Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi 2025 ni njia kuelekea COP30
Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi 2025 ni njia kuelekea COP30
Mafuriko Kusini mwa Asia, moto wa nyika Amerika Kaskazini, na joto la kihistoria barani Ulaya vimeonesha kile ambacho wanasayansi wameonya kwa miaka mingi, mabadiliko ya tabianchi yanazidi kasi kuliko hatua za kisiasa za kuyakabili.
Katika muktadha huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameaandaa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wakati wa wiki ya ngazi ya juu ya Mjada Mkuu wa Baraza Kuu, akizitaka nchi kuongeza ahadi zao za tabianchi kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP30 utakaofanyika mwezi Novemba mjini Belém, Brazil.
Mkutano huo, umnaofanyika leo tarehe 22 Septemba katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, umeundwa kama jukwaa la kuanzisha mkutano wa COP30, lakini tofauti na mazungumzo mapana ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi huu ni mkutano wa ngazi ya juu mahsussi, ambapo Wakuu wa Nchi, viongozi wa Serikali, biashara, na jumuiya za kiraia wanatarajiwa kuwasilisha ahadi thabiti na mipango mipya ya kitaifa ya tabianchi.
Hatua thabiti kwa muongo ujao
Kwa mujibu wa waandaaji, mkutano huu una jukumu la wazi, wahusika wa Mkataba wa Paris makubaliano muhimu ya 2015 ya mabadiliko ya tabianchi lazima walete mipango yao mipya NDCs au iliyorekebishwa ambayo ni Michango Iliyopangwa ya Kitaifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi inayoakisi “hatua thabiti kwa muongo ujao.”
Katibu Mkuu António Guterres amesisitiza bayana kuwa ahadi zilizopo hazitoshi hata kidogo, na ni sehemu ndogo tu ya nchi wanachama walio na NDCs zilizorekebiishwa kwa 2025. Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi UNFCCC, mipango ya kitaifa ya sasa itapunguza tu hewa chafuzi duniani kwa asilimia 2.6 kufikia 2030 ikilinganishwa na viwango vya 2019 ikiwa ni kiwango kidogo mno dhidi ya upunguzaji wa asilimia 43 ambao wanasayansi wanasema unahitajika ili kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi 1.5 Celsius juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.
Hivyo basi, mkutano huu ni shinikizo na pia fursa. Viongozi wanatarajiwa si tu kurudia ahadi, bali pia kutangaza NDCs mpya, kuonesha jinsi zitakavyotekelezwa, na kusisitiza jinsi zinavyolingana na mchakato wa kasi wa nishati safi.
Kwa nini sasa?
Uharaka wa mkutano huu umeimarishwa na hali za kisayansi na kisiasa. Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani WMO limeripoti kuwa 2024 ulikuwa mwaka wenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa, kwa wastani wa nyuzi 1.6 Celsius juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda. Wakati huohuo, mazingira ya kisiasa kimataifa yamegawanyika zaidi.
Marekani, ambayo ilijiondoa kwenye Mkataba wa Paris mapema 2025, bado ni miongoni mwa wachafuzi wakubwa kihistoria. Kujitoa kwake kwenye ufadhili wa tabianchi na ahadi za nishati safi kumeacha mataifa yanayoendelea yakijiuliza kama msaada ulioahidiwa utawafikia.
Hata hivyo, kasi ya kweli ipo. Uwekezaji katika nishati safi ulifikia zaidi ya dola trilioni 2 mwaka 2024, ukizidi mafuta ya kisukuku kwa mara ya kwanza, na mipango kama vile Mkataba wa Kukomesha Kuzalishwa kwa Mafuta ya Kisukuku unapata nguvu. Mkutano huu utajaribu kubaini kama mwenendo huu chanya unaweza kuendelezwa na kupanuliwa.
Mambo ya kuzingatia
Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi si kikao cha mazungumzo ya makubaliano, lakini matokeo yake yataweka mwelekeo wa COP30 huko Belém. Brazil imeahidi kuuweka mkutano huo kwenye haki ya tabianchi, ulinzi wa misitu, na nishati mbadala. Lakini mafanikio huko Belém yatategemea kwa kiasi kikubwa kinachotokea New York wiki hii.
Wachambuzi wataangalia ishara tatu kuu, Kwanza, je, wachafuzi wakubwa wataleta mipango itakayoziba pengo la uzalishaji? Pili, je, ufadhili wa tabianchi utaongezeka zaidi ya ahadi za ishara tu, hasa kwa Mfuko wa Hasara na Uharibifu ambao umepokea chini ya dola milioni 789 pekee? Na mwishowe, je, viongozi watakubali kwamba upanuzi wa matumizi ya makaa ya mawe, mafuta, na gesi hauendani na malengo ya Paris?
Bila maendeleo kwenye maeneo haya, COP30 inaweza kuwa tena jukwaa la matarajio yasiyotimizwa.
Mikakati yenye hatari kubwa
Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mkutano huu ni zaidi ya mchakato. Ni kuhusu kujenga upya imani katika mshikamano wa kimataifa wakati dunia inazidi kugawanyika, na kuthibitisha kwamba hatua za mabadiliko ya tabianchi zinaweza kufungua manufaa ya kiuchumi na kijamii.
“Fursa za hatua za tabianchi hazijawahi kuwa wazi zaidi,” umesisitiza Umoja wa Mataifa, zikionesha uundaji wa ajira, kuboreshwa kwa afya, na usalama wa nishati unaohusiana na upanuzi wa nishati safi.
Lakini kwa jamii nchini Pakistan na India zilizohamishwa na mafuriko makubwa, au kwa wakulima katika Pembe ya Afrika wanaokabiliwa na ukame, mkutano huu si fursa bali ni suala la kuishi. Pengo kati ya athari za mabadiliiko ya tabianchi na hatua za kukabiliana nayo za kisiasa halijawahi kuonekana kuwa kubwa zaidi.
Kutoka maneno hadi vitendo
Mkutano huu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Septemba 2025 si mbadala wa COP30, lakini unaweza kuwa na umuhimu sawa. Hapa ndipo viongozi wanaweza kuweka upya malengo, kuongeza uaminifu, na kujenga kasi kuelekea Brazil.
Iwapo utazalisha ahadi mpya thabiti, ufadhili wa kuaminika, na mwelekeo wazi kuhusu mafuta ya kisukuku, unaweza kusaidia kuokoa ahadi ya Paris.
Mazungumzo ya kusaka suluhisho
Zaidi ya hotuba za wakuu wa nchi, wiki ya ngazi ya juu ya Mjada Mkuu wa Baraza Kuu itajumuisha mazungumzo ya suluhisho vikao vya mada vinavyokusanya serikali, biashara, na jumuiya za kiraia pamoja na viongozi wa kitaifa. Mazungumzo haya yatashughulikia maeneo matano muhimu:
- Kupunguza : mikakati ya kupunguza matumizi ya mafuta ya kisukuku na kuharakisha usambazaji wa nishati mbadala.
- Mnepo: kuimarisha uwezo wa jamii kustahimili mafuriko, ukame, na mawimbi ya joto yanayoathiri dunia tayari.
- Ufadhili : kuongeza ufadhili wa tabianchi kwa mataifa yanayoendelea, kuhakikisha ruzuku si mikopo pekee na kutoa msaada.
- Uadilifu wa taarifa: kupambana na upotoshaji na kuboresha uwazi wa takwimu na taarifa za tabianchi.
- Maeneo mengine mtambuka: kuanzia mifumo ya chakula hadi mabadiliko yenye haki
Uchambuzi na matangazo muhimu kutoka kwenye mazungumzo haya yataingizwa kwenye Muhtasari wa Mwenyekiti, utakaowasilishwa katika kikao cha kufunga tarehe 24 Septemba.