Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake

Mtazamo mpana wa mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la kuadhimisha miaka themanini ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe Mtazamo mpana wa mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la kuadhimisha miaka themanini ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa waadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa hii leo umeadhimisha miaka 80 tangu kusainiwa kwa Mkataba wake tarehe 26 Juni 1945, tukio lililotoa matumaini mapya kwa dunia iliyokuwa imechoka kutokana na vita kuu mbili za dunia, mauaji ya halaiki na ukoloni. Katika maadhimisho hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kumbukizi ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa ni fursa ya kukumbuka ujasiri wa waanzilishi wa taasisi hiyo na kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kukabili changamoto zinazokabili dunia hivi sasa. 

Kwaya ya Vijana ya Sing for Hope, na mpiga kinanda David Watkins, katika ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa tukio lililofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani katika Ukumbi wa Baraza Kuu, ukumbi unao wakutanisha nchi wanachama wote 193 wa Umoja wa Mataifa .

Wahudhuriaji wa tukio hili walioneshwa video fupi ya tukio la utiaji saini wa kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945 na kisha viongozi mbalimbali kuzungumza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la kuadhimisha miaka themanini ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe

Kiongozi Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alianza hotuba yake kwa kuweka taswira ya uzito wa kuanzishwa kwa shirika hilo, mathalani mfanyakazi namba mbili Major Brian Urquhart alikuwa ni mwanajeshi wa Uingereza aliyepata ulemavu katika vita vya pili ya dunia, hivyo wakati wa majadiliano kila mtu alielewa nini hasa umuhimu wa amani na kazi ya Umoja wa Mataifa katika kuimarisha amani duniani.

Lakini sasa Guterres anasema  Kuna imani potofu kwamba amani ni ujinga. Haki ni hisia na kwamba siasa halisi pekee ni siasa za madaraka na maslahi binafsi. Lakini wafanyakazi wa mwanzo wa UN walikuwa wa kweli na waliguswa na vita na walijua: Amani ni jambo la ujasiri zaidi, la kivitendo zaidi, la lazima kuliko yote. Na katika kujenga Umoja wa Mataifa, waliunda kitu cha kipekee. Mahali ambapo mataifa yote  makubwa na madogo yanaweza kuja pamoja kutatua matatizo ambayo hakuna nchi inaweza kutatua peke yake.”

Tweet URL

Kauli ya Rais wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu

Rais wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, katika hotuba yake amesema historia ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa inatufundisha kuwa hata katika giza kuu la vita na ukoloni, viongozi walichagua mshikamano na akasisitiza kuchagua matumaini badala ya kukata tamaa.

Bi. Baerbock akatoa swali kwa kila mtu kujitafakari  “Hivi leo tunawaona watoto bila wazazi wakisaka chakula Gaza, vita ikiendelea Ukraine. ukatili wa kijinsia Sudan, magenge yakitisha watu Haiti, chuki zisizochujwa mitandaoni, na mafuriko pamoja na ukame ulimwenguni kote. Je, huu ndio ulimwengu uliokusudiwa na Mkataba wetu?”

Mbali na viongozi kuzungumza mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Maria Ressa mwandishi wa habari kutoka nchini Ufilipino naye amehutubia na kusema Vita kubwa zaidi tunayokabiliana nayo leo ni kutokujali na inasababisha kudhoofisha utu wetu: katika ulimwengu wa kimwili, ambapo vita vinapamba moto kutoka Ukraine hadi Gaza; na katika ulimwengu wa mtandaoni, ambapo akili na hisia zetu zinatumiwa na maubepari katika kujipatia faida.”