Wakalimani wa Umoja wa Mataifa katika Dunia inayoongozwa na AI
Wakalimani wa Umoja wa Mataifa katika Dunia inayoongozwa na AI
Kwa mtazamo wa haraka, kazi yao huenda ikaonekana kana kwamba haipo lakini hakuna kikao cha Baraza Kuu, Baraza la Usalama, mkutano au jukwaa la Umoja wa Mataifa linaloweza kuendelea bila wao. Mjadala wa Ngazi ya Juu ulioanza 22 Septemba unakutanisha karibu wakuu wa nchi na serikali 150, haungewezekana pia bila wakalimani wa lugha za moja kwa moja wanaowezesha viongozi wa dunia kuelewana papo kwa papo.
Mara nyingi, kazi yao huhitaji ubunifu wa haraka kwa kuwa hotuba nyingi hazitolewi mapema na wajumbe.
Kabla ya kuanza kwa Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Liudmila Blagonravova wa Idhaa ya Kirusi ya Umoja wa Mataifa amezungumza na wakalimani Anna Kadysheva (Mkalimani wa Kiingereza) na Sergei Gogin (Mkalimani wa Kirusi) kuhusu jinsi walivyojiandaa kwa tukio hili kubwa na namna zana mpya za akili mnemba zinavyoathiri kazi yao.
Kuwa daima na taarifa
Kwa wingi wa vikao na mikutano itakayofanyika wakati wa Mjadala Mkuu, idadi ya wakalimani wa UN pekee haitoshi. Ili kukidhi mahitaji, watumishi kutoka huduma nyingine za lugha huunganishwa, wakiwemo watafsiri wa nyaraka na wafanyakazi wa kuripoti kwakutumia maneno.
“Wenzetu kutoka huduma za lugha wanasaidia sana wakati mzigo wa kazi ni mkubwa,” amesema Kadysheva.
Wakalimani pia hujiandaa binafsi kwa kufuatilia hali za kisiasa na hotuba za awali.
“Ni lazima tuwe na uelewa mpana wa mambo ya sasa. Mkalimani ni lazima uwe na tarifa daima,” amesema Gogin.
AI ni tishio au nyenzo?
Pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya akili mnemba- AI, wengine wamehofia kwamba kazi ya utafsiri inaweza kutoweka. Hata hivyo, huduma za tafsiri za UN zinaamini binadamu bado hawana mbadala.
“Katika muktadha wa hali ya juu kama vile mikutano ya Umoja wa Mataifa, ambapo kila neno ni muhimu na lina maana, mkalimani maalumu ambaye ni binadamu ni lazima. Uangalizi wa kibinadamu unahitajika, hasa kutokana na uchezaji wa maneno usioweza kutafsiriwa, lugha ya picha, kejeli, AI bado inapambana na hayo yote,” amesema Kadysheva.
Akiunga mkono suala hilo Gogin akaongeza kuwa “Kazi hii itakuwa ni ushirikiano kati ya mashine na binadamu. Kwa sasa haiwezekani kuiachia akili mnemba pekee, hasa katika vikao vya siri vinavyohusu mikataba ya kimataifa.”
Usaidizi wa kidijitali
Kwa sasa, wakalimani hutumia akili mnemba kuandaa mikutano, ikiwemo kutengeneza kamusi maalum za istilahi.
“Akili mnemba hutuandalia msamiati wa kiufundi kwa sekunde chache. Bila teknolojia hii, tafsiri ya papo kwa papo ingekuwa ngumu zaidi,” amesema Kadysheva.
Kwa upande wake Gogin amebainisha kuwa akili mnemba inarahisisha maandalizi:
“Badala ya kupitia nyaraka zote, tunaweza kuomba muhtasari au hoja kuu za ripoti.”
Kila sekunde ni muhimu
Kadysheva amesema wakati mwingine hawapewi hotuba mapema, na hapo akili mnemba husaidia kuelewa msimamo wa nchi au muktadha wa mjadala. Aidha, maendeleo ya kidijitali yamepunguza changamoto za kusubiri nakala za karatasi dakika ya mwisho.
“Sasa hotuba zikishapatikana, tunazipokea mara moja mtandaoni. Kila sekunde tunayookoa ni ya thamani kubwa.”
Huduma za utafsiri za Umoja wa Mataifa zinaendelea kuleta pamoja utaalamu wa kibinadamu na uwezo wa zana za kisas aza teknolojia, kuhakikisha kuwa hotuba za viongozi zinatafsiriwa kwa usahihi na kwa wakati jambo ambalo ni muhimu kwa mawasiliano ya kimataifa katika mjadala wa Ngazi ya Juu.