Jumuiya ya kimataifa kuweka misingi ya utawala wa AI
Jumuiya ya kimataifa kuweka misingi ya utawala wa AI
Ukuaji wa kasi wa zana zinazotumia Akili Mnemba au AI ulimwenguni kote bado haulingani na sheria bora, zilizokubaliwa kimataifa kuhusu jinsi teknolojia hii yenye nguvu inadhibitiwa. Lakini hilo linaenda kupatia muarobani katika mkutano wa ngazi ya juu katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa tarehe 25 Septemba 2025 siku ya Alhamisi ambao umepangwa kwenda kujadili kwa pamoja na kuleta utawala bora wa kimataifa wa AI.
Uwekezaji, matumaini na wasiwasi: haya ni maeneo matatu au yanaweza kuelezwa kuwa vichochezi vikubwa katika Akili Mnemba pamoja na athari zake.
Kwa sababu changamoto na fursa ni za kimataifa, majibu pia yanahitajika kuwa ya kina zaidi kuliko suluhu zilizogawanyika na zilizo kimya ambazo zimepitishwa mpaka hadi sasa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2024 iligundulika kuwa nchi 118 hazikuwa sehemu ya mipango yoyote muhimu ya "kimataifa" ya utawala wa AI iliyoundwa katika miaka ya hivi karibuni, na kwamba ni mataifa saba tu, yote kutoka kwa nchi zilizoendelea ndio zilikuwa zinatekeleza mipango hiyo.
Mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu kuhusu utawala wa AI, utakaofanyika tarehe 25 Septemba, unaadhimisha kwa mara ya kwanza nchi zote 193 Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwa na kauli kuhusu namna utawala wa kimataifa wa AI unavyoendelezwa.
Tukio hili linataka kushughulikia ukosefu wa uwakilishi pamoja na diplomasia kutoka duniani kote, mkutano unawaleta pamoja wanasayansi, wanachama wa jumuiya ya teknolojia, sekta binafsi na mashirika ya kiraia.
Kujenga vizuizi kwa njia mpya ya kusimamia maendeleo ya teknolojia kwa usalama
Mkutano huo utaangazia vyombo viwili vipya vya kihistoria “Mazungumzo ya Kimataifa kuhusu Utawala wa AI na Jopo Huru la Kimataifa la Kisayansi kuhusu AI” vyote vinalenga kuanzisha mfumo wa utawala wa kimataifa jumuishi zaidi, kushughulikia masuala yanayozunguka teknolojia hii yenye nguvu, na kuhakikisha kuwa inawanufaisha watu wote
Vyombo hivi viwili vilitokana na mapendekezo yaliyotolewa na kundi la wataalam na watunga sheria (Bodi ya Ushauri ya Ngazi ya Juu ya Ujasusi Bandia) katika ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ya 2024, iliasisiwa kupitia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Agosti 2025, lililoidhinishwa kwa kauli moja na Nchi Wanachama wote na kusifiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kama “hatua muhimu katika juhudi za kimataifa za kutumia faida za akili mnemba wakati wa kushughulikia hatari zake.”
Lengo la majadiliano haya ni kushirikishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa utawala wa AI na kushirikishana matukio muhimu ya AI. Mazungumzo hayo, ambayo yanatarajiwa kuwa eneo kuu la ulimwengu la kuzingatia AI, litatengeneza nafasi ya pamoja kwa serikali, tasnia, mashirika ya kiraia na wanasayansi kubadilishana mazoea bora na kukuza maelewano, kwa kuzingatia kanuni za pamoja,
Jopo la Kimataifa, kwa msaada kutoka kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa, litatoa mwongozo usio na upendeleo, unaotegemea ushahidi juu ya hatari, fursa, na athari za AI, na itasaidia kuhakikisha kuwa utungaji sera unazingatia tathmini huru za kisayansi.
Jopo hilo litatoa ripoti ya mwaka, itakayowasilishwa katika mkutano wa kila mwaka wa Mazungumzo.
Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa Amandeep Singh Gil, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Teknolojia ya Kidijiti na Inayoibuka amesema “Vyombo hivi viwili vya kimataifa sio tu kazi mpya bali wanajenga vizuizi vya usanifu mpya wa utawala wa teknolojia. Ni ahadi yetu kwa vizazi vijavyo kuhakikisha kwamba ubinadamu unasalia katikati ya maendeleo ya teknolojia.”
Gil amesisitiza hatua ya msingi inayowakilishwa na mkutano wa tarehe 25 Septemba “Athari za AI ni za kimataifa, lakini utawala wake sio. Kupitia Mazungumzo ya Kimataifa, kwa mara ya kwanza, nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa zitaketi pamoja katika kuunda ushirikiano wa kimataifa juu ya utawala wa AI.”
Ameeleza kuwa “Jopo la Kisayansi litawaleta pamoja wanasayansi wakuu kutoka duniani kote ili kupunguza hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu hatari, fursa na athari za AI. Jopo hilo litasaidia kuhakikisha kwamba sera za AI zina msingi katika ushahidi bila ya kuwa na upendeleo.”
Wazungumzaji katika mkutano huo wa ngazi ya juu
Wazungumzaji wa mkutano huo ni pamoja na Annalena Baerbock, Rais 80 wa Baraza Kuu (UNPGA), Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Pedro Sánchez Pérez-Castejón, Waziri Mkuu wa Uhispania na Arnoldo André Tinoco, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Costa Rica.
Hotuba zao zitafuatiwa na kauli za Nchi Wanachama na Waangalizi wa Umoja wa Mataifa, pamoja na vyombo vya mfumo wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine, huku kauli za wahusika zisizo za kiserikali zitakuwa zinatolewa mara kwa mara kati ya zile za Nchi Wanachama.