Miaka 30 ya Azimio la Beijing, Umoja wa Mataifa washerehekea mafanikio katika haki za wanawake
Miaka 30 ya Azimio la Beijing, Umoja wa Mataifa washerehekea mafanikio katika haki za wanawake
Wanawake
Kumekuwa na maendeleo, lakini changamoto nyingi bado zipo, hii ndiyo msingi mkuu wa hotuba zilizotolewa katika mkutano wa ngazi ya juu wa kuadhimisha miaka 30 ya Azimio la Beijing kuhusu Haki za Wanawake leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Usawa wa kijinsia umekuwa kitovu cha mjadala kwa wajumbe waliowasili New York, Marekani kushiriki katika mijadala ya jumla ya kisera ya Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rais wa Baraza Kuu amesema kuwa kuna pengo kubwa la usawa ambalo bado halijapatiwa suluhisho. Kauli ‘anakimbia kama msichana’ hutumika kama tusi,” Annalena Baerbock amebainisha. “Viongozi wanawake wenye sifa kubwa hupewa jina la ‘alama za utofauti,’ ilhali kiongozi mwanamke wa dunia hukosolewa mitandaoni si kwa hotuba aliyotoa, bali kwa kuvaa viatu virefu visivyofaa. Haya yote yakitokea, tunatambua kuwa safari bado ni ndefu.”
Hakuna hata nchi moja duniani ambapo wanawake wako sawa kabisa na wanaume. Na bado kuna maeneo mengi ambapo hata kuzungumza tu kuhusu haki za wanawake kunaweza kugharimu maisha,” ameongeza.
Baerbock ametoa takwimu za kutisha kuhusu ukatili na haki za uzazi. “Mwanamke mmoja kati ya watatu duniani atakumbwa na ukatili wa kingono angalau mara moja katika maisha yake. Mmoja kati ya watatu,” amesema. “Kutekeleza ahadi za Beijing, uamuzi huu wa mapinduzi, pia kunamaanisha hakuna mwanasiasa mwanaume, jaji au kiongozi wa dini anayeweza kuthubutu kuwaambia wasichana wetu wafanye nini na miili yao, kwa sababu wao ni binadamu, si mali. Hii ni miili yetu. Ni chaguo letu.”
Amesisitiza kuwa kufanikisha usawa wa kiuchumi kunaweza kuchukua zaidi ya karne moja. “Kwa mwendo wa sasa, itachukua miaka 123,” Baerbock amesema. “Kufunga pengo la kijinsia kutaongeza pato la dunia kwa dola trilioni saba.”
Katibu Mkuu wa UN atoa wito wa kuharakisha maendeleo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameliita Azimio la Beijing “ahadi kubwa zaidi ya kisiasa ya kimataifa kuhusu haki za wanawake kuwahi kutolewa.” Amesema limechangia maendeleo katika elimu, afya ya mama na ulinzi wa kisheria: “Hata hivyo, maendeleo haya yamekuwa ya polepole na yasiyo sawa. Na hakuna nchi ambayo imefanikisha usawa kamili kwa wanawake na wasichana. Lengo la 5 la Maendeleo Endelevu usawa wa kijinsia lipo mbali sana na kufanikishwa.”
“Tuwe wazi: haki na fursa sawa si suala la kisiasa za vyama,” amesisitiza. “Ni sharti la kimataifa na msingi wa amani, ustawi na maendeleo.”
Guterres amekumbusha kuwa mwaka huu, serikali zimeidhinisha tena dhamira yao kwa Jukwaa la Beijing. “Tume ya Hali ya Wanawake imepitisha Azimio jipya la Kisiasa, likiahidi utekelezaji wa haraka na kamili wa Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji,” amesema. “Sasa ni lazima nchi zote zitekeleze ahadi hizi. Tunahitaji msaada wazi na usio na mashaka katika ngazi ya juu kabisa na mipango halisi inayoungwa mkono na uwekezaji wa kweli.”
Wasilisheni mipango yenu
Katibu Mkuu amebainisha kuwa miaka 80 iliyopita Mkataba wa Umoja wa Mataifa ulithibitisha haki sawa za wanaume na wanawake, na miaka 30 iliyopita Azimio la Beijing lilithibitisha haki za wanawake kama haki za binadamu.
“Leo hapa ukumbini, lazima tusikie jinsi mnavyokusudia kuyageuza matarajio haya kuwa uhalisia: tangazeni ahadi zenu. Wasilisheni mipango yenu. Pamoja, tufanikishe usawa kwa wanawake na wasichanausawa ambao dunia yetu inauhitaji sana,” António Guterres amehitimisha.
Mifumo ya kulinda haki za wanawake inavunjwa
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake, UN Women, Sima Bacchus, yeye ameonya kuwa mifumo iliyoundwa kulinda haki za wanawake inazidi kudhoofishwa. “Njia ambazo zilipaswa kukuza na kufadhili usawa wa kijinsia zinaporomoshwa kimyakimya lakini kwa makusudi,” amesema. “Hii siyo tu kurudi nyuma. Ni kujiondoa kabisa. Lakini mustakabali haujaamuliwa. Njia nyingine inawezekana.”
Mkutano wa Beijing wa mwaka 1995 uliwaleta pamoja wawakilishi kutoka serikali 189 na maelfu ya washiriki, ambao walipitisha Azimio na Jukwaa la Utekelezaji lililoeleza malengo ya kimkakati katika maeneo 12 muhimu kuanzia elimu na afya hadi kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Baada ya miaka 30, viongozi wa Umoja wa Mataifa wameonesha kuwa changamoto kuu inabaki kuwa jinsi ya kuyageuza matarajio haya kuwa uhalisia.