawasiliano ITU linalohusika na teknolojia za kidijitali, limeungana na mjasiriamali wa teknolojia na mwanamuziki  nyota will.i.am pamoja na kampuni ya Google ili kutoa mafunzo ya Akili mnemba AI na roboti kwa wanafunzi barani Afrika.

Mpango huu, ulio tangazwa leo wakati wa tukio la masuala ya kidijitali Digital@UNGA Anchor Event katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kandoni mwa Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGGA80 unalenga kutoa mafunzo ya vitendo kwa vijana katika jamii zisizo na rasilimali nyingi, hasa katika nchi ambapo mpango wa pamoja wa ITU na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF wa  Giga initiative unasaidia shule kuunganishwa na mtandao wa intaneti.

ITU inasema mpango mpya pia utafungua fursa za ujuzi wa kidijitali shuleni “Huu mpango utafungua milango mipya ya fursa za uelewa wa AI miongoni mwa vijana, na kuwawezesha kuongoza mabadiliko ya kidijitali yanayobadilisha jinsi tunavyoishi, kufanya kazi na kuwasiliana,” amesema Doreen Bogdan-Martin, Katibu Mkuu wa ITU.

Ameongeza kuwa “ITU inafanya kazi kuhakikisha vijana barani Afrika wanapata mafunzo na zana zinazohitajika kufanikisha maisha katika dunia inayotegemea AI.”

Kuwaunganisha waliobaki nyuma

Kwa mujibu wa ITU mpango huu unashughulikia changamoto mbili, kuunganisha idadi kubwa ya watu wasiopata intaneti na kujenga ujuzi wa kidijitali katika jamii ngumu kufikika, huku kipaumbele maalumu kikilenga wasichana na makundi yasiyojiweza.

Kwa sasa, bilioni 2.6 za watu hawako mtandaoni duniani, wakiwemo watoto bilioni 1.3 na barani Afrika, inaongoza kwa asilimia 60 ya vijana ambao hawako katika mtandao wa intaneti limesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Mara shule zikiwa zimeunganishwa kupitia mradi wa Giga initiative, wanafunzi wenye umri wa miaka 10 hadi 18 watapata mafunzo ya ITU kupitia muungano wa mafunzo ya AI na mpango wa Robotics for Good Youth Challenge, yote yakiwa sehemu ya mpango wa ITU wa AI for Good.

Mafunzo ya vitendo na msaada wa kitaalamu

Ikiwa imeungwa mkono na Balozi wa ITU wa AI Skills Coalition, will.i.am, mwanzilishi wa wakfu wa i.am Angel Foundation, mpango huu utawapatia shule nyenzo za vifaa vya roboti, mtaala wa AI unaolingana na eneo, na mafunzo kwa walimu.

“Kwenye uchumi wetu wa kidijitali, ni dharura kusaidia vijana katika maeneo yenye changamoto kufikia kasi ya AI, ili waweze kushiriki kikamilifu,” alisema will.i.am akiongeza kuwa “Kwa ujuzi wa masomo ya sayansi, hisabati na teknolojia STEM, roboti, na AI, akili zenye mvuto barani Afrika zitawekwa kwenye nafasi ya kufanikisha mafanikio na kutatua changamoto kubwa za dunia.”

Google yachangia kuendeleza ujuzi

Kampuni ya Google, kupitia tume yake ya hisani Google.org, inachangia utaalamu wa AI pamoja na dola milioni 1 za Marekani kuanzisha mpango huu.

“Ili kufaidika kikamilifu na fursa zinazotolewa na AI, lazima tufanye ujuzi huu upatikane kwa kila mtu, kila mahali,” amesema James Manyika, Makamu wa Rais wa Utafiti, Maabara, Teknolojia na Jamii katika kampuni ya Google.

Ameongeza kuwa “Tunachukulia mpango huu wa mafunzo ya AI na roboti kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa dhamira yetu barani Afrika, ambapo Google inafanya kazi ya kupanua muunganisho, kuongeza upatikanaji wa zana za AI, na kuendeleza ujuzi barani kote.”

Kuzindua programu barani Afrika

Mpango huu utaanza katika awamu ya kwanza kwenye nchi za Ghana, Ivory Coast, Kenya, Nigeria, na Afrika Kusini, ukijumuisha mitaala maalumu, mafunzo kwa walimu, kits za robotics, na maonyesho ya kitaifa. Utaunda msingi wa kuendeleza mafunzo ya ujuzi wa AI na roboti katika shule barani Afrika, na baadaye kupanuliwa kote duniani.