Viongozi wa UN, AU na EU waahidi kushirikiana kwa ajili ya amani na maendeleo barani Afrika
Viongozi wa UN, AU na EU waahidi kushirikiana kwa ajili ya amani na maendeleo barani Afrika
Amani na Usalama
Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika AU na Muungano wa Ulaya EU, wamethibitisha tena dhamira yao ya kuendeleza amani na maendeleo endelevu barani Afrika, kwa kuahidi ushirikiano wa kina zaidi ili kukomesha migogoro, kuimarisha mnepo na kukabiliana na changamoto za kimataifa kuanzia madeni hadi mabadiliko ya tabianchi.
Walipokutana katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York hii leo kando ya wiki ya mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza kuu, viongozi wa mashirika hayo matatu wametoa tamko la pamoja baada ya mkutano wao wa sita wa pande tatu.
Wamesisitiza tena kuunga mkono mfumo wa kimataifa kama “njia bora zaidi ya kushughulikia changamoto za leo,” wakisisitiza utii kwa Katiba ya Umoja wa Mataifa na kuonesha wasiwasi juu ya kuongezeka kwa dharau dhidi ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu kote duniani.
Migogoro barani Afrika
Sehemu kubwa ya tamko hilo ilijikita kwenye migogoro ya Afrika, hususan vita vinavyosababisha maafa nchini Sudan, ambavyo sasa viko mwaka wa tatu. Mashirika hayo matatu yametoa wito wa kuongezwa kwa msaada wa pamoja ili kuhakikisha “kusitishwa kwa mapigano mara moja na suluhisho endelevu” kupitia mazungumzo ya kisiasa jumuishi.
Wameahidi pia uratibu madhubuti zaidi katika eneo la Sahel, ambako vurugu za makundi yenye silaha zinaendelea kuyumbisha jamii, na wakathibitisha kuunga mkono juhudi za maridhiano na maendeleo.
Kuhusu Libya, walmeidhinisha ramani ya barabara ya Umoja wa Mataifa ya kufufua mchakato wa kisiasa uliokwama, huku wakisisitiza juhudi endelevu za kushughulikia changamoto za uhamiaji kwa mujibu wa viwango vya kibinadamu.
Tamko hilo pia limeunga mkono juhudi zinazoendelea za amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, likiunga mkono Baraza la Amani na Usalama la AU pamoja na azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kuhusu Somalia, mashirika hayo matatu yamesisitiza kuunga mkono Ujumbe wa AU wa Msaada na Ustawi, na kusisitiza haja ya ufadhili endelevu ili kuhakikisha operesheni zenye ufanisi.
Ushirikiano na changamoto za kimataifa
Wakielekea mbele, UN, AU na EU wamesema wataimarisha ushirikiano wa pande tatu ili kusukuma suluhu zinazoongozwa na Waafrika kwa changamoto za amani na usalama.
Wametaja Ajenda ya Afrika 2063 na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 ya Maendeleo Endelevu kama mifumo ya mwongozo na wakabainisha maandalizi ya Mkutano wa Kilele wa AU-EU utakaofanyika Angola mwezi Novemba mwaka huu.
Viongozi hao wamesisitiza suala la ufadhili kama kipaumbele, wakitoa wito wa utekelezaji kamili wa ahadi ya Sevilla au Sevilla Commitment ili kufungua uwekezaji, kushughulikia mzigo wa madeni na kufanya mageuzi ya benki za maendeleo za kimataifa. Pia wameonya kuwa madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi yanaathiri zaidi jamii zilizo hatarini, na wakahimiza ahadi thabiti katika mkutano wa COP30 utakaofanyika Brazil mwezi Novemba mwaka huu.
Wakionesha kumbukumbu ya miaka 25 ya Azimio la Baraza la Usalama namba 1325 kuhusu wanawake, amani na usalama, wamesisitiza tena dhamira yao ya kuendeleza uongozi na ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa amani.
Afrika Isiyozuilika
Mapema leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alihutubia jukwaa la Unstoppable Africa 2025 la Mpango wa Biashara ya Afrika Duniani, lililoandaliwa na AU na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Global Compact mpango mkubwa zaidi duniani wa uendelevu wa makampuni, ukiwa na zaidi ya kampuni 18,000 na mashirika yasiyo ya kibiashara katika zaidi ya nchi 160.