Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kijana mkimbizi aeleza faida na changamoto za msaada wa UN nchini Uganda

Bahati (kulia), ambaye alikimbilia Uganda mwaka 2008 kutokana na vita mashariki mwa DRC akizungumza na John Kibego (kushoto) kutoka Radio washirika wetu Kazi-Njema FM iliyoko mjini Hoima.
UN News
Bahati (kulia), ambaye alikimbilia Uganda mwaka 2008 kutokana na vita mashariki mwa DRC akizungumza na John Kibego (kushoto) kutoka Radio washirika wetu Kazi-Njema FM iliyoko mjini Hoima.

Kijana mkimbizi aeleza faida na changamoto za msaada wa UN nchini Uganda

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake, Bahati Yoane, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi katika kambi ya Kyangwali nchini Uganda, ametoa ushuhuda wa jinsi shirika hilo limekuwa msaada mkubwa katika maisha yake, huku pia akieleza changamoto zinazowakabili wakimbizi nchini Uganda.

Moja ya mchango mkubwa unaotolewa na Umoja wa Mataifa kwa dunia tangu ulipoanzishwa mwaka 1945 ni kusaidia mamilioni ya watu wanaolazimika kufungasha virago kukimbia makwao na kuwa wakimbizi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita.

Uganda ni moja ya nchi zinazohifadhi maelfu ya wakimbizi wengi kutoka Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wakisaidiwa chini ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na mengine.

John Kibego kutoka Radio washirika wetu Kazi-Njema FM iliyoko mjini Hoima amepata fursa ya kuzungumza na mmoja wa wakimbizi hao akielezea mchango mkubwa wa Umoja wa Mataifa kwake.

Mashirika ya UN yamekuwa muhimu kwangu-Bahati

Bahati, ambaye alikimbilia Uganda mwaka 2008 kutokana na vita mashariki mwa DRC, amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa nguzo muhimu katika maisha yake. “Wamenisaidia kusoma kuanzia shule ya msingi, sekondari hadi mafunzo ya kuendesha gari. Pia nimefaidika na msaada wa chakula kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP,” amesema.

Kwa mujibu wa Bahati, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani UNHCR limemsaidia kupata mafunzo na leseni ya udereva, hatua aliyosema imebadilisha maisha yake. “Nimeweza kusimama mwenyewe kwa sababu ya msaada huu,” ameongeza.

Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, kijana huyo ameeleza changamoto kubwa zinazokabili wakimbizi nchini Uganda. Anasema ongezeko la idadi ya wakimbizi, ambao sasa ni zaidi ya milioni moja wengi wao wakitoka DRC limepelekea kupungua kwa rasilimali kama ardhi ya kulima na mgao wa msaada wa chakula.

Msaada kwa wakimbizi umepungua

“Awali tulikuwa na mashamba ya kutosha, lakini sasa yamepungua. Pia msaada wa chakula umepungua kwa sababu wakimbizi wameongezeka,” ameeleza Bahati, akitoa wito wa msaada zaidi kwa wakimbizi.

Aidha, Bahati amesema kuwa pamoja na msaada mkubwa anaopokea, angetamani kuona Umoja wa Mataifa ukiongeza juhudi za kurejesha amani nchini kwake ili wakimbizi wengi waweze kurejea nyumbani. “Ni vyema kuwa salama hapa Uganda, lakini heri zaidi kama tungekuwa salama nyumbani kwetu,” amesema.

Uganda kwa sasa inahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi barani Afrika, ikiwemo wakimbizi kutoka Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, huku vita mashariki mwa Congo vikionekana kuendelea licha ya jitihada za kimataifa kutafuta suluhu ya kudumu.