Shambulio msikiti Sudan takribani watoto 11 waripotiwa kuuawa
Shambulio msikiti Sudan takribani watoto 11 waripotiwa kuuawa
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF, Catherine Russell, ametoa taarifa leo Septemba 22 akielezea mshtuko wake kufuatia shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya msikiti ulioko kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abu Shouk, Al Fasher, Kaskazini mwa Darfur wakati wa sala ya Alfajiri siku tatu zilizopita.
"Shambulio hili dhidi ya msikiti ni la kushtua na halina msamaha," amesema Rusell.
Ameongeza kwamba, "ripoti za awali zinaonesha kuwa idadi ya watoto wasiopungua 11, wenye umri wa kati ya miaka kati ya 6 na 15, walifariki duniani katika shambulio hilo, ambalo pia limeathiri nyumba za jirani. Watoto wengine wengi wamejeruhiwa."
Kwa zaidi ya siku 500, watoto wa Al Fasher wamekuwa wakikabiliwa na mazingira magumu ya kuzingirwa na wapiganaji wa Rapid Support Forces. Watoto hao wamenaswa katikati ya mapigano, wakiwa na ugumu wa kupata chakula, maji safi na huduma za afya, na wanalazimika kushuhudia matukio ya kutisha ambayo hakuna mtoto anayepaswa kuyaona.
Mashambulizi yamelenga huduma za kibinadamu
Mbali na shambulio hilo la msikiti, Russell amefichua kuwa lori la maji linalofadhiliwa na UNICEF pia limeshambuliwa na ndege isiyo na rubani huko Al Fasher jana. Lori hilo lilikuwa likisambaza maji safi kwa watu 8,500 waliokimbia makazi yao na wagonjwa wa hospitali, ikiwemo hospitali ya Al Saudi, ambayo ni mojawapo ya vituo vichache vya afya ambavyo bado vinafanya kazi mjini humo. Hili ni lori la tatu la UNICEF kushambuliwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, jambo linalohatarisha maisha ya wafanyakazi wa kibinadamu na usambazaji wa misaada muhimu.
"Huku Al Fasher ikiwa imezingirwa, mashambulio kama haya yanaondoa uhai wa familia nyingi ambazo zinakosa maji safi, wakati utapiamlo na magonjwa kwa watoto yanaongezeka kwa kasi," amesema Russell.
"Familia za wakimbizi na hospitali sasa zinategemea karibu kabisa malori ya maji. Bila huduma hii, wengi watalazimika kutumia vyanzo vya maji visivyo salama, na kuwaweka watoto katika hatari ya kupata magonjwa hatari yatokanayo maambukizi kupitia maji machafu."
Wito wa ulinzi na uwajibikaji
Russell amesisitiza kuwa ni jambo la kusikitisha na la kinyume cha sheria kwamba watoto wanaendelea kuuawa, kujeruhiwa na kuathirika kisaikolojia katika vita ambavyo hawakuvianzisha na hawawezi kuvizuia. Nyumba zao, shule, na maeneo ya ibada, ambayo yanalindwa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu,sasa yamegeuzwa kuwa shabaha ya mashambulio.
UNICEF imezitaka pande zote zinazopigana kumaliza mashambulio haya, zitimize wajibu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, na kuhakikisha watoto wanalindwa watoto wanalindwa wakati wote.
"Maisha ya watoto yapo hatarini, na kutokujali hakuwezi kuvumiliwa. Uchunguzi wa haraka na wa kina lazima ufanyike kuhusu vitendo hivi vya kinyama, na wale wote waliohusika lazima wawajibishwe kikamilifu," amesema Russell.
"Kila mtoto ana haki ya kuwa salama. UNICEF inasimama pamoja na watoto wa Al Fasher na Sudan. Hatutachoka kudai ulinzi wao na kukuza sauti zao hadi mapigano yakome," amesisitiza Bi.Rusell.