UN yajipanga kuhakikisha Dunia inapata habari bila mkwamo
UN yajipanga kuhakikisha Dunia inapata habari bila mkwamo
Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukianza rasmi hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani zaidi ya watu 40,000 wanatarajiwa kuunganishwa kwenye mtandao wa intaneti (Wi-Fi) kusikiliza kile kitakachoelezwa na viongozi wa ngazi za juu, pamoja na wakuu wa nchi na serikali.
Mjadala huo pia unafuatiliwa na kurushwa hewani na mamia ya waandishi wa habari na wananchi wengine kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Akihojiwa na Idhaa ya Kireno ya Umoja wa Mataifa, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia habari na teknolojia, Bernardo Mariano, amesema maandalizi hufanywa kwa miezi kadhaa ili kuhakikisha hotuba za viongozi zinapeperushwa bila hitilafu za kiufundi wala kuvurugwa na mashambulizi ya mtandaoni.
Mariano amesema “Kipindi hiki dunia nzima inatazama hotuba na mijadala kutoka Baraza Kuu. Huu ni muda ambao maudhui ya Umoja wa Mataifa yanatumiwa zaidi duniani kote.”
Ameeleza kuwa miaka michache iliyopita ukurasa wa mtandao wa UN uliwahi kushindwa kuhimili idadi kubwa ya wageni, hali iliyosababisha maboresho makubwa yaliyoongeza uwezo wake kwa mara 100.
Kukabili mashambulizi ya mtandaoni
Kwa mujibu wa Mariano, hatua za kuimarisha ulinzi wa kimtandao huanza mapema mwezi Agosti na kuendelea hadi mwezi Septemba.
“Tunafuatilia kila aina ya mashambulizi ili yasilete madhara. Tayari tunakabiliana na baadhi yake, lakini tumetengeneza mifumo ya kuhakikisha haivurugi matangazo yanayorushwa mubashara,” amesema.
Wingi wa watumiaji wa Wi-Fi
Changamoto nyingine kubwa ni kuhakikisha mtandao unawatosheleza washiriki walio katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
“Kwa kawaida tunahudumia wafanyakazi 10,000, lakini wiki hii tunafikia watu 40,000. Na tofauti na miaka iliyopita, sasa kila mtu anatumia video. Ndiyo maana tumeboreshwa uwezo wa Wi-Fi katika miaka miwili iliyopita,” amesema
Uzinduzi wa mjadala wa kimataifa kuhusu AI
Mwaka huu pia hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa pembeni ya mijadala inayofanyika kwenye Baraza kuu pia kutafanyika mjadala wa ngazi ya juu kuhusu Akili Mnemba AI, jukwaa jipya litakalowaleta pamoja serikali na wadau kujadili ushirikiano wa kimataifa na mbinu bora za kudhibiti matumizi ya akili mnemba.
“Ni muhimu nchi zote, maskini kwa tajiri, zikubaliane kwamba akili mnemba ni suala la sasa, si la baadaye. Tunapaswa kuongeza manufaa yake na kupunguza madhara, hasa katika eneo la upotoshaji wa taarifa wakati wa chaguzi,” amesisitiza Mariano.
Amehitimisha mahojiano yake aliyofanyiwa na Felipe de Carvalho kwa kusema kuwa timu yake na nyingine nyingi za Umoja wa Mataifa zimejizatiti kuhakikisha picha na sauti bora zinapatikana ili dunia ifuatilie kikamilifu hotuba na maamuzi ya Baraza Kuu na kazi za Umoja wa Mataifa kwa ujumla.
Wiki ya viongozi imeanza rasmi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ikikusanya macho na masikio ya dunia nzima katika mijadala na maamuzi yanayoweza kuathiri mustakabali wa wote. Bofya hapa kufuatilia yale yote yanayoendelea katika Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mikutano mingine ya ngazi za juu.