Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angola: UN lazima ifanye mageuzi kwani dunia ina chaguzi mbili, kati ya amani na vita

Rais  João Manuel Gonçalves Lourenço wa Angola akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la UN mkutano wa 80.
UN Webcast
Rais João Manuel Gonçalves Lourenço wa Angola akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la UN mkutano wa 80.

Angola: UN lazima ifanye mageuzi kwani dunia ina chaguzi mbili, kati ya amani na vita

Amani na Usalama

Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika João Manuel Gonçalves Lourenço ametumia hotuba yake katika Kikao cha 80 cha Mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutoa onyo kali, “dunia imesimama mbele ya uchaguzi wa kufanya kila kitu ili kulinda amani au kukabiliana na vita na madhara yake yote, hivyo kuhatarisha mustakabali wa ubinadamu.”

Akihutubia mjadala huo chini ya kaulimbiu “Pamoja tuko Bora Zaidi: Miaka 80 na Zaidi kwa Amani, Maendeleo na Haki za Binadamu”, aliwataka viongozi wa dunia kukabiliana na ongezeko la misukosuko kwa kujitolea upya kwa mshikamano wa pande nyingi.

Wito wa mshikamano na mazungumzo

Kiongozi huyo wa Angola Lourenço amesifu urithi wa Umoja wa Mataifa katika kudumisha amani lakini akaonya kuwa mgawanyiko kati ya mataifa makuu unahatarisha miongo kadhaa ya maendeleo. “Ukinzani mkubwa unaoelezea mahusiano ya kimataifa kwa sasa unatufanya kuwa karibu zaidi na mlipuko wa kimataifa kuliko wakati wowote wa vita baridi,” amesema. Amesisitiza kuwa ni mazungumzo na hatua za pamoja pekee zinazoweza kuziba pengo, akiongeza kuwa “Hekima lazima ishinde tena juu ya misukumo mibaya ya mapambano ya kiwango kikubwa.”

Afrika: Amani na maendeleo haviwezi kutenganishwa

Akiangazia udhaifu wa Afrika, Rais huyo amewakumbusha wajumbe juu ya mapambano ya bara hilo katika chakula, maji, elimu, na usalama. “Sisi Waafrika, kutoka nchi zilizotawaliwa kwa karne nyingi, tunaelewa vyema kuliko mtu yeyote umuhimu wa amani,” amesema.
Ametaja jukumu la Angola katika kusuluhisha migogoro Sahel, Sudan, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, lakini akaonya kuwa udhaifu wa Umoja wa Mataifa mbele ya uvamizi na kuingiliwa kwa masuala ya ndani umechochea ukosefu wa utulivu.

Palestina, Cuba, na Vikwazo: Wito dhidi ya sura mbili

Katika sehemu yenye nguvu zaidi ya hotuba yake, Rais Lourenço amelaani hatua za kijeshi za Israel huko Gaza na kuondolewa kwa ujumbe wa Palestina katika Mkutano huo. “Watu wa Palestina hawawezi kulinganishwa na Hamas, kwa kuwa hakuna watu magaidi,’ sembuse watoto magaidi, amesema. Pia ametaka kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba na akapinga vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Zimbabwe na Venezuela, akivieleza kama vitendo vinavyo zidisha mateso ya wananchi wao.

Mageuzi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mustakbali

Akimulika mustakbali, Rais wa Angola ametaka mageuzi ya haraka kurejesha mamlaka ya Umoja wa Mataifa, kuanzia na kuongeza uwakilishi wa Afrika katika Baraza la Usalama. “Bila hatua hii muhimu, hatuwezi kuhakikisha utekelezaji wa Mkataba waZama Zijazo,” amesema.
Ameunganisha wito huo na mageuzi makubwa katika taasisi za kifedha za kimataifa na ahadi za mabadiliko ya tabianchi, akisisitiza kwamba haki inahitaji mataifa yaliyoendelea kiviwanda kugharamia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zilizo hatarini.
Amehitimisha kwa kusema“Umoja wa Mataifa ndilo shirika pekee lenye uhalali wa kuchukua hatua kwa niaba ya sisi sote, lazima tulilinde kwa gharama yoyyote”.