Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumefika hapa UN, tafadhali tusikilizeni

Emily Mohohlo wa Slum Dwellers International akizungumza na Assumpta Massoi wa Habari za UN Kiswahili pembezoni mwa UNGA80 jijini New York.
UN News Emily Mohohlo, Mratibu wa shirika la kiraia la Slum Dwellers International kutoka Afrika Kusini, akizungumza na Assumpta Massoi kandni mwa mkutano wa UNGA80 mjini New York Marekani.

Tumefika hapa UN, tafadhali tusikilizeni

Tabianchi na mazingira

Kando ya maadhimisho ya siku ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, hapa makao makuu kumefanyika mashauriano ya faragha yenye lengo la kusaka majawabu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Mashauriano ya leo ni sehemu ya mashauriano 10 yatakayofanyika kuelekea mkutano wa tabianchi wa wakuu wa nchi na serikali utakaofanyika keshokutwa Jumatano hapa Umoja wa Mataifa. 

Idhaa hii imezungumza na mmoja wa watoa mada kwenye mashauriano hayo ambayo matokeo yake yatawasilishwa kwenye mkutano wa viongozi. 

Katika uwanda wa wageni nje ya jengo la mikutano nakutana na Emily Mohohlo, Mratibu wa shirika la kiraia la Slum Dwellers International kutoka Afrika Kusini linalojikita katika kuhakikisha maeneo ya mabanda mijini yanakuwa jumuishi, yana mnepo na maisha yao yanaboreshwa.

Na umuhimu wa mkutano huu anasema, “Mkutano huu ni muhimu kwangu kwa sababu katika maisha halisia kuna joto kupindukia na linasababisha vifo kwa wanawake na pia kutoweka kwa mbinu zao za kujipatia kipato. Hivyo kwangu naona kama tunaweza kujumuika pamoja katika ngazi ya kijamii na kupata takwimu sahihi na kisha watafiti watusaidie. Tunahitaji wabia kwani tayari tumeshachukua hatua.”

Kwa hiyo ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano?

Njooni mshirikiane nasi, kwa sababu tuna takwimu kutoka mashinani lakini hatuna uwezo wa kifedha. Tukipata fedha kutoka kwa watafiti itakuwa vema. Tunajua wana takwimu lakini si kutoka mashinani.”

Nilipomuuliza umuhimu wa Umoja wa Mataifa wakati huu unatimiza miaka 80 akafunguka.

“Ndio sasa una miaka 80, lakini bado hatuoni vya kutosha mafanikio yake mashinani. Huwezi kusaidia mtu mmoja mmoja. Waje kwenye vikundi na itakuwa vema kwa sababu kuna idadi kubwa ya watu.”

Akatamatisha na ujumbe kwa Umoja wa Mataifa.

“Tumefika hapa, tafadhali tusikilizeni. Hakuna chetu bila kutushirikisha. Asante.”