Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama la UN lakutana kwa dharura kujadili tukio la ndege za kivita za Urusi nchini Estonia

Mtazamo mpana wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wanachama wanakutana juu ya vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa.
UN Photo/Manuel Elías
Mtazamo mpana wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wanachama wanakutana juu ya vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa.

Baraza la Usalama la UN lakutana kwa dharura kujadili tukio la ndege za kivita za Urusi nchini Estonia

Amani na Usalama

Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa leo limeitisha kikao cha dharura kufuatia uvunjaji wa Urusi wa sheria za anga ya Estonia. “Ukiukaji wa sheria za anga za nchi huru haukubaliki.” Kauli hii ilitolewaleo kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Msaidizi wa Katibu Mkuu, Miroslav Jenča. Sababu ya kikao hicho ni tukio lililotokea Septemba 19, ambapo, kwa mujibu wa Estonia, ndege tatu za kivita aina ya MiG-31 za Urusi zilivunja sheria na kuingia katika anga yake.

Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Estonia, ndege hizo ziliingia anga ya nchi hiyo bila kibali na bila mipango ya safari, hali ambayo ingeweza kutishia ndege zingine. Kufuatia tukio hilo, ndege za kivita za Italia aina ya F-35, zinazoshiriki katika jukumu la NATO kulinda anga ya Estonia, ziliondoka kukabiliana nazo.

Mamlaka za Estonia zimesema kuwa huu ni uvunjaji sheria wa tano kwa anga yake unaofanywa na Urusi mwaka 2025, na zimeomba mashauriano na washirika wa NATO.

Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imedai kwamba safari hiyo ilifanyika kwa kufuata njia iliyoidhinishwa juu ya maji ya kimataifa ya Bahari ya Baltiki, zaidi ya kilomita tatu kutoka kisiwa cha Vaindloo, na haikuvunja sheria ya anga ya Estonia.

Jenča amebainisha kuwa Umoja wa Mataifa hauna uthibitisho wa madai hayo. Amesisitiza kwamba tukio la Estonia si la pekee. Mapema Septemba, uvunjaji wa sheria kuingia anga za Poland na Romania na ndege zisizo na rubani za Urusi ulishuhudiwa.

Msaidizi wa Katibu Mkuu Miroslav Jenča akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa.
UN Photo/Manuel Elías
Msaidizi wa Katibu Mkuu Miroslav Jenča akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa.

Mwisho wa hotuba yake, Jenča ameelekeza uangalizi wa wajumbe wa Baraza la Usalama kwenye mashambulizi yanayoendelea dhidi ya Ukraine. Kwa mujibu wa mamlaka za Ukraine, ndani ya wiki moja iliyopita Urusi imerusha zaidi ya ndege zisizo na rubani aina ya kamikaze 1,500, mabomu yanayoongozwa kwa ndege 1,280 na makombora 50 ya aina mbalimbali.

Mashambulizi katika maeneo ya Dnipro, Chernihiv na Khmelnytsky yamesababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia. Katika mkoa wa Belgorod nchini Urusi, mamlaka za eneo zimesema watu wawili waliuawa kutokana na mashambulizi ya Ukraine.

Miroslav Jenča amerudia wito wake wa kusitishwa kwa mapigano “kikamilifu, mara moja na bila masharti” na kueleza utayari wa Umoja wa Mataifa kusaidia juhudi zozote za maana kuelekea “amani ya haki, ya kudumu na ya kina.”

Shirikisho la Urusi: Ndege za Urusi hazikuvuka sheria ya anga ya Estonia

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyansky, amesema kuwa Septemba 19, ndege tatu za kivita za Urusi aina ya MiG-31 zilifanya “safari iliyopangwa kutoka Karelia kuelekea uwanja wa ndege ulioko katika mkoa wa Kaliningrad, ambayo ilifanyika kwa kufuata kanuni za kimataifa za matumizi ya anga.”

Kwa mujibu wake, ndege hizo hazikupotoka katika njia iliyokubaliwa wala kuvuka anga ya Estonia, na njia yake ilipita juu ya maji ya kimataifa ya Bahari ya Baltiki.

“Iwapo Estonia ingetaka, wangeweza kujiridhisha wenyewe. Lakini Tallinn haina nia hiyo, lengo ni tofauti  kinyume na ukweli na akili ya kawaida, kuibua hofu na kuishutumu Urusi kwa uchokozi,” amesema Polyansky.

Marekani: Tutalinda kila kipande cha ardhi ya NATO

Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, katika hotuba yake ya kwanza kwenye Baraza la Usalama, amelaani vitendo vya Urusi, ambavyo kwa mujibu wake “tena vimevunja sheria za anga za nchi wanachama wa NATO.”

Amekumbusha kuwa siku tisa zilizopita, Baraza lilijadili tukio la ndege zisizo na rubani za Urusi juu ya anga ya Poland, na Septemba 19 kulitokea tukio jipya ambapo ndege tatu za kivita za Urusi ziliruka maili 10 za baharini ndani ya anga ya Estonia.

“Marekani na washirika wetu tutalinda kila kipande cha ardhi ya NATO. Urusi lazima ikome mara moja mwenendo huu hatari,” amesisitiza mwanadiplomasia huyo wa Marekani.

Waltz amesema hatua kama hizi za Moscow zinaweza kuonesha ama nia ya kuongeza mzozo na kuhusisha nchi nyingi zaidi vitani, au udhaifu wa udhibiti juu ya wanaoendesha ndege za kijeshi. Ametoa wito kwa Urusi “kuheshimu amani na usalama wa kimataifa, kuheshimu mamlaka ya majirani na kujiepusha na uvunjaji wa sheria za anga zao.”

Mwakilishi huyo wa Marekani alibainisha kwamba Marekani, pamoja na Rais Trump, inaendeleza “juhudi kubwa za kumaliza vita hivi vibaya,” na akasisitiza tena kwamba Moscow ianze mazungumzo ya moja kwa moja na Kyiv.

Estonia: Tuna ushahidi usiopingika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Margus Tsahkna, amewasilisha picha za rada mbele ya Baraza la Usalama, ambazo kwa mujibu wake zinaonesha ndege za kivita za Urusi katika maeneo yake.

“Walionya,” amesema, akiongeza kuwa kulikuwa na ishara za wazi kupitia njia zote, lakini “hakukuwa na majibu.” Waziri amesisitiza kuwa “ukiukaji huu wa sheria za anga ni wa wazi kabisa, na Urusi inasema uongo tena kama ilivyofanya mara nyingi.”

Amekumbusha uvamizi wa Georgia mwaka 2008, uvamizi wa Crimea mwaka 2014 na uchokozi dhidi ya Ukraine mwaka 2022, akitoa wito kwa Shirikisho la Urusi “Kwa hiyo tafadhali, msiseme uongo tena tuna ushahidi usiopingika.”