Ukraine: Taasisi za kimataifa zimekuwa dhaifu
Ukraine: Taasisi za kimataifa zimekuwa dhaifu
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema taasisi za kimataifa zimekuwa dhaifu wanachoweza kufanya ni kutoa matamko makali pekee na kwamba kwa sasa duniani sheria pekee za Kimataifa haziwezi kusaidia nchi kujilinda bila ya kuwa na silaha pamoja na marafiki wenye nguvu wa kukusaidia.
"Habari viongozi, marafiki na wote ambao mngependa kuwa marafiki sababu mnataka amani kama vile ambavyo sisi tunataka amani.." Hiyo ndio ilikuwa salamu ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akiwa mzungumzaji wa pili hili leo siku ya pili ya Mjadala mkuu wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.
Umoja wa Mataifa ukitimiza miaka 80 Rais wa Ukraine anasema mambo yamerudi kama ilivyokuwa zamani.
“Hivi sasa hakuna mtu isipokuwa sisi wenyewe tunaoweza kujihakikisha usalama, ni ushirikiano wenye nguvu, washirika wenye nguvu na silaha pekee. Karne ya 21 haina tofauti sana na ilivyokuwa zamani. Mataifa yanataka amani lakini bado yanapaswa kutumia silaha. Ina kera lakini hiyo ndiyo hali halisi. Sio sheria za kimataifa, wala mashirikiano, ni silaha ndio huamua nani atakayesalimika.”
Pamoja na kuwa duniani kuna taasisi zinazosimamia haki na sheria za kimataifa lakini Rais huyu wa Ukraine nchi ambayo ipo kwenye vita na taifa la Urusi kwa zaidi ya miaka 11 sasa huku hali ikiwa mbaya zaidi tangu mwezi Februari mwaka 2022 amewaambia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wakimsikiliza wakati akitoa hotuba yake kwamba ...
“ Mnajua vyema kabisa kwamba sheria za Kimataifa hazifanyi kazi kikamilifu isipokuwa tu pale ambapo una marafiki wenye nguvu ambao wako tayari kuzisimamia na hata hilo lilkifanyika bado hazitaweza kufanya kazi bila kutumia silaha,... ni mbaya, .. lakini bila hivyo mambo yangekuwa mabaya zaidi, hakuna dhamana ya usalama isipokuwa marafiki na silaha, hakuna mUkriani aliyechagua aina hii ya ukweli, na ninavyowajua watu wetu wangechagua kipaumbele tofauti , waukraine ni watu wa amani.”
Akitumia zaidi ya dakika 20 Zelenskyy alizungumzia mambo mengine yahusuyo amani na usalama yanayoendelea duniani na kueleza namna nchi yake inavyotumia fedha nyingi katika vita badala ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Amehimiza hatua zichukuliwe kwani sasa maendeleo ya teknoljia yanafanya mambo kuwa magumu zaidi akitolea mfano teknolojia ya Akili Mnemba AI katika matumizi ya ndege zisizo na rubani drone na kwamba sasa zinatumika katika vita na zinaleta maafa makubwa.