Hakuna uhusiano wa usonji na matumizi Acetaminophen/Paracetamol- WHO
Hakuna uhusiano wa usonji na matumizi Acetaminophen/Paracetamol- WHO
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) leo Jumatano tarehe 24 mwezi Septemba 2025, limesema hakuna uhusiano wowote kati ya ugonjwa wa usonji miongoni mwa watoto na matumizi ya dawa aina ya kupunguza maumivu aina ya Acetaminophen ijulikanayo pia kama Paracetamol wakati mama akiwa mjamzito.
Usonji ni hali inayompata mtoto au utofauti au changamoto katika mfumo wake wa ufahamu na ubongo na kusababisha changamoto za kimawasiliano, tabia na kudhibiti hisia mwili.
Zingatia sayansi na si uvumi
Taarifa ya WHO iliyotolewa leo Geneva, Uswisi imesema hadi sasa hakuna ushahidi wa kisayansi kuhusu hilo,na taarifa za kisayansi ndiyo zinapaswa kuaminiwa na si uvumi.
Kulingana na takwimu za WHO, takribani idadi ya watu milioni 62 duniani kote (yaan mtu 1 kati ya watu 127) wana ugonjwa wa usonji.
WHO inasema ingawa uelewa wa hali hii umekuwa ukiongezeka na uchunguzi ukiboreshwa katika miaka ya hivi karibuni, sababu zake bado hazijathibitishwa kikamilifu, na inafahamika kuwa kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia.
Paracetamol na chanjo za watoto zathibitishwa kutokuwa na uhusiano na usonji
Utafiti wa kina umefanyika katika muongo mmoja uliopita, ukichunguza kwa undani uhusiano kati ya matumizi ya dawa ya paracetamol wakati wa ujauzito na usonji. WHO imebainisha kuwa hadi sasa, hakuna uhusiano wowote wa moja kwa moja uliowahi kuthibitishwa kupitia tafiti hizi za kisayansi.
Hata hivyo,WHO imeshauri wanawake wote kuendelea kufuata ushauri wa madaktari au watoa huduma za afya, ambao wanaweza kusaidia kutathmini hali za mtu binafsi na kupendekeza dawa zinazofaa.
“ Dawa yoyote inapaswa kutumiwa kwa tahadhari wakati wa ujauzito, hasa katika miezi mitatu ya mwanzo, na kufuata mwongozo wa wa wataalamu wa afya,” imesema WHO.
Ushahidi unathibitisha chanjo hazisababishi usonji
Kadhalika, shirika hilo limesema kuna ushahidi wa kutosha na wa kina unaothibitisha kuwa chanjo za watoto hazisababishi usonji. Tafiti kubwa na zenye ubora wa hali ya juu kutoka nchi mbalimbali zimefikia hitimisho moja.
WHO imefafanua kuwa tafiti za awali zilizopendekeza uhusiano huo zilikuwa na dosari na zimebatilishwa. Tangu mwaka 1999, wataalamu huru wanaoshauri WHO wamethibitisha mara kwa mara kwamba chanjo—ikiwemo zile zenye kemikali za thiomersal au alumini—hazisababishi usonji au matatizo mengine ya ukuaji.
Umuhimu wa ratiba ya chanjo
Ratiba za chanjo za watoto hutengenezwa kwa umakini mkubwa na wataalamu wa kimataifa na hutumiwa maoni kutoka kila nchi duniani kote. Katika miaka 50 iliyopita, ratiba hizi zimeokoa maisha ya watu takriban milioni 154, na zimeendelea kuboreshwa ili kulinda watoto na watu wazima dhidi ya magonjwa 30 ya kuambukiza.
Kila pendekezo la chanjo kutoka Kikundi cha Ushauri wa Kimkakati cha Wataalamu wa Chanjo (SAGE), kikundi huru cha ushauri kwa WHO, linatokana na ukaguzi wa kina wa ushahidi na limeundwa kwa makini ili kutoa kinga bora dhidi ya magonjwa hatari na kuhakikisha zinatolewa wakati unaohitajika zaidi.
Hatari za kuvuruga au kuchelewesha ratiba ya chanjo
WHO imeonya kuwa kuvuruga au kuchelewesha ratiba ya chanjo huongeza hatari ya maambukizi kwa mtoto husika na kwa jamii nzima. Watoto wachanga ambao ni wadogo sana kupokea chanjo na watu walio na kinga dhaifu ndio walio katika hatari kubwa zaidi.
Viongozi w anchi kujadili usonji wakati wa mkutano wa NCDs kando ya UNGA80
Kesho Alhamisi Septemba 25, kando ya Mjadala Mkuu wa UNGA80, viongozi watajadili usonji na matatizo ya ukuaji wa mishipa ya fahamu, ikiwa ni kwenye mkutano wa 4 wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Magonjwa Yasiyoambukiza na Afya ya Akili.
WHO imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua zaidi ili kuelewa sababu za usonji na kutoa msaada bora kwa mahitaji ya watu wenye usonji na familia zao.
Shirika hilo limethibitisha kujitolea kwake kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo mashirika yanayoongozwa na watu wenye usonji, mashirika mengine yanayowakilisha watu wenye uzoefu wa moja kwa moja wa hali hiyo na ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia ushahidi na bila unyanyapaa.