Tambueni kinachoendelea Mashariki mwa DRC kuwa ni mauaji ya halaiki - Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo, amehutubia mkutano wa 80 wa Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA80) jijini New York, Marekani na kusema kwamba vita dhidi ya ukosefu wa haki, ubaguzi na ufisadi ni muhimu ili kuzuia migogoro, akikumbusha kuwa makubaliano ya amani hayawezi kuwa ya mafanikio bila hakikisho la haki na usaidizi kwa manusura.
"Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DCR) haitaki huruma wala upendeleo. Tunahitaji haki, ukweli, na heshima ya hadhi," amesema Tshisekedi, akiendelea kusema kuwa nchi yake itaendelea kupigania haki kwa dhuluma zinazoendelea kutokea, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kigaidi na mauaji ya kimbari yaliyotokea katika maeneo mbalimbali mashariki mwa nchi.
Amesisitiza kuwa historia itawahukumu viongozi kwa matendo yao ya uhalifu na siyo kwa maneno yao, na kwamba dunia inahitaji kusimama kwa imani katika haki ili kuweka mwisho kwa mzunguko wa machafuko unaoendelea katika eneo la Maziwa Makuu.
Tunataka Tume Huru ya Kimataifa ichunguze mauaji DRC
Katika hotuba yake amesisitiza pia umuhimu wa kutambuliwa kwa mauaji ya halaiki DRC akitaka jamii ya kimataifa kutambua maumivu na majanga yanayokumba nchi yake kwa miongo kadhaa.
“DRC ni nchi yenye maisha, rasilimali asili, na ustahimilivu wa binadamu. Tunataka kuchangia amani. Hata hivyo amani inaanza na kutambuliwa kwa maafa yaliyotokea kwenye taifa letu,” amesema Tshisekedi.
Hivyo akasema, “tunaomba kwa dhati mbele ya mkutano huu: Tambuaeni mauaji ya halaiki DRC, tuunge mkono mapambano yetu kwa haki na ukweli, na tusaidieni kujenga amani endelevu katika moyo wa Afrika.”
Amesisitiza kwamba bila kutambuliwa kwa maafa hayo, amani halisi haiwezi kupatikana, na kwamba utulivu wa kanda unahitaji ushirikiano wa kimataifa kwa msingi wa haki.
Hivyo ametaka Umoja wa Mataifa kuunda Tume huru ya uchunguzi ya kimataifa, ili kusaka ukweli, kutoa haki kwa manusura, na kuondoa mzunguko wa ukosefu wa uwajibikaji ambao umedumaza juhudi za amani na maendeleo kwa miongo kadhaa.
Mikataba ya amani: Washington DC, Doha, Nairobi, Luanda
Rais huyo wa DRC pia amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa kati ya nchi yake na Rwanda.
Katika hotuba yake, Tshisekedi ametoa shukrani zake kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa uongozi wake ambao ulisababisha mazungumzo ya amani na kusainiwa kwa Makubaliano ya Amani ya Washington mnamo Juni 27, 2025.
Makubaliano hayo yamelenga kumaliza mgogoro kati ya Rwanda na DRC, kwa kuhakikisha uondokaji kamili na wa kuthibitishwa wa vikosi vinavyodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kutoka katika maeneo ya DRC.
Rais Tshisekedi amefafanua kuwa makubaliano hayo pia yanahusisha kuondoa silaha na kuunganisha makundi ya silaha yasiyo ya kiserikali katika Jeshi la Wananchi la DRC (FARDC) na Polisi ya Kitaifa ya Congo, pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa ushirikiano wa pamoja katika masuala ya usalama.
Utekelezaji wa mkataba utaleta amani ya kweli
Ameweka wazi kuwa uondokaji wa vikosi vya Rwanda, kumalizika kwa msaada wao kwa kundi la waasi wa M23, na kurudi kwa mamlaka ya serikali ya DRC katika maeneo yote yaliyoshikiliwa ni masharti muhimu ambayo hayawezi kujadiliwa ili kufanikisha amani ya kweli.
Tshisekedi ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa makubaliano haya yanafikiwa na kutekelezwa kikamilifu, akiongeza kuwa uadhibu wa wale wanaohusika na uhalifu lazima uendelee ili kumaliza mzunguko wa vurugu.
Aidha, Rais wa DRC amekumbusha juhudi nyingine za kidiplomasia katika kutafuta amani, akitaja sahihi ya Makubaliano ya Doha mnamo Julai 19, 2025, kati ya DRC na M23, ambapo pande zote zilieleza nia ya kuendeleza majadiliano ya amani. Ametoa shukrani zake kwa Kiongozi Mkuu wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, kwa mchango wake mkubwa katika mchakato wa amani.