Mkutano wa UN wasukuma suluhisho ya mataifa mawili wakati mataifa zaidi yakitambua Palestina
Mkutano wa UN wasukuma suluhisho ya mataifa mawili wakati mataifa zaidi yakitambua Palestina
Mkutano wa ngazi ya Juu wa kimataifa kuhusu utatuzi wa amani wa suala la Palestina umefunguliwa leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, chini ya uenyekiti wa pamoja wa Ufalme wa Saudi Arabia na Ufaransa.
Marais na wakuu wa serikali wamekusanyika kuthibitisha tena makubaliano ya kimataifa juu ya suluhisho la mataifa mawili na kusukuma hatua madhubuti, zilizoratibiwa na zenye muda maalumu ili kumaliza mzozo wa muda mrefu wa Mashariki ya Kati.
Mkutano huu unafanyika wakati ambapo mataifa mengi yanaendelea kutambua rasmi Taifa la Palestina, huku mengine yakitangaza msimamo huo wakati wa kikao hicho.
Kutambuliwa kwa Palestina kunazidi kuongezeka
Kasi ya mataifa kuitambua Palestina imeongezeka katika siku za hivi karibuni. Uingereza, Canada, Australia na Ureno jana zilijiunga na orodha ya mataifa yaliyotangaza hadharani kutambua Palestina, hatua inayotafsiriwa kama mabadiliko makubwa ya kidiplomasia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, akizungumza kwenye mkutano huo amesisitiza kuwa taifa la Palestina ni haki, si zawadi, na kukataa hoja kwamba utambuzi huo unatia nguvu misimamo mikali.
Hali haiwezi kuvumilika na inazidi kuwa mbaya
Katika hotuba yake, Guterres ameonya kwamba hali ilivyo Gaza na eneo zima “haiwezi kuvumilika na inazidi kuzorota kila saa,” akisisitiza haja ya kuchukua hatua za haraka.
Katibu Mkuu pia amekaribisha ahadi zilizotolewa na baadhi ya Mataifa Wanachama za kuitambua Palestina, akibainisha kuwa hatua hizo zinaimarisha uungwaji mkono kwa mfumo wa suluhisho la mataifa mawili.
Mataifa mawili huru na yenye mamlaka
Guterres amesisitiza tena kwamba njia pekee ya amani ya kudumu ni kuanzishwa kwa mataifa mawili la Israel na la Palestina yaliyo huru, ya kidemokrasia, yanayoweza kusimama, yenye mipaka inayoendelea, na yenye mamlaka kamili, yakishi kwa amani na usalama, na kuunganishwa kikamilifu katika jumuiya ya kimataifa.
Amehitimisha kwa kusema kuwa utaifa wa Wapalestina ni haki, si zawadi, na akaonya kwamba kukanusha haki hiyo kutakuwa zawadi kwa makundi yenye misimamo mikali kila mahali.
Macron: Utambuzi ndio njia pekee ya amani
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza kuwa Ufaransa sasa inaitambua rasmi Palestina kama taifa. Katika hotuba yake katika mkutano huo, amesisitiza kuwa haki za Wapalestina hazipunguzi usalama wala uhalali wa Israel.
“Utambuzi wa haki halali za wananchi wa Palestina hauondoi haki za wananchi wa Israeli, ambazo Ufaransa imetetea tangu mwanzo,” amesema Macron. “Utambuzi huu ndio suluhisho pekee litakalowaletea Israeli amani na ushindi dhidi ya Hamas na wale wote wanaochochea chuki na uhasama.”
Saudi Arabia yatoa wito wa hali mpya Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud, amepongeza mataifa yaliyotambua Palestina na kuyataka mengine kufuata nyayo zao. Amesisitiza kuwa hali mpya ya kisiasa inahitajika itakayohakikisha amani, uthabiti na ustawi wa kanda hiyo.
Abbas alaani uvamizi wa Israel na mashambulizi ya Hamas
Akizungumza kwa njia ya video, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ametoa wito wa mazungumzo ya dharura na Israel “kumaliza umwagaji damu na kuleta amani ya kina.”
Ameelaani “uhalifu wa uvamizi wa Israel na pia mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba 2023 kusini mwa Israel”. Abbas ametangaza kuwa Hamas haitakuwa na nafasi katika serikali ya Palestina ya baadaye, akisisitiza kuwa makundi yote lazima yakabidhi silaha zao kwa Mamlaka ya Palestina ili kuunda “taifa moja halali, lenye umoja na sheria moja.”