Guterres awasihi viongozi kufanikisha ufadhili kwa ajili ya mustakabali imara, jumuishi na endelevu
Guterres awasihi viongozi kufanikisha ufadhili kwa ajili ya mustakabali imara, jumuishi na endelevu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amefungua Mkutano wa kwanza wa kila miaka miwili wa Uchumi Endelevu, Jumuishi na Imara kwa wito wa kuchukua hatua thabiti ili kurekebisha mifumo ya kifedha ya kimataifa na kuziba pengo la maendeleo linaloongezeka.
Akihutubia hii leo viongozi wa dunia, wakuu wa taasisi za kifedha za kimataifa na wawakilishi wa majukwaa ya kimataifa kama vile G7, G20 na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP30, katika kikao cha ngazi ya juu kando ya mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80 Guterres amesisitiza umuhimu wa kihistoria wa mkutano huo.
“Mkutano huu wa Kila Miaka Miwili si kikao kingine tu. Huu ni wa kwanza wa aina yake. Huu ni ushirikiano wa kweli wa kimataifa kwa vitendo,” amesema.
Katibu Mkuu amebainisha kwamba mkutano huu umetokana na hofu ya kuongezeka kwa mzigo wa madeni, mazungumzo ya kifedha yaliyogawanyika, na kutengwa kwa nchi zinazoendelea kwenye maamuzi muhimu.
Amesema “Tunashuhudia pengo la ufadhili likipanuka na changamoto ya madeni ikienea huku nchi zinazoendelea zikikosa kushirikishwa kwenye maamuzi hata ya yale yanayowahusu moja kwa moja.”
Pengo la ufadhili na mageuzi ya mfumo wa kifedha
Guterres amesisitiza umuhimu wa kuhamasisha rasilimali zaidi ili kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Sote tunakubaliana kuwa fedha zaidi zinahitajika kuhamasishwa na kwamba usanifu wa sasa wa kifedha wa kimataifa unahitaji mageuzi ili kuendana na changamoto za dunia ya sasa.”
Ametaja maeneo ambayo tayari kuna makubaliano ambayo ni “kuongeza mara tatu uwezo wa mikopo wa benki za maendeleo ya kimataifa, kutumia vyema fedha binafsi, kuboresha mbinu za msaada wa madeni, na kuendeleza ushirikiano wa ushuru wa kimataifa jumuishi”.
Nguzo Tatu: Ushirikiano, usawa, ujumuishi
Katibu Mkuu ameeleza nguzo tatu zinazouongoza mkutano huu:
- Ushirikiano: “hasa kwa kuzingatia kushuka kwa ahadi za misaada na kuongezeka kwa misuguano ya kibiashara.”
- Usawa: kujenga madaraja kati ya mazungumzo ya kifedha ya maendeleo ambayo yamegawanyika.
- Ujumuishi: kuhakikisha nchi zinazoendelea “zinakuwa na kauli na ushawishi mkubwa zaidi katika maamuzi yanayowahusu.”
“Mgao wa nguvu za kiuchumi duniani ni usio na usawa kwa kiwango kikubwa, na haupaswi kuwa msingi wa kuamua ushiriki,” amesisitiza.
Kutoka kwa ahadi hadi hatua
Akitambua hatua zilizochukuliwa, Guterres ameonya dhidi ya kuridhika.
Amesema “Hatua zimechukuliwa, lakini sasa lazima tuende mbali zaidi. Mikutano si lengo bali ni njia ya kufanikisha matakwa ya watu wanaosubiri vitendo sasa.”
Aliwataka viongozi kutumia fursa hii ya kisiasa kubadilisha ahadi kuwa hatua halisi kwa uchumi wa kimataifa ulio wa haki na imara.
Amesisitiza “Tuitumie Mkutano huu kuimarisha ushirikiano wetu na kuchukua hatua thabiti kuelekea mustakabali ulio imara, jumuishi na endelevu.”