Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huu ni wakati wa hatua na si wa sherehe kurejesha hadhi ya UN: Baerbock

General Assembly President Annalena Baerbock addresses the opening of the general debate of the UN General Assembly's 80h session.
UN Photo
General Assembly President Annalena Baerbock addresses the opening of the general debate of the UN General Assembly's 80h session.

Huu ni wakati wa hatua na si wa sherehe kurejesha hadhi ya UN: Baerbock

Amani na Usalama

Akikumbuka miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock leo amefungua Majadiliano  Mkuu wa Batraza Kuu UNGA80 kwa kuwakumbusha nchi wanachama kwamba wakati huu “sio mwaka wa kawaida na sio wakati wa sherehe, bali ni kwa kutafakari juu ya kushindwa kwa taasisi na umuhimu wake endelevu.”

Bi. Baerbock amesema “Maelfu ya yatima Gaza wamekwama kwenye mabaki ya majengo wakila mchanga, wakilazimika kunywa maji machafu . Wanawake wa miaka tisini nchini Ukraine wanajificha kutokana na mashambulizi ya Ndege zisizo na rubani. Watoto nchini Haiti wanaogopa hata kutembea Kwenda shule.”

.Ameongeza kuwa “Tukiangalia hali hizi, sasa sio wakati wa kusherehekea lakini ni wa kujiuliza Umoja wa Mataifa uko wapi?”

Sio katiba inayoshindwa ni wanachama

Akiwajibu wakosoaji wanaouliza kama Umoja wa Mataifa haifai tena, Rais juyo wa Baraza Kuu amekanusha kwa uthabiti wazo kwamba taasisi yenyewe haifai. “Magari ya kivita yaliingia Ukraine kwa sababu Ibara ya 2 halieleweki vya kutosha kuhusu uhuru wa taifa? Wakati raia wanauawa Gaza, sheria za kibinadamu zinashindwa kulinda raia?” amehoji.

“Sio Katiba inashindwa,” amesema, akisisitiza kwamba Umoja wa Mataifa ni imara tu kadri nchi wanachama wanavyotaka kuenzi kanuni zake na kuwawajibisha wanaokiuka sheria.

Athari ya UN duniani haiwezi kupuuzia

Licha ya kushindwa, Rais Baerbock amesisitiza umuhimu usiopingika wa mashirika ya Umoja wa Mataifa katika kuokoa maisha na kukuza heshima ya binadamu. “Bila Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF, watoto milioni 26 wangekosa elimu. Bila Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, watu karibu milioni 125 wangekosa msaada wa chakula unaookoa maisha. Bila Shirika la Afya Duniani WHO, chanjo zaidi ya bilioni moja zingekuwa  hazijapokewa,” ameongeza.

Ameendelea kusema kwamba “Ndiyo, tuna kushindwa. Lakini fikiria jinsi ambavyo hali ingekuwa mbaya zaidi bila Umoja wa Mataifa”.

Tu bora zaidi tukiwa pamoja

Akirejelea kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945, Rais huyo wa Baraza Kuu amesema taasisi hiyo ilizaliwa katika “dunia iliyo katika moto na yenye haja ya kutafuta faraja.” Amekumbusha kuhusu kizazi kilichokumbwa na Vita vya Dunia viwili, ukoloni, na mabaya ya mauaji ya Holocaust, lakini kilichoamua kubadilisha njia mpya.

“Hadithi ya taasisi hii si hadithi ya ushindi wa urahisi,” amesisitiza. “Ni hadithi ya kushindwa na kuamka. Ya kujinua tena wenyewe na wengine na kujitahidi zaidi.”

 Kukabili changamoto

Rais Baerbock amesisitiza kuwa kuna changamoto za sasa zisizo na mipaka kuanzia janga la afya, mabadiliko ya tabianchi hadi akili Mnemba ambazo hakuna taifa linaloweza kushughulikia peke yake.

“Duniani hii iliyounganishwa kidijitali, ama tunashirikiana au tunateseka peke yetu,” ameonya. “Ungejisikiaje ukienda kwenye ndege ikiwa hakungekuwa na Shirika la Usafiri wa Anga la Kimataifa?Watoto wako wangejisikiaje ikiwa AI haiko chini ya udhibiti?”

Amewahimiza viongozi kukumbatia kaulimbiu ya Mkutano wa 80: “Tu Bora Pamoja: Miaka 80 na Zaidi kwa Amani, Maendeleo, na Haki za Binadamu.”

Ni wakati wa kutenda au kupoteza

Akieleza wakati huu kama hatua ya kukomaa au kushindwa, Rais huyo amesisitiza nchi wanachama kuunga mkono kikamilifu mageuzi ya Umoja wa Mataifa na kutekeleza Mkataba wa zama Zijazo. “Tunahitaji kuwa na Umoja wa Mataifa unaoweza kubadilika, unaotumika kwa gharama nafuu, na unaofaa kwa madhumuni,” amesisitiza.

“Kuwaacha mamilioni ya watu wakikalia umaskini wa kina, wakiwa hatarini kwa majanga, na wakikosa haki zao za binadamu sio tu kushindwa kimaadili. Ni njia ya kutengeneza vurugu za kimataifa,” amesema akiongeza kuwa “Kwa maneno rahisi, bila Malengo ya Maendeleo Endelevu, hakuna amani ya kudumu.”

Wito kwa viongozi

Mwisho, Rais Baerbock ameonesha kuwa uchaguzi ujao wa Katibu Mkuu anayefuata ni kipimo kingine cha uaminifu wa Umoja wa Mataifa, akibainisha kuwa taasisi hiyo haijawahi kumteua mwanamke.

“Utashtuka kuona, kati ya wagombea bilioni nne, hakuna mmoja aliyetegemewa?” ameuliza.

“Kama miaka 80 iliyopita, tunasimama katika njia ya mgongano,” amehitimisha. “Ni jukumu letu kuonyesha uongozi sawa na wa awali kuchukua hatua pale ambapo ni muhimu, kuenzi kanuni za Katiba yetu, kuwa bora pamoja, na kuonesha watu duniani kuwa Umoja wa Mataifa uko leo, kesho na kwa vizazi vinane vijavyo.”