Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika Kusini: Umefika wakati wa UN kuongozwa na mwanamke

Rais Cyril Matamela Ramaphosa wa Afrika Kusini akihutubia Mjadala Mkuu wa kikao cha themanini cha Baraza Kuu. la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Loey Felipe
Rais Cyril Matamela Ramaphosa wa Afrika Kusini akihutubia Mjadala Mkuu wa kikao cha themanini cha Baraza Kuu. la Umoja wa Mataifa

Afrika Kusini: Umefika wakati wa UN kuongozwa na mwanamke

Masuala ya UM

Afrika Kusini imesema umefika wakati wa Umoja wa Mataifa kuongozwa na mwanamke na kwamba nchi hiyo inaunga mkono uchaguzi wa kiongozi mwanamke kushika wadhifa wa juu zaidi wa taasisi hiyo kubwa zaidi duniani

Hayo yamesemwa na Rais wa Afrika Kusini Cyril Matamela Ramaphosa wakati akihutubia katika siku ya kwanza ya kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani. 

Kwa dakika takriban 25 Rais Ramaphosa ameeleza masuala mbalimbali ambayo nchi yake inaunga mkono na yale inayopendekeza kufanyiwa mabadiliko na kuboreshwa

UN kuongozwa na mwanamke

Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake na ikiwa mwaka huu dunia inaadhimisha miaka 30 tangu kufanyika kwa mkutano mkubwa wa wanawake wa Beijing  Rais Cyril Ramaphosa amesema Afrika Kusini inathibitisha dhamira yake isiyoyumba katika kuwawezesha wanawake na ushiriki wao kamili wa usawa na wa maana katika nyanja zote za maisha. “Ndiyo, na tunaunga mkono uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwanamke .”

Akizungumzia zaidi hilo ameeleza kuwa mkutano wa Beijing “umetukumbusha wajibu wetu wa pamoja wa kuendeleza haki za binadamu, utu na haki kwa wote. Sisi sote ni sawa, wanaume kwa wanawake na hakuna sababu kwamba tunaendelea kuwaweka wanawake wa ulimwengu nyuma.”

“Ndiyo, na tunaunga mkono uchaguzi wa Katibu Mkuu  wa Umoja wa Mataifa mwanamke.”

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945 Umoja wa Mataifa umekuwa ukiongozwa na Makatibu Wakuu wanaume pekee na Rais huyo wa Afrika Kusini amesema muda sasa umefika wa taasisi hiyo kubwa zaidi duniani kuongozwa na mwanamke

Matumizi makubwa ya fedha kwenye silaha

Akizungumzia tarifa iliyotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuhusu matumizi makubwa ya fedha kwenye silaha wakati ambao masuala ya msingi yakikosa ufadhili.

Rais huyo wa Afrika kusini amesema “Tunatengeneza silaha wakati tunapaswa kutengeneza miundombinu ya kijamii ambayo itaendeleza maisha ya watu wetu. Tunapigana vita vinavyosababisha vifo na uharibifu wakati tunapaswa kupigana na umaskini na kuendeleza maisha ya watu wanaoishi katika mazingira magumu. Lazima tuchukue hatua madhubuti kunyamazisha bunduki zote kila mahali ili kufikia lengo la maendeleo endelevu na amani ya kimataifa na ninaamini kuwa hili ni lengo ambalo linawezekana kufikiwa.”

Baraza la Usalama

Kuhusu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akasema “Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limethibitisha kushindwa kufanya kazi katika muundo wake wa sasa katika kutekeleza majukumu yake ya kimkataba yanayolitaka kudumisha amani na usalama wa kimataifa.”

Amesem Afrika Kusini inasalia kuwa na wasiwasi mkubwa wa mmomonyoko wa uaminifu wa Baraza hilo la usalama kwa kushindwa kwake kuhakikisha kuna uwajibikaji na kuzingatiwa kwa sheria za kimataifa huku hali ya usalama na changamoto za kibinadamu zikiongezeka katika lika pembe ya dunia ikiwemo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sudan, Gaza na kwingineko.

“ Ni jambo la kutia wasiwasi sana kwamba kuna nchi zinazoendelea kudharau sheria za Kimataifa na pia kukaidi maazimio ya Umoja wa Mataifa kutoka kwenye Mahakama ya Kimataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Haki -ICJ.”

Masuala mengine aliyozungumzia ni pamoja na kesi nchi yake iliyowasilisha mahakamani kuhusu Israel na Palestina, kutaka suluhusu ya uwepo wa mataifa mawili kwenye mzozo baina ya Israel na Palestina na kuheshimiwa na kupewa uzito unaostahili taasisi ya Umoja wa Mataifa.

G20 Afrika

Kwa mara ya kwanza mwaka huu kundi la nchi tajiri zaidi duniani G20 linatarajia kufanya mkutano wake katika ardhi ya Afrika ambapo mkutano huo utafanyika nchini Afrika Kusini.

Rais Rhamaposa amesema katika urais wao wa G20 mwaka huu wanaongozwa na kuhamasisha usawa, mshikamano na uendelevu.

“Tumezialika nchi za G20 katika kutoa kipaumbele kwenye mazungumzo yahusuyo kujiandaa na kukabiliana na majanga yasababishwayo na mabadiliko ya tabianchi, kuhakikisha wanakabiliana na madeni himilivu, pili kuzisaidia nchi kuwa na madeni ambayo hayatawafanya kushindwa kufanya mambo mengine ya kiuchumi kwa ajili ya maendeleo, tatu kujadiliana jinsi ya kutafuta fedha kwa ajili ya nishati jadidifu na mbadala na nne ni kutumia madili waliyonayo kuyaongeza thamani katika maeneo yanapochimbwa ili kuchangia maendeo ya jamii za maeneo hayo” 

Sikiliza hotuba yake yote hapa