Viongozi wa UN watoa wito wa hatua mpya za kusongesha SDGs
Viongozi wa UN watoa wito wa hatua mpya za kusongesha SDGs
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito kwa viongozi wa dunia kuimarisha tena dhamira ya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs, akionya kuwa maendeleo hayategemei ukosefu wa rasilimali bali ni juu ya maamuzi ya serikali.
“SDGs zinafuata sheria ya faida zinazoongezeka,” amesema kwenye tukio la ngazi ya juu kuhusu Malengo ya Maendeleo Ebnndelevu la “Wakati wa SDGs: kutimiza ahadi”. Lililofanyika leo Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
Ameongeza kuwa “Kadiri tunavyosonga mbele kwenye kila lengo ndivyo inavyokuwa rahisi kufanikisha mengine. Na kasi inajengeka.”
Akieleza vipaumbele vya matumizi ya dunia, Guterres amesisitiza, “Mwaka 2024, matumizi ya kijeshi duniani yalikuwa mara kumi na tatu ya misaada rasmi ya maendeleo. Hiyo ni sawa na Pato la Taifa lote la bara la Afrika. Kwa maneno mengine, hii siyo suala la rasilimali ni suala la uchaguzi.”
Maendeleo yamepatikana, lakini pengo bado lipo-Baerbock
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa , Annalena Baerbock, ameeleza hatua zilizopatikana tangu mwaka 2015, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa vifo vya watoto kwa nusu, nishati mbadala kuzalisha zaidi ya asilimia 40 ya umeme duniani, karibu watu bilioni moja kupata maji salama ya kunywa, na ulinzi wa hifadhi ya jamii kufikia zaidi ya nusu ya binadamu.
Hata hivyo, ameonya kuwa ni asilimia 35 pekee ya malengo ya SDGs yako kwenye mkondo sahihi, huku karibu nusu yaani asilimia 47 yakionesha maendeleo duni na asilimia 18 yakirejea nyuma.
“Katika wakati ambapo mahitaji yanaongezeka, misaada rasmi ya maendeleo ilipungua kwa asilimia 7.1 mwaka jana,” amesema, akiongeza kuwa nchi zinazoendelea zililipa kiwango cha kuvunja rekodi cha dola trilioni 1.4 ili kuhudumia madeni ya nje mwaka 2023.
“Changamoto yetu siyo ukosefu wa suluhisho. Ni ukosefu wa ari ya kisiasa na wakati mwingine kwa makusudi ukosefu wa rasilimali,” amesisitiza Bi. Baerbock.
Wito wa kutokata Tamaa-Malkia Mathilde
Akisisitiza ujumbe huo, Malkia Mathilde wa Ubelgiji, ambaye ni Balozi wa SDGs wa Umoja wa Mataifa, amesema, “Hatuwezi kumudu kukata tamaa. Ni muhimu zaidi katika kipindi kigumu kama hiki kuwajibika na kuunganisha juhudi zetu ili kutimiza malengo na thamani tulizokubaliana mwaka 2015.”
Tukio la Wakati wa SDG 2025 limefanyika katika nusu ya Muongo wa Hatua wa Umoja wa Mataifa, ikielezwa kuwa ni hatua muhimu ya kuharakisha maendeleo na kuthibitisha tena ari ya mshikamano wa kimataifa.
Viongozi kutoka Afrika, Asia na Pasifiki, Ulaya, Amerika ya Kusini na Karibea, pamoja na nchi ndogo za visiwa, wameshiriki majadiliano ya kimkakati kuhusu maendeleo ya SDGs na mikakati ya kufanikisha Ajenda ya 2030.
Kikao hicho cha ngazi ya juu kilifuatiwa na jukwaa la wadau wengi lililowakutanisha vijana, viongozi wa biashara, wanawake, watu wenye ulemavu, na wawakilishi kutoka maeneo yenye mizozo, kwa lengo la kuhamasisha hatua za haraka na uwekezaji mahsusi ili kuhakikisha maendeleo yanaunda mustakabali wa haki, shirikishi na endelevu kwa wote.